Songwe. Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo amesema vita yake na baadhi ya wakuu wa wilaya ni wao kuingilia masilahi ya wananchi.
Mulugo alitoa kauli hiyo jana Novemba 17 wakati wa uzinduzi wa mtambo mpya na wa kisasa wa kuchakata na kuchenjua dhahabu (CIP) katika kampuni ya Green Pasific unaogharimu Sh10 bilioni ukiwezeshwa na benki ya NMB.
Mulugo amesema Songwe wamepita wakuu wengi wa wilaya ambapo wakati mwingine akianza kugombana nao, sababu kubwa huwa ni wao kuingilia maslahi ya wananchi wake, akieleza kuwa kwa sasa wilaya hiyo imetulia tangu kuletwa kwa Solomon Itunda.
Amesema Itunda anafanya kazi nzuri ikiwamo ya kuunganisha makundi yote ya wananchi.
“Kwa Mkuu wa Wilaya huyu (Itunda) nimefika mwisho, wamepita wakuu wengi hapa na wakati mwingine nikigombana nao kutokana na kuingilia masilahi ya wananchi”
“Tangu mwaka jana wilaya hii imetulia, hakuna migogoro anaunganisha makundi yote, tunaomba usihamishwe hapa, labda upewe ukuu wa mkoa ila kama ukuu wa wilaya usihame, mimi anayegusa masilahi ya wananchi wangu lazima niruke na yeye” amesema Mulugo.
Kwa upande wake Itunda amesema alipofika wilayani hapo alikutana na viongozi na kukubaliana njia ya kumaliza changamoto zote ni mawasiliano na majadiliano, akieleza kuwa nia ni kuona wananchi wanapata huduma kama anavyotaka Rais Samia Suluhu Hassan.
Kuhusu changamoto ya umeme wilayani humo, Itunda amekiri kero hiyo akieleza kuwa baada ya mwaka mmoja wataondokana na tatizo hilo kufuatia mradi unaojengwa, ambao utazalisha megawati 41 badala ya zilizopo 20 kutotosha hasa maeneo ya migodini.
“Songwe imeendelea kubadilika na tunahitaji wawekezaji wengi kufungua fursa za kiuchumi na ajira kwa vijana, bado hatuna hoteli hapa wilayani, sisi Serikali tunaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji”
“Wachimbaji wote zingatieni sheria na taratibu za nchi, Songwe ni wilaya ya tatu kitaifa katika sekta ya madini tukichangia Sh50 bilioni kwa mwaka kwenye mfuko wa Serikali, hivyo bado tunahamasisha uchimbiaji” amesema Itunda.
Kwa upande wake Katibu na mwanasheria wa kampuni hiyo, Dauson David amesema mradi huo utatoa fursa ya ajira kwa vijana zaidi ya 350 ikiwamo mikataba ya muda na moja kwa moja.
Amesema mtambo huo wenye teknolojia ya Carbon in Pulp (CIP) unaweza kuchakata na kuchenjua dhahabu tani 10 kwa saa, tofauti na uliokuwapo ambao ulikuwa na uwezo wa kuchakata tani tatu kwa saa moja.
“Mradi huu ni wa mwekezaji mzawa, Frederick Asheri ambapo tumewezeshwa na benki ya NMB, lengo ni kuongeza thamani katika sekta ya madini na tumezingatia viwango vyote vya kimataifa bila kuathiri mazingira na afya ya jamii” amesema David.
Kaimu Ofisa madini mkoani humo, Richard Seyaza amesema licha ya manufaa na faida ya mradi huo, amemtaka mwekezaji huyo kuzingatia sheria za uchimbaji hasa kwa kutoathiri mazingira na jamii inayozunguka mgodi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa NMB Nyanda za Juu Kusini, Wogofya Mfalamagoha, Meneja wa benki hiyo tawi la Mkwajuni mkoani hapa, Yohana Bundala amesema kwa kutambua mchango wa sekta ya madini wameanzisha program ya NMB Mining Club ili kutoa fursa ya kuwasaidia kiuchumi wachimbaji.
“Kutokana na uwezeshaji huu wa mtambo katika kampuni hii, tunatarajia kuona idadi kubwa ya wachimbaji wakija kupata huduma, sekta ya madini kwetu ni ya kimkakati hivyo hii ni fursa kwenu wadogo kwa wakubwa” amesema Bundala.
Mmoja wa wananchi katika kijiji cha Mbangala uliopo mgodi huo, Rebecca Sanua amesema wanaona mabadiliko chanya na yenye matumaini ya uchumi wao kuimarika kutokana na kuwapo kwa uwekezaji huo mkubwa.