CCM wataka utaratibu msimamo wa ACT kupiga kura siku moja, Zanzibar

Unguja. Wakati Chama cha ACT Wazalendo kikiendelea na msimamo wake kupinga uchaguzi mkuu kufanyika siku mbili visiwani Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema ni vyema chama hicho kikafuata taratibu kwani kura hiyo ipo kwa mujibu wa sheria.

Mara kadhaa viongozi wa ACT Wazalendo wakiongozwa na Mwenyekiti wao Taifa, Othman Masoud wamekuwa wakisema katika uchaguzi ujao hawatakubali na hawapo tayari kuona uchaguzi Zanzibar ukifanyika kwa siku mbili.

Hivi karibuni katika mikutano ya hadhara ya chama hicho, Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema hawapo tayari kuingia kwenye uchaguzi huo hata kwa nusu siku.

Kwa kawaida Zanzibar, hufanya uchaguzi wa mapema ambapo siku ya kwanza wanaopiga kura ni wenye kazi maalumu vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, maofisa wa tume wenyewe na watu wengine,  siku ya pili wakipiga kura wananchi wote.

“Kama watu wanajiamini wanatakiwa wazingatie katiba waingie uwanjani masanduku ya kura ndiyo yaamue mwenye nguvu,” alisema Othman

Akizungumza na waandishi wa habari Makao makuu ya CCM Zanzibar leo Novemba 18, 2024, Katibu wa Kamati Maalumu, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar, Khamis Mbeto amesema wanashangazwa na kauli zinazotolewa na chama hicho kwani uchaguzi wa siku mbili upo kwa mujibu sheria.

Sheria namba nne ya uchaguzi ya mwaka 2018 ibara ya 82 ndiyo inayozungumzia kuhusu kura ya mapema kisiwani humo.

Katika sheria hiyohiyo ibara ya 15 inazungumzia utaratibu wa uandikishaji na jinsi ambavyo kila chama kinatakiwa kuweka mawakala wake, huku ibara ya 75 ikieleza mchakato mzima wa upigaji kura utakavyokuwa.

“Kama wanaona hawapo tayari ni vyema kufuata utaratibu kupeleka muswada katika Baraza la Wawakilishi ili sheria hiyo ifanyiwe marekebisho, lakini sio kwa kauli a kuonesha kutishia amani, amesema Mbeto

Wakati Mbeto akisema hivyo, Othman amesema wameshaomba kuondolewa utaratibu huo mara kadhaa lakini Serikali haijajibu.

Katibu huyo amesema hakuna mtu yeyote mwenye uamuzi tofauti na baraza la wawakilishi, “hata Rais hawezi kubadilisha hilo hata CCM haina mamlaka hayo isipokuwa Barazani. kitu cha kisheria kinaondolewa kisheria sio matakwa na maneno ya utashi,” amesema

Kwa mujibu wa Mbeto, utaratibu wa kupiga kura kwa siku mbili uliwekwa kutokana na sheria kutaka kila mtu apige kura eneo alipojiandikisha.

“Kwa hiyo wapo maofisa wa Tume ya Uchaguzi ambao husimamia uchaguzi nao wana haki ya kupiga kura, hivyo wanatumia siku hiyo kupiga kura kabla ya kwenda kusimamia mchakato huo maeneo mengine,” amesema.

Mbeto amesema msimamo wa chama ni kwamba iwapo sheria ikibadilishwa na kuondoa kura ya mapema hakina shaka chenyewe kipo tayari, lakini hakipo tayari kuvunja katiba na sheria za nchi kwa ajili ya matakwa ya watu wachache.

Amesema utaratibu wa kupiga kura ya mapema haupo Zanzibar pekee bali kuna nchi nyingine hufanya hivyo zikiwamo Marekani, Nezaland, Afrika Kusini na Hispania.

Mbeto amesema chama hicho hakitakuwa tayari kuona kuna viashiria vya kutaka watu kuvuja damu, kwani hivyo ni viashiria vya kuhamasisha wananchi kuingia kwenye matatizo.

Katika ushauri wake kwa chama hicho Mbeto amesema, “lazima tujue hivi vyama ni vya kupita lakini Zanzibar itaendelea kuwepo hivyo kila mmoja ailinde kwa wivu mkubwa.

Kuhusu kauli ya ACT kuwa CCM inaogopa kuingia kwenye uchaguzi,  Mbeto amesema chama hicho hivi sasa kinajiamini kuliko wakati wote kwa sababu Dk Mwinyi amefanya mambo makubwa kwa wananchi.

“Kutokana na utendaji wa Dk Mwinyi, ndio maana umewashtua na wameanza kutafuta visingizio, lakini kwa jinsi maendeleo yaliyofanywa tunaamini Dk Mwinyi atashinda kwa asilimia sio chini ya 85, kwanza anauzika na amefanya vitu vinaonekana wananchi wanachotaka ni maendeleo.”

Related Posts