Yanga kupitisha panga lingine, yaleta watu wa kazi

SEAD Ramovic ndiye kocha mkuu wa Yanga akichukua mikoba ya Miguel Gamondi aliyetimuliwa Oktoba 15 mwaka huu sambamba na msaidizi wake, Moussa N’daw.

Yanga jana mchana ilimtangaza rasmi kocha wa zamani wa Azam na KMC, Abdi Moalin kama Mkurugenzi wa Ufundi mpya.

Lakini katika kujenga benchi jipya la kazi likiwa na jukumu la kuiongoza timu hiyo katika michezo ijayo kwa kuanza na hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Novemba 26 mwaka huu, ameongezwa mtu mwingine wa kuchukua nafasi ya N’daw, raia wa Senegal.

Ikumbukwe kwamba, Ramovic alipokabidhiwa mikoba ya kuifundisha Yanga amewabakisha makocha wengine wote waliokuwa wasaidizi kwa Gamondi akiwamo kocha wa viungo Taibi Lagrouni, kocha wa makipa Alaa Meskini na mchambuzi wa mikanda ya video Mpho Maruping.

Katika kuhitaji msaidizi makini ambaye watakuwa wakifanya kazi vizuri, kocha huyo Mjerumani amemvuta mshkaji wake, Mustafa Kodro anayetokea nchini Bosnia-Herzegovina.

Kodro ambaye alikuwa msaidizi wa Ramovic pale TS Galaxy, amezaliwa Agosti 29, 1981 huko Mostar nchini Bosnia-Herzegovina huku akiwa na UEFA Pro Licence.

Kabla ya kuwa kocha, Kodro katika kipindi chake cha kucheza soka alikuwa kiungo mkabaji, akizitumikia Zvijezda na FK Velez Mostar zote za Bosnia-Herzegovina.

Kazi ya ukocha alianzia FK Velez Mostar akiwa kocha msaidizi ambapo majukumu hayo aliyachukua kuanzia Agosti 5, 2019 hadi Juni 1, 2022. Juni 2, 2022 akatua FK Sarajevo kabla ya kuachana nayo Oktoba 19, 2022, ndipo Desemba 28, 2022 akatua TS Galaxy aliyoachana nayo hivi karibuni alipopata dili la Yanga.

Kocha huyo alianza kufanya kazi pamoja na Ramovic Desemba 2022 baada ya Ramovic kuwa TS Galaxy tangu Oktoba 2021. Wawili hao wamepishana miaka miwili tu ambapo Ramovic ana 45 wakati Kodro akiwa na 43.

Kabla ya kuongezwa kwa kocha msaidizi, Yanga ilimchukua Abdihamid Moallin kuwa mkurugenzi wa ufundi.

Moalin ambaye alikuwa kocha mkuu wa KMC, amepanda cheo akiwa Mkurugenzi wa Ufundi mpya ndani ya Yanga.

Mtu wa mwisho kushika nafasi hiyo ndani ya Yanga alikuwa kocha Mdachi Hans van Der Pluijm wakati timu hiyo ikiwa chini ya kocha mkuu Mzambia, George Lwandamina enzi ya uongozi wa Bilionea marehemu Yusuf Manji.

Kama ulidhani panga la Yanga limeishia kwa kocha Miguel Gamondi, basi umekosea kwani mabosi wa klabu hiyo wamepania kuanza upya kwa kuwaondoa baadhi ya wafanyakazi katika vitengo vingine, huku wengine waliowahi kuondolewa wakirudishwa.

Baada ya kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi pale Yanga, sasa kuna fagio litapita ndani ya sekretarieti ya klabu hiyo.

Ingawa bado Yanga haijaweka wazi lakini taarifa za uhakika ni kwamba uongozi wa klabu hiyo utapitisha fagio la watendaji wa sekretarieti kwa sababu mbalimbali za kiutendaji.

Mchakato huo tayari umeshapata baraka za Kamati ya Utendaji katika kikao kilichoketi Novemba 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa watendaji hao kutoongezewa mikataba yao.

Mabadiliko hayo yataanzia idara ya fedha ambapo mtu mmoja atachomolewa.

Idara ya Sheria nayo itakumbana na mabadiliko hayo kwa bosi mmoja naye kuondolewa.

Kitengo cha mauzo ya jezi nako kutapita fagio kubwa. Tayari kuna baadhi ya tuhuma zimewaweka nje watendaji watatu ambao wanasimamia mauzo ya jezi za klabu hiyo moja ya madai ikiwa kubainika kujihusisha na bidhaa feki.

Hivi karibuni, Mwanaspoti limepita makao makuu ya klabu hiyo na kukuta duka la kuuza jezi za klabu hiyo limefungwa huku baadhi ya wanachama wakieleza ni kutokana na tuhuma hizo.

Hata hivyo, kesho Jumatano klabu hiyo inazindua jezi zake mpya kwa ajili ya michuano ya kimataifa ambapo timu hiyo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa Kundi A.

Katika hatua nyingine, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine bado ataendelea kuitumikia klabu hiyo kufuatia kuongezewa mkataba.

Mtine, raia wa Zambia, tangu atue Yanga klabu hiyo imeendelea kupata mafanikio huku ikibainisha kwamba utulivu wa kiutendaji wa klabu hiyo ni vitu vilivyombeba.

Yanga pia imemrudisha Hafidh Saleh ambaye alikuwa nje ya kikosi hicho baada ya awali kuondolewa wakati wa utawala wa Kocha Gamondi.

Mara baada ya kuondolewa kwa Gamondi, Mwanaspoti limepata taarifa ya kurudishwa kwa Hafidh.

Related Posts