WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa maagizo kwa jeshi la Polisi nchini, kumtafuta mmliki wa jengo lililoanguka na kuleta maafa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Majaliwa ametoa agizo hilo hii leo tarehe 18 Novemba 2024, kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, wakati wa ibada maalum ya kuaga miili 15 ya watu waliopoteza maisha kufuatia kuanguka kwa jengo hilo.
Waziri Mkuu amesema kuwa, tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maagizo manne, kufuatia tukio hilo wakati akizungumza na wananchi jana, akiwa nchini Brazil kwa ziara maalum ya kikazi.
Baadhi ya maagizo yaliyotolewa na Rais Samia, ni pamoja ma Serikali kubeba gharama zote za matibabu kwa walionusulika sambamba na kubeba gharama zote za mazishi kwa waliopoteza maisha.
Katika hatua hiyo Waziri Mkuu aliviagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kumtafuta mmiliki wa jengo hilo, kwa lengo la kupata taarifa zaidi kuhusu tukio hilo ambalo limegusa watanzania wengi.
“Serikali inakamilisha uchunguzi wa kujua chanzo cha tukio hilo, sambamba na hilo naagiza jeshi la Polisi kumtafuta mmiliki wa jengo kujua kwanini jengo hilo limeanguka.” Alisema Majaliwa
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa, zoezi la uokoaji bado linaendelea na halitositishwa mpaka pale mtu wa mwisho atakapo patikana, huku idadi ya waliookolewa mpaka kufika mchana wa leo ni 86, huku waliopoteza maisha wakiwa 16.