Serikali kusambaza vitabu vya tuzo ya Mwalimu Nyerere

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Anneth Komba amesema Serikali inagharamia uchapishaji na usambazaji shuleni nakala za vitabu vitatu, vilivyoshinda tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu kwa mwaka 2024.

Amebainisha hayo leo Novemba 18,2024 jijini hapa wakati wa hafla ya uzinduzi wa usambazaji wa vitabu hivyo iliyohudhuriwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda na Taasisi ya TET.

Vitabu vilivyoshinda tuzo hizo ni vilivyopo kwenye nyanja za riwaya, shairi na vitabu vya watoto.

Aidha, tuzo hizo zilizotolewa Aprili 13, 2024 zilienda kwa mwandishi wa riwaya ya ‘Gereza la kifo’ kilichoandikwa na  Amiri Abdala, ‘Ushairi wa Mtale wa Ngariba’ ulioandikwa na Hamisi Husain na kitabu cha watoto cha ‘Zawadi’ kilichoandikwa na Blandina Lucas.

Sambamba na zawadi ya pesa taslimu, vyeti walivyopewa washindi hao, Serikali inagharamia uchapishaji wa nakala za vitabu na kuvisambaza shuleni.

”Pamoja na washindi hawa kukabidhiwa zawadi ya Sh10 milioni, kila mwandishi anachapishiwa nakala 140,000 ya kitabu chake. Jumla ya fedha za Serikali zilizotumika kuchapisha vitabu hivyo ni Sh400 milioni, huku nakala nyingine 80,182 za kitabu cha watoto zikichapishwa kwa msaada wa Benki ya Dunia kwa gharama ya zaidi ya Sh47 milioni” ameeleza Komba.

Kadhalika Komba amesema usambazwaji wa vitabu vya ushairi na riwaya utafanyika kwa shule zote za sekondari bara na visiwani, huku kitabu cha watoto kikisambazwa kwa shule za msingi.

“Kitabu cha hadithi za watoto cha Zawadi kitasambazwa kwa shule za msingi zilizopo kwenye halmashauri 41 nchini, ambapo ni sawa na asilimia 25 ya halmashauri zote ambazo wanafunzi wake hawakufanya vizuri katika upimaji wa ustadi wa kusoma” ameeleza.

Pia, Komba amesema, halmashauri zitakazobakia zitapewa nakala za vitabu hivyo vilivyochapishwa kwa gharama za Serikali.

Akizungumza kwenye hafla hiyo,  Profesa Adolf Mkenda amesema kati ya changamoto zinazokumba sekta ya uandishi wa vitabu ni pamoja na waandishi hao kutoenziwa pamoja na ugumu wa soko la bidhaa hizo nchini.

“Waandishi wengi hapa nchini wamekosa kuenziwa na kubaki katika historia ya Taifa, kuna baadhi ya wanasiasa wanaenziwa kwa barabara shule kupewa majina yao kitu ambacho ni tofauti sana kwa tasnia hii, waandishi wana mengi ya kuenziwa tofauti na wanasiasa ni vyema Serikali ijifunze namna bora ya kuwaenzi watu hawa wenye mchango mkubwa kwenye jamii “amesema Mkenda

Amesema sekta ya uandishi inadorora siku hadi siku kutokana na watu kupoteza tamaduni ya kusoma vitabu, huku kampuni za uchapishaji wa vitabu vikiwa na hatihati ya kufungwa.

Anasema changamoto hizi ndizo zilizosababisha kuwepo kwa shindano la tuzo za Mwalimu Nyerere zenye lengo la kuhamasisha tasnia uandishi pia  ikiwatia moyo waandishi hao.

Mkenda amesisitiza kuwa moja ya maazimio ya tuzo hizo ni pamoja na kuchangamsha sekta ya vitabu hapa nchini.

“ Tunachangamsha sekta hii ya uandishi wa vitabu kwa kuwasaidia waandishi kuchapisha kopi za vitabu vyao, huku hati miliki ikibakia kwa mwandishi, nia na madhumuni  ni kukuza na kukisambaza Kiswahili ndani na nje ya nchi,” ameeleza

Kadhalika, Mkenda amesema Serikali itahakikisha vitabu vyote vyenye jumbe za kujenga, vitanunuliwa na kusambazwa katika shule mbalimbali.

“Tutanunua vitabu vyote vyenye jumbe za kujenga ikiwa ni njia ya kuwatia moyo waandishi wa vitabu hivyo na gharama walizoingia kuvichapisha” ameeleza Profesa Mkenda

Related Posts