Dar es Salaam. Shahidi wa 13, Ditektivu Sagenti Samweli, akiongozwa na mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter, ameieleza Mahakama kuwa, mwaka 2019 wakati wa tukio hilo, alikuwa akifanya kazi Kituo cha Polisi Kigamboni, akiwa na cheo cha Ditektivu Koplo (DCPL).
Mashahidi hao waliokuwa kwenye timu ya upelelezi wa kesi hiyo wametoa simulizi hiyo wakati wakitoa ushahidi wao jana Jumatatu, Novemba 18, 2024.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, mshtakiwa mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam anakabiliwa na shitaka la mauaji ya mkewe Naomi Marijan kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Anadaiwa kumuua mkewe huyo Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili wake kwa moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku kisha akaenda kuyazika masalia ya mwili huo na majivu shambani kwake na kupanda migomba juu yake.
Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake, Ditektivu Sagenti Samweli, akiongozwa na mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter, ameieleza Mahakama kuwa mwaka 2019, wakati wa tukio hilo alikuwa akifanya kazi Kituo cha Polisi Kigamboni, akiwa na cheo cha Ditektivu Koplo (DCPL).
Kwa mujibu wa ushahidi wake, Julai 16, 2019 saa nane mchana akiwa kazini, alielekezwa na Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC- CID) kuongoza na timu ya upelelezi kwenda Gezaulole, Kigamboni nyumbani ka mtuhumiwa kufanya upelelezi.
Waliongozwa na mtuhumiwa mwenyewe, Luwongo na walipofika, kiongozi wa msafara aliwaita mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na mjumbe kisha mtuhumiwa aliwaongoza ndani ya nyumba yake kwenye chumba alimokuwa akilala mkewe.
Chumbani humo mtuhumiwa aliwaonesha sehemu Naomi alipodondoka kulikokuwa na damu chini na kitandani na wataalamu wa uchunguzi wa sayansi jinai walichukua matone ya damu.
Kisha mtuhumiwa aliwaongoza mahali alikouchoma mwili wa marehemu, kwenye banda la kuku ambamo alichimba shimo akaujaza mkaa akauchoma mwili huo.
Kwenye banda hilo kulikuwa na damu ambayo mtuhumiwa alisema ni yake iliyomtoka baada ya kujiumiza wakati akitoa masalia ya majivu ya mwili wa marehemu.
Masalia hayo aliyaweka kwenye mfuko wa saruji akaenda kuyazika shambami kwake Kijiji cha Morogoro Wilaya ya Mkuranga.
Shahidi alichora ramani ya tukio mahali ambako mauaji yalifanyika na mwili ulikochomewa kisha mshtakiwa aliwaongoza katika kijiji hicho.
Huko kiongozi wa msafara aliita majirani pamoja na viongozi wa kijiji na mshtakiwa aliwapeleka shambani sehemu alikozika masalia ya mwili wa marehemu na kukuta mashina matatu ya migomba. Mshtakiwa aliwaeleza kuwa, mabaki ya mwili wa marehemu aliyazikia kwenye mgomba wa kwanza.
Walifukua kwenye mgomba huo na kuona majivu, mifupa na meno yaliyoungua, lakini walipochimbua kwenye shina lingine la mgomba hapakuwa na kitu.
“Wakati anatuongoza alikuwa kwenye hali nzuri na ndio maana tulipofika shambani alituonesha kuwa masalia ya marehemu aliyazika kwenye mgomba,” amedai shahidi huyo.
Amedai kuwa walifika huko shambani jioni walitumia mwanga wa tochi na taa za magari walilokuwa nalo na kwamba kazi hiyo ilimalizika saa 4:00 usiku.
Shahidi huyo amehitimisha kuwa alichora ramani ya eneo hilo na mtuhumiwa Luwongo, alizisaini.
Baada ya maelezo hayo, shahidi huyo amehojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi, Hilda Mushi.
