KONGAMANO LA KODI LAANZA JIJINI DODOMA

Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha Bw. William Mhoja (wa kwanza kulia walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali, (wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha Bw. Juma Mkabakuli, katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma. 

Na. Eva Ngowi, WF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imefanya kongamano la kodi kikanda kwa kuwakutanisha Wadau kutoka sekta binafsi wakijumuisha wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali pamoja na Makundi Maalum ili kuboresha mifumo ya kodi itakayochochea mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini.

Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Sera Bw. William Mhoja, katika kongamano la kwanza la kodi kikanda kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, lililofanyika jijini Dodoma.

Bw. Mhoja alisema kongamano hilo litasaidia kuboresha uratibu wa ukusanyaji maoni na kuongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika uaandaji wa bajeti ya Serikali na utunzi wa sheria.

“Hatua hii ni moja ya utamaduni wa kutambua mchango wa wananchi kupitia kodi, ada na tozo mbalimbali ambazo zinawezesha ujenzi wa Taifa letu” Alisema Bw. Mhoja.

Alisema kuwa lengo la kongamano hilo lilikuwa kupata maoni mbalimbali kwa nchi nzima ikiwa ni pamoja na kupita kwenye Kanda ikiwemo Kanda ya Dodoma ambayo ukusanyaji maoni umenza, Arusha, Mwanza, Kigoma, Mbeya, Iringa na baadae Mtwara na kuhitimisha zoezi hilo Dar es Salaam.

Alisema kuwa katika kongamano hilo maoni yote yatakayotolewa na wadau mbalimbali yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuyafanyia utafiti kabla ya kufanyiwa utekelezaji.

“Hivyo Serikali inawaahidi kwamba maoni yao yanazingatiwa sana kama ambavyo mmeona katika Hotuba za bajeti na Serikali inawakaribisha sana kushiriki na kutoa maoni. Kimsingi maoni ya wananchi wote yanazingatiwa na nawaomba sana wananchi wote wajitokeze kutoa maoni na maoni yao yatafanyiwa kazi kwa sababu mengine yanahitaji kufanyiwa utafiti kwanza kabla ya kuyaleta kwenye utekelezaji” alisema Bw. Mhoja.

Aidha, aliwashukuru Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) pamoja na TradeMark Afrika kwa kushirikiana na Serikali hususan katika kudhamini baadhi ya shughuli mbalimbali katika makongamano haya.

“Ni wazi kuwa ushirikiano huu unalenga kuendelea kukuza uchumi, kuzalisha ajira zaidi na kuwa na maendeleo endelevu” alisisitiza Bw. Mhoja.

Kwa upande wa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Alexander Mallya, aliwaasa wafanyabiashara kote nchini watoe maoni yao kuhusiana na masuala mazima ya mapendekezo ya mabadiliko ya kodi.

“Kwa niaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara tunawahamasisha wafanyabiashara wa mikoa yote Tanzania kushiriki makongamano haya yatakapowafikia kwenye Kanda zao, kwenye mikoa yao kushiriki kikamilifu na kutoa maoni yao kuhusu suala zima la mapendekezo ya mabadiliko ya kodi”, Alisema Bw. Malya

Kongamano hili ni mwendelezo wa Kongamano la Kodi Kikanda lililoanzishwa na Wizara ya Fedha mwezi Novemba mwaka 2023 ambapo vikao vilifanyika Kikanda katika Mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Shinyanga, Kigoma, Lindi na Mtwara.

Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Juma Mkabakuli (wa kwanza kushoto) akiwa na Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha Bw. William Mhoja wakisikiliza maoni mbalimbali yanayotolewa na wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama akizungumza na wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali (hawamo pichani) katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Bw. Alexander Mallya, akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa SACCOS ya UMAPIDO na mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodaboda na Bajaji Bw. Simon Mangula, akiwasilisha maoni yake kuhusiana na masuala ya kodi katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma.  

Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha Bw. William Mhoja (wa kwanza kulia walioketi), akiwa katika picha ya pamoja na wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali, (wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi Idara ya Sera, Wizara ya Fedha Bw. Juma Mkabakuli, katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Dodoma. 

Related Posts