Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kisarika iliyopo Uru, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Manuari Agusti (16) amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa Shule ya Msingi Ongoma.
Tukio hilo limetokea wakati majengo chakavu ya shule hiyo yalipokuwa yakibomolewa kwa ajili ya ujenzi mpya.
Mwanafunzi aliyekuwa likizo baada ya kumaliza mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili, alifariki dunia Novemba 14, 2024, baada ya kuangukiwa na ukuta wakati shughuli za ubomoaji wa majengo ya shule hiyo zilipokuwa zikiendelea.
Tukio hilo lilimsababishia majeraha makubwa kichwani ambapo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC).
Akizungumza leo Jumatatu, Novemba 18, 2024, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa shule husika ilikuwa ikibomolewa ili kujengwa upya baada ya madarasa ya awali kuonekana kuwa chakavu.
Mhagama amesema mwanafunzi huyo aliyekuwa akiishi na bibi yake, alitoka nyumbani bila kuaga na kwenda kushuhudia shughuli za ubomoaji wa majengo ya shule hiyo.
Katika harakati hizo, mwanafunzi huyo alisimama karibu na moja ya majengo yanayobomolewa na ukuta wa jengo hilo ulimwangukia bila mafundi kumwona.
“Wakati ukuta ule ulipoporomoka, mafundi hawakumwona mtoto aliyekuwa amesimama jirani na jengo hilo. Walishituka baada ya kusikia kelele zake alipodondokewa na ukuta,” amesema Mhagama.
Aidha, Mhagama aliongeza kuwa shughuli za ubomoaji zilikuwa zikisimamiwa na mafundi waliokuwa wakitekeleza maelekezo ya mhandisi wa wilaya.
Mwananchi Digital imetembelea nyumbani kwa mwanafunzi huyo na kuzungumza na babu yake, Emily Mushi aliyekuwa akiishi naye.
Emily amesema mjukuu wake alikwenda aneo hilo siku hiyo baada ya tangazo lililotolewa kuhusu wananchi kushiriki katika shughuli hiyo.
“Novemba 9,2024 tulitangaziwa kanisani kuwa kutakuwa na ubomoaji wa shule ya msingi Ongoma kuanzia Jumatatu Novemba 10. Mjukuu wangu alikwenda shuleni kushiriki na wenzake, lakini ukuta ulivunjika ghafla na kumuangukia,” amesema Emily.
Amesema baada ya ajali hiyo, mjukuu wake aliwahishwa Hospitali ya Mawenzi kabla ya kuhamishiwa KCMC. Hata hivyo amesema Novemba 16, 2024, alifariki dunia.
Naye bibi wa marehemu, Matilda Chuwa amesema kifo cha mjukuu wao kimewaachia maumivu makubwa, hasa kwa mama yake ambaye marehemu alikuwa mtoto wa pekee.
“Wakati tukio hilo linatokea, nilikuwa mjini nikiwa kwenye shughuli zangu. Nilipopigiwa simu, nilikimbia kwenda Mawenzi. Ni maumivu makubwa, kwa sababu huyu mtoto alikuwa wa pekee kwa mama yake,” amesema Matilda.