Wakili Mushi: Umeieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa ndio mlikuwa mnamuhoji akawa anawaeleza, kuna mahali popote ulikoandika hayo maelezo ya mtuhumiwa alivyokuwa anakueleza?
Shahidi: Niliandika kwenye diary (shajara).
Wakili: Ni kweli kwamba hukuieleza Mahakama kuwa maelezo hayo ya mtuhumiwa ulikuwa unayaandika kwenye diary?
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa hapa mahakamani hukutoa nyaraka yoyote kuhusu hayo maelezo aliyokuwa akikueleza mtuhumiwa?
Wakili: Ulichora ramani eneo la tukio la mauaji ya nani?
Shahidi; Mauaji ya Naomi.
Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba kwenye ramani ya nyumbani kwa marehemu hakuna jina la marehemu?
Shahidi: Niliandika kosa la mauaji.
Wakili: Utakubaliana na mimi pia ramani uliyoichora ukiwa shambani haina jina la marehemu?
Wakili; Shahidi umesema kwenye banda la kuku mlikuta damu, damu hiyo ilipelekwa wapi?
Shahidi; Ilichukuliwa na timu ya forensic
Wakili: Utakubaliana na mimi kuwa wakati ukitoa ushahidi wako hukusema hiyo damu ilichukuliwa na timu ya forensic?
Wakili: Wewe ulikuwa mpelelezi katika shauri hili?
Shahidi: Nilikuwa miongoni mwa timu ya wapelelezi.
Wakili: Kwa hiyo unajua kila hatua ya kilichoendelea ikiwamo kuchukua sampuli kupeleka kwa mkemia na majibu yake?
Kwa upande wake shahidi wa 14, katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mzava ameieleza Mahakama kuwa wakati wa tukio hilo, mwaka 2019 alikuwa anafanya kazi Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO).
Kwa mujibu wa ushahidi wake Julai 16, 2019 asubuhi aliitwa na mkuu wake ASP Ahmed Makelle ambaye alimweleza kuwa ameunda timu ya wapelelezi wa jalada la uchunguzi wa kupotea Naomi na kwamba wakati huo mshitakiwa alikuwa anashikikiwa kama mtuhumiwa.
Amedai kuwa, timu ya wataalamu wa ukaguzi ilichukua vielelezo kwa ajili ya uchunguzi kama vile matone ya damu, nguo, viatu na mswaki chumbani kwa marehemu.
Kwenye banda la kuku timu hiyo ilichukua masalia ya majivu mahali ambako mtuhumiwa aliwaeleza kuwa ndiko alikouchomea mwili wa Naomi huko shambani Mkuranga.
Pia, walichukua masalia ya mifupa meno na udongo wa eneo hilo, kisha wakaandika maelezo ya mtuhumiwa.
Julai 17, shahidi hiyo alipewa jukumu la kumpeleka mtuhumiwa kwa Mlinzi wa Amani, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo kwa Hakimu Mfawidhi Matrona Luanda, akiwa katika hali nzuri kiafya.
Baada ya Mlinzi wa Amani kumaliza kuchukua maelezo ya mtuhumiwa, alimkabidhi shahidi huyo bahasha ya maelezo ya mtuhumiwa kisha akamrudisha mahabusu na bahasha akamkabidhi ASP Makelle
Julai 29, 2019 alipigiwa simu kutoka Ofisi ya Mkemia kwenda kuchukua majibu ya vielelezo alivyokuwa ameviwasilisha Julai 24, 2019.
Vielelezo hivyo ni sampuli zilizochukuliwa eneo la tukio nyumbani na shambani kwa mtuhumiwa, zikiwamo mpanguso wa mate kutoka kwa mtuhumiwa na kwa mtoto kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba.
Ripoti ya uchunguzi wa kimaabara kuhusu vielelezo hivyo, aliipeleka kwa mkuu wa upelelezi na vielelezo vilivyosalia alivikabidhi kwa mtunza vielelezo.
Kesi hiyo inaendelea leo Jumanne, Novemba 19, 2024.