RC SERUKAMBA AIUNGA MKONO REA UGAWAJI MITUNGI YA GESI 9800 IRINGA

REA yahamasisha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta maeneo ya vijijini

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba ameunga mkono juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) za kusambaza mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 9,800 mkoani humo itakayoendelea kuhamasisha na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mhe. Serukamba amezungumza hayo leo Novemba 18, 2024 mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA katika mkoa huo iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu, Mha. Advera Mwijage.

Mhe. Serukamba ameipongeza REA kwa mradi huo na miradi mingine mbalimbali inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ikiwemo ya kufikisha umeme kwenye vijiji na vitongoji.

“Nawapongeza REA kwa kuendelea kusambaza mitungi ya gesi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi. Nawapongeza pia kwa kuendelea kufikisha umeme katika maeneo mbalimbali, natoa rai kwenu kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo makampuni makubwa katika kutekeleza miradi hiyo nchini ili kuifanya kuwa na tija kwa wananchi.” Amemalizia Serukamba.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mha. Mwijage ameeleza kuwa, mitungi hiyo itasambazwa katika wilaya tatu ikiwemo Kilolo, Iringa na Mufindi ili kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama.

Ameongeza kuwa kampuni ya Lake Gas itaanza kusambaza gesi za kupikia mkoani humo mwezi Januari mwaka 2025 ili wananchi waanze kunufaika na nishati hiyo.

Katika hatua nyingine, Mha. Advera amewataka Watanzania kuchangamkia fursa ya ujenzi wa vituo vya mafuta kwa kuwasilisha maombi REA.

“Mradi utahusisha ujenzi wa vituo vya mafuta kuanzia lita 10,000 hadi lita 15,000 za mafuta na naipongeza Serikali kwa kuendelea kuleta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii, ” Amesema Mha. Mwijage.

Related Posts