Sababu za ufaulu kuimarika Zanzibar

Unguja. Kwa kipindi cha nyuma, shule za Zanzibar zilikuwa zikifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa, lakini sasa hali imebadilika huku mikakati mbalimbali ikitajwa kuleta mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na serikali kutoa kipaumbele katika sekta hiyo.

Katika bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2024/25 ya Sh5.18 trilioni, sekta ya elimu imepangiwa bajeti ya Sh830 bilioni ikiwa ndio sekta inayoongoza kuliko sekta zote.

Kutoa kipaumbele katika sekta hiyo ndio moja ya sababu inayotajwa kuleta mageuzi makubwa sekta ya elimu

Katika kutatua changamoto cha shule za Zanzibar kufanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa, Serikali iliunda timu maalumu kwa kushirikiana na sekta binafsi kuchunguza changamoto zinazoikabili sekta ya elimu na kupata suluhu ya kudumu.

 Miongoni mwa changamoto zilizobainika ni pamoja na mrundikano wa wanafunzi, uwepo wa mikondo miwili ya asubuhi na jioni, ubovu wa mindombinu, uchache wa walimu na maslahi madogo.

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa anasema pia bajeti ya maendeleo ya elimu imeongezeka kutoka Sh19 bilioni mwaka 2020 hadi kufikia Sh518 bilioni mwaka 2024.

“Miundombinu ya elimu haikuwa rafiki, wanafunzi walikuwa 120 ndani ya darasa moja na walimu wawili, mmoja anafundisha mwingine anatuliza nidhamu ya watoto. Ndio maana tukaamua tujenge madarasa,”

Anasema uandikishaji wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 535,467 mwaka 2020 hadi kufikia wanafunzi 620,609 katika ngazi zote za elimu. Jumla ya watoto 35,941 walirejeshwa shuleni kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita,” amesema

 Amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu kwa kujenga shule za kisasa katika maeneo yote Unguja na Pemba ili kuleta mageuzi katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri Lela, jumla ya madarasa 2,738 yamejengwa na shule za ghorofa 35 kwa kipindi cha miaka minne huku madarasa mengine mapya 2,037 ikiwemo shule 26 za ghorofa na shule za kawaida 53 tayari ujenzi wake umeanza kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2024-2025.

 Amesema, pia zimefanyiwa ukarabati mkubwa shule 91 ambapo asilimia 67 za msingi na asilimia 87 za sekondari zinaendeshwa kwa mkondo mmoja.

Anasema ufaulu wa wanafunzi wa vipawa na michepuo katika mtihani wa darasa la saba umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 27,5 mwaka 2023 na ufaulu katika kidato cha pili umeongezeka kutoka asilimia 76.8 hadi kufikia asilimia 94.6, huku ufaulu kidato cha nne ukiongezeka kutoka asilimia 55.4 hadi kufikia asilimia 94.6.

 Kutokana na hali hiyo, ufaulu katika kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimia 55.4 hadi kufikia asilimia 85.6 mwaka 2023 na kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 96.2 hadi kufikia asilimia 99.6 mwaka 2024.

Burhan Haji Omar mdau wa elimu, amesema pamoja na mafanikio hayo bado jitihada zaidi zinahitajika ili miundombinu iendane na mabadiliko ya mitalaa kulingana na teknolojia inavyobadilika.

“Changamoto ya elimu yetu sio tu kwenye miundombinu, lakini elimu inayotolewa inaendana na matakwa ya sasa ya soko la ajira? Hili ni jambo linalohitaji kuangaliwa kwa kina ili kukimbizana na ulimwengu,” amesema

Licha ya mabadiliko hayo wapo baadhi ya wananchi wanaoona kuwa bado mabadiliko ya elimu ni madogo ikilinganishwa na umuhimu wa sekta hiyo.

“Kwenye miundombinu wamejitahidi, lakini tukumbuke kuwa elimu sio tu miundombinu lakini tunatakiwa kuwa na vifaa vya kutosha, walimu wenye weledi, lakini ukiangalia bado walimu ni walewale waliokuwapo awali,”anasema,

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Walimu Zanzibar (Zatu), Salim Ali Salim anasema kuna mambo mawili ambayo yamechangia kuimarika kwa elimu. Anayataja mambo hayo ni pamoja na kuendeleza mfumo wa elimu uliopo na kuimarisha uwajibikaji na utoaji wa huduma katika elimu.

Katibu huyo wa Zatu, anasema pia maslahi ya wafanyakazi yameimarishwa, hivyo angalau hali za wafanyakazi zinazingatiwa na ushirikishwaji kupitia vyama vyao.

 Meneja wa mradi wa kuboresha elimu ya sekondari Zanzibar kutoka Good Neighbours Tanzania, Ye Jincho, anasema kwa sasa kuna mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na wao kupitia Shrika la Korea (KOICA), waliamua kushirikiana na Serikali kuinua kiwango cha elimu hususani katika masomo ya sayansi, hisabati na Kingereza ambayo yalionekana kuwa mwiba mgumu.

“Mafunzo waliyopatiwa walimu kupitia Tehama, yataongeza ubora, ujuzi na weledi katika kazi zao kusimamia shughuli za ufundishaji na ufunzaji na imani yetu kuwa sasa kuna walimu ambao ni nyenzo nzuri ya Serikali katika sekta hiyo katika kuboresha elimu ya Zanzibar,” amesema

Mwanafunzi kutoka sekondari ya Mtende, Issa Juma Nahoda anasema kwa sasa walimu wanafahamu kutumia Tehama, hivyo inakuwa rahisi pia kuwafundisha wanafunzi wakaelewa kwa haraka.

“Mabadiliko hivi sasa ni makubwa kwani ufaulu wa wanafunzi umeongezeka na kupunguza wimbi la wanafunzi wanaopata sifuri ikilinganishwa na kipindi cha nyuma,” anasema Nahoda.

Related Posts