Na Jane Edward, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amekutana na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Bi. Veronica Nduva, akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha katika maandalizi ya kufanikisha Maadhimisho ya miaka 25 tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Jumuiya hiyo mnamo Novemba 29- 30, 2024.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu Novemba 18, 2024, Bi. Nduva pia ametumia fursa hiyo pia kumpongeza Mhe. Makonda kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kudumisha amani na utulivu wa Mkoa wa Arusha sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi na Utalii wa Mkoa wa Arusha na hatimaye kuinua pato la Mkoa na la mwananchi mmoja mmoja.