Kipa Pamba azitamani namba za Diarra, Camara

WAKATI Pamba Jiji ikijiandaa kuvaana na Simba Novemba 22, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kipa wa timu hiyo, Yona Amos amesema bado hajajipata na anatamani kuwa miongoni mwa makipa watano bora ili kufikia ubora wa makipa kama Djigui Diarra (Yanga) na Moussa Camara (Simba).

Amos ameidakia Pamba Jiji katika mechi 11 za Ligi Kuu na kuambulia cleensheet tatu huku akiruhusu mabao 13, ambapo Camara anaongoza akiwa na cleensheet nane wakati Diarra akiwa nazo saba.

Kipa huyo wa zamani wa Tanzania Prisons aliyejiunga na Pamba Jiji kwenye usajili wa dirisha kubwa msimu huu, alisema hajafikia kwenye kiwango anachokitamani na hajioni kama kwa sasa anastahili kujumuishwa kwenye orodha ya makipa watano ama 10 bora kwenye ligi kwani hajaisaidia timu yake ipasavyo.

“Kwanza mimi namba zangu ni ndogo kazini, kwenye makipa watano bora kwa sasa sipo kwa sababu timu yangu haiko sawa kwenye matokeo, hii inanipa chachu nizidi kupambana hata kwenye wale 10 niwepo lakini kwa sasa hata watano simo kwa sababu timu yangu tunapoteza na kuruhusu mabao,” alisema Amos.

Alisema ili kutimiza hayo anapaswa kudumisha nidhamu, kujituma na kuonyesha ubora wake kila anapopewa nafasi ya kuipambania timu yake, huku ushindi wa kwanza walioupata dhidi ya Fountain Gate ukiwapa motisha na morali ya kujituma ili wawe na mwendelezo katika mechi zijazo.

“Nimejipanga vizuri kupambana kuipa klabu matokeo mazuri na kuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango bora tunaomba Mungu atupe mwendelezo mzuri na upambanaji ili tukae sawa kwenye ligi,” alisema Amos

Aliongeza kuwa mchezo dhidi ya Mashujaa FC ulioisha kwa mabao 2-2 katika Uwanja wa CCM Kirumba, ulimuuma zaidi kwani timu yake iliongoza mpaka dakika ya 70 lakini ikaruhusu mabao mawili ya kusawazisha, huku akimmwagia sifa kipa mkongwe wa timu hiyo, Shaban Kado.

“Shabani Kado anatujenga kiakili na kutupa moyo wa kupambana na kujituma akituelekeza kupitia uzoefu wake na mbinu mpya na sisi tunayapokea ili tuendelee kufanya vizuri na kusaidia nchi, klabu na maisha baada ya mpira,” alisema kipa huyo.

Related Posts