Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Jerry Silaa, amesema kasi aliyokuwa nayo alipokuwa sekta ya ardhi ataindeleza katika sekta ya habari, akianza na mijadala na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Alitoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa habari kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
Akiwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Silaa, alisifika kwa kushughulikia migogoro ya ardhi, kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kumhamisha huku akisifu utendaji wake.
Katika mkutano huo, Waziri Silaa amewaahidi wanahabari na wadau wa sekta ya habari kufanya kazi kwa ukaribu ili tasnia hiyo kusonga mbele, akisema atafanya ziara ya kutembelea vyombo vya habari sambamba na kufanya mazungumzo na makundi ya sekta hiyo.
“Nawaahidi nitaendelea kuwa karibu na tasnia ya habari, nitafanya kazi kwa moyo mmoja, kuhakikisha nawafikia wote, dhamira yangu ya dhati ni kuleta mageuzi katika sekta ya habari.
“Nitaanza kutembelea makundi kisha chombo kimojakimoja kuwasikiliza na kubadilishana uzoefu ili sekta yetu iwe bora na yenye mchango mkubwa. Novemba 21, nitakutana na umoja wa haki ya kupata taarifa ndani yake kuna taasisi 16 za kihabari,’’amesema.
Katika hatua nyingine, Silaa alikubaliana na hoja ya mjumbe wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF) Neville Meena aliyesema mkutano huo umechelewa kwa sababu uchaguzi wa serikali za mitaa unakaribia, akishauri ungefanyika mapema zaidi.
“Ni kweli kongamano hili ingefanyika mapema lingesaidia, lakini tutumie kongamano hili kutengeneza mkutano wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” amesema Silaa.
Waziri Silaa amesema michango yote iliyotolewa na wadau wa mkutano Serikali itaifanyia kazi ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya habari nchini.
Katika mkutano huo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema taasisi hiyo ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wanahabari, huku akiwataka kujiepusha na vitendo vya uchochezi, kuzingatia maadili katika uandishi kuripoti habari zenye ukweli.
“Jeshi la polisi katika uchaguzi linalinda usalama, kutatua matatizo madogo ya jamii, kuzuia vitendo ya kihalifu kabla ya kujitokeza, kulinda mikutano ya kampeni, kutoa ulinzi kwa wagombea na kuhakikidha usalama wakati wa kuhesabu kura,” amesema Misime.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba amesema lengo la mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ni kuboresha ni kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa sekta ya habari.
Katika mkutano huo, wajumbe waliazimia mambo matano kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, ikiwamo wanahabari kuzingatia sheria, kanuni na maadili katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji 2024 kwa kutumia kalamu zao kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya uchaguzi kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, sambamba na kujiepusha kutumika vibaya na wagombea.
Mengine ni wanahabari kupewa mafunzo kuhusu sheria na kanuni za uchaguzi hasa maeneo usalama wao binafsi, kwa kuzingatia maadili ya uandishi, Serikali wadau wa habari na polisi kufanya mikutano ya pamoja yenye lengo la kulinda amani, utulivu na usalama na wamiliki wa vyombo vya habari kulipa vizuri wanahabari.
“Wanahabari wazingatie kanuni na maadili ili kuepusha Taifa na wananchi kuingia katika migogoro isiyo ya lazima, badala yake kipaumbele kiwe kuzingatia uzalendo wa kwa Taifa kupitia kalamu zao,” amesema Christina Mwangosi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambo ya Ndani.
Mwangosi amewataka pia wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanawapatia vitendea kazi wanahabari wao vinavyowatambulisha katika matukio mbalimbali ili kujilinda na usalama wao.
Mkutano ulihusisha wanahabari, wadau wa elimu,maofisa wa Serikali na makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi.