Nairobi. Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi limekataa na kurejesha mchango wa fedha kutoka kwa kwa Rais William Ruto na Gavana Johnson Sakaja, likisema halitaki kutumika kisiasa.
Askofu Mkuu Philip Anyolo amesema: “Kanisa Katoliki linapinga vikali matumizi ya matukio kama harambee na mikusanyiko mingine kama majukwaa ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa. Wanasiasa wanahimizwa kuepuka kugeuza madhabahu kuwa jukwaa la hotuba za kisiasa, kwani vitendo hivyo vinadhalilisha utakatifu wa maeneo ya ibada.”
Jumapili, Novemba 17, 2024, Rais Ruto alitoa Ksh600, 000 (Sh12.3 milioni) kwa Kwaya ya Kanisa Katoliki la Soweto na Baraza la Wamisionari wa Parokia. Pia alitoa Ksh2 milioni (Sh41.2 milioni) kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya padri, huku Gavana Sakaja akitoa Sh200,000 (Sh4.1 milioni).
Rais aliahidi kununua basi la parokia na kuongeza ahadi ya Sh3 milioni (Sh61.6 milioni) nyingine kwa ujenzi wa nyumba ya kasisi.
Askofu Anyolo amelitaka kanisa kudumisha uadilifu kwa kukataa michango inayoweza kuhatarisha uhuru wake au kusaidia kujitajirisha kwa njia zisizo za haki.
Amewahimiza viongozi wa kisiasa kuonyesha uongozi wa kimaadili kwa kushughulikia masuala nyeti yaliyoibuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kenya (KCCB) kama migogoro ya kisiasa, ufisadi, siasa za ubinafsi, ukiukwaji wa haki za binadamu, na uhuru wa kujieleza.
“Kanisa lazima libaki kuwa chombo huru kisichohusishwa na ushawishi wa kisiasa, ili liweze kuhudumu ipasavyo kama mahali pa ukuaji wa kiroho na mwongozo wa jamii,” amesema Askofu Mkuu Anyolo katijka taarifa yake.
Endelea kufuatilia Mwananchi.