Geita. Mahakama Kuu Kanda ya Geita, imepokea vielelezo vinne vilivyotolewa na upande wa jamhuri katika kesi ya mauaji inayomkabili Fikiri Kapala na mwenzake Agustino Jumanne wanaodaiwa kumuua Salome Lukanya kwa kumkata na kitu chenye ncha kali.
Kesi hiyo namba 2782 ya mwaka 2024 inasikilizwa na Jaji wa Mahakama hiyo, Griffin Mwakapeje.
Vielelezo vilivyopokewa ni hati ya daktari ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, fomu mbili za makabidhiano ya vielelezo na vifaa vilivyochukuliwa wakati wa upekuzi nyumbani kwa washtakiwa.
Akiongozwa leo Jumanne Novemba 19, 2024 na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Godfrey Odupoy, shahidi wa nane, Cosmas Cassian ambaye ni ofisa tabibu katika Zahanati ya Nyakaduha wilayani Geita, ameieleza Mahakama kuwa Aprili 22, 2024 akiwa kazini, aliombwa kuufanyia uchunguzi mwili wa Salome.
Amedai kuwa, baada ya kufika nyumbani kwa marehemu akiwa na ofisa upelelezi wa wilaya alikutana na askari wengine wakiwa na ndugu wa marehemu wakaingia chumbani kwa ajili ya uchunguzi.
Cassian ameieleza Mahakama kuwa, mwili wa marehemu ulikuwa umelala eneo lililokuwa na damu nyingi huku jicho la kushoto likiwa limetobolewa na kitu chenye ncha kali na eneo la shingo nalo lilikuwa limekatwa na kitu chenye ncha kali.
Amesema, kwa mujibu wa daktari, kifo cha Salome kilitokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na majeraha aliyoyapata.
Shahidi wa tisa katika kesi hiyo, G 8517 Coplo Mang’oina ambaye ni mtunza vielelezo makao makuu ya polisi Mkoa wa Geita ameieleza Mahakama kuwa alikabidhiwa fomu mbili za makabidhiano ya vielezo vilivyochukuliwa nyumbani kwa washtakiwa.
Pia, amekabidhi vielelezo ambavyo ni kirungu kidogo pamoja na tochi nyeusi, vilivyochukuliwa nyumbani kwa mshtakiwa wa pili, Agustino Jumanne.
Vielelezo vingine ni koti lenye rangi ya kaki, buti, suruali nyeusi na tochi vilivyochukuliwa nyumbani kwa mshtakiwa wa kwanza, Fikiri Kapala wakati wa upekuzi.
Shahidi wa tano katika kesi hiyo, John Bundala ambaye ni ofisa mtendaji wa Kijiji cha Isulwabutundwe Wilaya ya Geita ameieleza Mahakama kuwa Januari 2024, Fikiri Kapala alifika ofisini kwake akitaka kibali cha kwenda kumtafuta mkewe ambaye alikuwa ameondoka nyumbani bila taarifa.
“Nilimpa barua ya kwenda kumtafuta mkewe na alirudi baada ya wiki tatu akidai amempata mkewe na alirudi akiwa na barua ikionyesha amelipwa Sh100,000 baada ya kumfumania mkewe huyo akiwa na mwanamume ,” amedai shahidi huyo.
Amedai kuwa alimweleza kuwa baadaye mkewe alirudi kwa wazazi wake na alipomuomba waambatane kurudi nyumbani kwao, mkewe alikataa na aliyekuwa akimzuia ni mama mkwe aliyemtaja kwa jina la Salome Lukanya.
Amedai Aprili 22/2024 alipigiwa simu na kuelezwa kwenye kijiji hicho kuna tukio la mauaji katika Kitongoji cha Isadukilo na kuelezwa kuwa Salome ameuawa kwa kukatwa mapanga.
Amesema baada ya kupokea taarifa hizo alienda eneo la tukio na kutoa taarifa polisi na alipowahoji waliokuwa nyumbani hapo, walidai kuwatambua wauaji waliwataja kuwa ni Fikiri Kapala, Agustino Jumanne na mtu mwingine ambaye hawakumtambua.
Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili, Paul Hombo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza na Rukia Marandu anayemtetea mshtakiwa wa pili.
Kesi hiyo bado inaendelea kwa upande wa mashitaka kuendelea kutoa ushahidi wake.