Katika kila uchaguzi, jamii ina nafasi ya kipekee ya kuamua mustakabali wake kwa kuchagua viongozi watakaosukuma mbele maendeleo na kuboresha maisha ya watu.
Kuchagua viongozi wenye maadili, uwajibikaji na maono kunatoa mwanga wa maendeleo endelevu katika jamii.
Katika ulimwengu wa sasa ambako aghalabu maadili ya uongozi yamekuwa yakididimia ni muhimu kwa wananchi kuelewa mambo ya kuzingatia ili kupata viongozi bora.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari anasema mara nyingi kunakuwa na hamasa katika uchaguzi wa mkuu kuliko wa Serikali za mitaa.
“Uchaguzi wa viongozi wenye tija ni msingi wa maendeleo ya jamii. Bila uongozi thabiti na wenye maadili, rasilimali za umma zinapotea na tunakosa maendeleo ya kweli na elimu inahitajika katika uchaguzi huu kwa wananchi,” anasema Profesa Bakari.
Anasema kwa sasa kumekuwa na watu wengi wenye uwezo wa kuongoza tofauti na zamani, walioelimika walikuwa wachache.
Katika kipindi hicho, mwanazuoni huyo anasema wasomi wengi waliishia kidato cha nne au darasa la saba.
Profesa Bakari anasema wananchi wanatakiwa kuzigatia vitu muhimu kwa wagombea kipindi cha kampeni ili kuwasaidia kupata mtu sahihi atakayewaongoza.
Kigezo cha kwanza kinachopaswa kuzingatiwa ni uadilifu wa kiongozi, kwa kuwa viongozi wenye maadili wana nafasi nzuri ya kuboresha jamii.
“Jamii inahitaji viongozi ambao wanaweka mbele masilahi ya watu na si ya kibinafsi. Uadilifu ni msingi wa kiongozi anayetamani kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi,” anasema Profesa Bakari.
Historia ya kiongozi husika ni jambo lingine lililotajwa na Profesa Bakari, linalopaswa kutumika katika kupima uwezo wa kiongozi.
Anasema uongozi bora unahitaji uwazi na uwajibikaji. Viongozi wanaoweka wazi uamuzi wao wanajenga imani kwa wananchi. Kiongozi anayetoa maelezo ya wazi kuhusu uamuzi wake hupunguza shaka na kutiliana shaka.
“Viongozi wanaowajibika na wenye uwazi mara nyingi hujenga imani na kuhamasisha watu kufuata maono yao. Uwajibikaji ni muhimu kwa sababu jamii inahitaji viongozi ambao wanakubali makosa na wako tayari kujifunza.”
Kujitolea na upendo kwa jamii
Anasema jamii inahitaji viongozi wenye kujitolea kwa masilahi ya umma na upendo kwa jamii wanayoiongoza.
“Upendo wa kweli wa kiongozi kwa jamii inaonekana kupitia juhudi zake za kuboresha maisha ya watu, hata katika mazingira magumu,” anasema Profesa Bakari.
Viongozi wenye moyo wa kujitolea hawaangalii gharama, bali wanajali kuboresha maisha ya watu. Kiongozi anayejali maendeleo ya jamii anafanya kazi kwa bidii hata katika mazingira magumu na changamoto nyingi.
Ni muhimu kwa jamii kuchagua viongozi wanaoonyesha nia ya dhati ya kuboresha maisha ya watu na kuleta mabadiliko chanya.
Profesa Bakari anasema jamii inahitaji viongozi wenye nia ya dhati ya kuboresha maendeleo ya muda mfupi na mrefu, hii inajumuisha mipango madhubuti ya kuboresha miundombinu, elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.
“Kiongozi anayejali maendeleo ya jamii anapaswa kuwa na mipango inayoeleweka na inayotekelezeka ili kuboresha sekta mbalimbali,” anasema.
Viongozi wenye nia ya dhati wana nafasi nzuri ya kusaidia jamii kufikia malengo makubwa ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili watu wake.
Uwezo wa kusikiliza maoni ya watu
Kiongozi bora ni yule anayejua kusikiliza na kufuatilia maoni ya watu, jamii imekuwa ikilalamikia uwepo wa viongozi wasiowajibika kwa matatizo ya wananchi.
“Kiongozi anayejua kusikiliza mawazo ya watu wake ni kipimo cha uwezo wake wa kuwaongoza. Kusikiliza ni fursa ya kuelewa changamoto na kujua nini kinahitajika kufanywa,” anasema Profesa Bakari.
Kusikiliza maoni ya wananchi ni ishara ya heshima, inayomsaidia kiongozi kuwa karibu na jamii anayoiongoza.
Ushirikiano na ustahimilivu
Ustahimilivu ni kigezo kingine muhimu katika kuchagua viongozi. Viongozi wanaojua kushirikiana na kuvumilia changamoto ni wale wanaoweza kufanya uamuzi bora na kufanikisha malengo ya muda mrefu.
“Changamoto katika jamii ni nyingi na nzito, lakini viongozi wanaostahimili wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo endelevu kwa jamii,” anasema Profesa Bakari.
Katika jamii, kila mtu ana matarajio kwa viongozi wake. Changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinaweza kuwa nyingi na nzito kwa viongozi, lakini wale wanaostahimili wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.
Rekodi katika nafasi za zamani
Jamii inaweza kujifunza mengi kupitia rekodi za nyuma za viongozi, rekodi za mgombea ni kiashiria muhimu cha tabia na uwezo wake wa kufanya kazi.
“Historia ya kiongozi ni kiashiria cha uwezo wake wa kujituma, uadilifu, na jinsi anavyoshughulikia changamoto,” anasema Profesa Bakari.
Kiongozi mwenye historia nzuri ya kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu na uwajibikaji ni chaguo bora kwa jamii. Rekodi hizi zinaonesha kama kiongozi alikuwa mchapakazi au alikuwa anajiingiza katika vitendo vya kifisadi.
Historia ya kiongozi inaweza kuwa mwanga wa utendaji wake katika nafasi mpya au ya zamani.
Katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi, uzoefu na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi ni nyenzo muhimu kwa kiongozi. Jamii inahitaji viongozi wenye ujuzi na wanaoelewa changamoto za jamii.
Mchambuzi wa masuala ya maendeleo ya jamii, Profesa Rose Mwengaka anasema kuna haja kwa wananchi kufahamu uwezo na uzoefu wa wagombea bila kuangalia itikadi ya vyama.
“Uwezo wa kufanya uamuzi wenye tija unategemea uzoefu wa kiongozi. Viongozi wenye historia ya kutatua matatizo na kutoa majibu ya haraka kwa changamoto ni tunu kwa jamii yoyote,” anasema Profesa Mwengaka.
Pia, anasema kipaji cha uongozi ni kigezo kingine muhimu katika kuchagua viongozi bora, kiongozi mzuri ni yule anayewajali watu wake, mwenye uwezo wa kuwasikiliza na kushirikiana nao. Kipaji cha uongozi kinajumuisha uwezo wa kuwa na maono ya muda mrefu kwa jamii.
“Kiongozi mwenye kipaji cha asili cha uongozi ana uwezo wa kuunganisha watu na kutimiza malengo ya pamoja,” anasema Profesa Mwengaka.
Viongozi wenye kipaji cha uongozi wanajua jinsi ya kushawishi na kuwapa watu motisha ili kufanikisha malengo ya pamoja ya maendeleo.