TUZO ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu itaendelea kuchochea uandishi na usomaji hapa nchini na kuchangia kukuza lugha ya Kiswahili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 17/11/2024 jijini Dar es salaam , wakati wa hafla ya uzinduzi wa ugawaji wa vitabu viwili vilivyoshinda Tuzo hiyo kwa Mwaka 2022-2023 na kimoja cha Tuzo ya Mwaka 2023-2024.
“Tuzo hii itaendelea kuchochea waandishi wengi kuandika vitabu vizuri na vyenye maadili ambavyo vitasaidia katika kutumika shuleni kwa watoto wetu na hii itasaidia sana Watanzania wengi kupenda kujisomea vitabu vilivyoandikwa kwa lugha yao ya Kiswahili” amesema Prof.Mkenda”
Ameongeza kwa kueleza kuwa Serikali itaendelea kuipa nguvu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) katika kuhakikisha tuzo hii inaendelea kila mwaka na kushirikisha watu wengi na kufanya soko la uchapishaji wa vitabu wa hapa nchini lizidi kukukua. Vilevile, Serikali itaendelea kuhakikisha waandishi wote nchini wenye vipaji wanafikiwa na kushiriki na kuwasilisha miswaada yao kwa ajili ya tuzo ya mwaka 2024/2025 kwa wingi.
Nae Mwenyekiti wa Tuzo hiyo, Prof.Penina Mlama, ameendelea kuwahimiza Watanzania kujitokeza kuwasilisha miswada yao kwa ajili ya kushindaniwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw.Khamis Abdulla Said amesema vitabu hivyo vitaganywa shuleni ili wanafunzi wapate maarifa kupitia uandishi huo bunifu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la TET, Prof. Maulid Mwatawala ameshukuru namna serikali inavyoendelea kuwaunga mkono katika kuhakikisha TET inatekeleza majukumu yake na kuelezea namna uandishi wa vitabu vya mtaala mpya ulivyokamilika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, DKt. Aneth Komba, ameeleza kwamba vitabu vyote vilivyoandaliwa kwa kupitia maandiko ya washindi hao wa tuzo vitaanza kusambazwa shuleni ili wanafunzi waweze kujifunza .
Vitabu hivyo ni Zawadi(Hadithi za Watoto), Gereza la Kifo(Riwaya) na Mtale wa Ngariba( Ushairi) vimechapishwa kwa udhamini wa Serikali na Benki ya Dunia.