WAKATI Simba ikiwa kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na michezo mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika, inaelezwa uongozi wa klabu hiyo kesho Jumatano umepanga kuzindua jezi maalumu kwa michuano ya kimataifa.
Chanzo kutoka ndani ya Simba, kililiambia Mwanaspoti kuwa klabu hiyo imepanga kuzindua jezi hizo kabla ya mechi dhidi ya Pamba Jiji inayotarajiwa kupigwa Novemba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, wanaamini jezi hizo tatu yaani nyeupe, nyekundu na bluu zina ubora unaokidhi hadhi za kimataifa ambapo timu hiyo itaanza harakati zake za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika nyumbani dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola.
“Tunaamini ubora wa jezi hizo kwa ajili ya mashindano makubwa ya kimataifa na zitaanza kutumika katika hatua hii ya makundi,” kilisema chanzo hicho.
Simba imetinga kucheza makundi Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Al Ahly Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mchezo wa awali ikitoka suluhu ugenini.
Baada ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji, Simba itakuwa nyumbani Novemba 27 mwaka huu katika mechi ya kwanza ya Kundi A dhidi ya Bravos do Maquis.
Wakati huohuo, uongozi wa Yanga nao umepanga kesho Jumatano kufanya uzinduzi wa jezi za timu hiyo kwa ajili ya mashindano ya kimataifa.
Jezi hizo zitakazozinduliwa, zitaanza kutumika katika michezo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo timu hiyo imepangwa Kundi A ikianza na Al Hilal, Novemba 26 mwaka huu hapa nyumbani.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema baada ya uzinduzi kufanyika Novemba 20, jezi hizo zitaanza kupatikana katika Makao Makuu ya Klabu yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam sambamba na maduka ya GSM.
“Nitumie fursa hii kuwaambia mashabiki, wapenzi na wanachama wetu wa Klabu ya Yanga jezi zetu za kimataifa tayari zimeshafika na kwa mujibu wa mipango ya ofisi ya Mtendaji Mkuu jezi hizi zitazinduliwa siku ya tarehe 20,” alisema Kamwe.