Hali ilivyo miili waliokufa  ajali ya ghorofa ikiagwa

Dar es Salaam. Licha ya mvua inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam mamia ya wananchi wamejitokeza kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya ghorofa lililoporomoka eneo la Kariakoo jijini hapa.

Miili hiyo inaagwa leo Novemba 18, 2024 saa 7 mchana kwenye viwanja vya Mnazi mmoja.

Wananchi wanaendelea kujitokeza viwanjani hapa tayari kuaga miili ya wapendwa wao waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Uwanjani hapa, Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) wanaongoza kupokea waombolezaji.

Pia wapo wanajeshi ambao wamekaa wakisubiri taratibu nyingine.

Uwanjani hapo kuna eneo limewekwa meza 18 maalumu kwa ajili ya kuwekwa majeneza yenye miili na mbele ya kila meza kuna kiti kimoja hivyo kufanya idadi ya viti hivyo kuwa 18.

Aidha hadi jana usiku, ililiripotiwa watu 13 wamepoteza maisha na wengine 84 walijeruhiwa katika tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa kamati ya maafa, William Lukuvi amesema tayari utambuzi wa miili hiyo umefanyika kwa ndugu wa marehemu kuwa kuwatambua wapendwa wao.

Viongozi wa dini wakiwa viwanja vya Mnazi mmoja kuaga miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya ghorofa lililoporomoka eneo la Kariakoo.

Amesema utambuzi huo ulifanyika hospitali ambako miili ilihifadhiwa na baada ya hatua hiyo, walikubaliana iagwe leo tayari kwa maziko.

Amesema tukio la kuaga litakaloongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuanzia saa 7 mchana.

Hata hivyo hadi asubuhi ya leo, shughuli ya uokozi inaendelea huku wapita njia na wafanyabiashara katika eneo la Msimbazi na Mchikichini, wasiohusika kwenye tukio la uokozi wakizuiwa kusogelea eneo hilo.

Magari ya umma na binafsi pia yamezuiwa kupita kwenye eneo hilo ambalo limefungwa utepe kuanzia jirani na kilipo kituo cha mafuta cha Big Bon hadi mataa ya Gerezani.

Related Posts