Tumeenda kibabe Morocco 2025 | Mwanaspoti

Dar es Salaam. Tumeenda kibabe! Haya ndio maneno unayoweza kuyatumia kwa ilichofanya Taifa Stars baada ya kiwaduwaza Guinea ambao walitangulia kushangilia wakiona wamefuzu kisha kuja kukalishwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar, wenyeji wakishinda kwa bao 1-0 kisha kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 2025) zitakazofanyika nchini Morocco.

Stars kwa ushindi wa huu imejikatia tiketi ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya nne lakini mara mbili ikifuzu kupitia uwanja wa nyumbani, baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi H nyuma ya vinara DR Congo ikiziacha  Guinea nafasi ya tatu na Ethiopia iliyoburuza mkia.

Mara ya kwanza Stars ilifuzu Afcon 1980, iliyofanyika Nigeria, kisha 2019 nchini Misri, ikaenda tena Ivory Coast katika Afcon ya mwaka 2023, na sasa nchini Morocco 2025.

Bao la ushindi lililoibeba Taifa Stars lilifungwa na kiungo mshambuliaji Simon Msuva dakika ya 61, akimalizia pasi safi ya kiungo Mudathir Yahya iliyomkuta mfungaji akiwa nyuma ya mabeki wa Guinea na kuujaza mpira wavuni kwa kichwa safi kilichomuacha kipa Moussa Camara akishangaa.

Hii ni mara ya pili Msuva anafunga bao katika mchezo wa mwisho ulioipeleka Stars Afcon baada ya kufanya hivyo mwaka 2019, katika ushindi wa mabao 3-0 Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Uganda ambapo nyota huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 21, kisha Erasto Nyoni (dk 50 kwa penalti) na Aggrey Morris (dk 56).

Bacca, Job wamzima Guirassy

Tishio kubwa la Stars kwenye mchezo huo alikuwa mshambuliaji Sehrou Guirassy anayeongoza kwa ufungaji kwenye mechi za kuwania kufuzu akifunga mabao sita lakini jana alikutana na watu wa kazi mabeki wa kati Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na Dickson Job ambao hawakumpa nafasi ya kufanya shambulizi lolote la hatari.

Mabeki hao ni kama walikuwa wanapeana kazi ambapo Bacca alikuwa akimzima juu huku Job akifanya yake chini na kumweka kwenye wakati mgumu akishindwa kufanya alichofanya mechi tatu zilizopita dhidi ya wapinzani wengine ambapo alifunga mfululizo.

Stars inafuzu kwa mara ya kwanza ikiwa na kocha mzawa Hemed Morocco, baada ya mwaka 1980 kufuzu ikiwa chini ya Mpoland Slawomir Wolk akisaidiana na Joel Bendera, Emanuel Amunike raia wa Nigeria aliipeleka mwaka 2019, huku 2023 ikienda chini ya Adel Amorouche raia wa Algeria.

Stars yalamba milioni 505

Hatua ya kufuzu kwa Stars imejihakikishia jumla ya Sh505 milioni ambapo bao la ushindi huo limewapa Sh5 milioni lakini pia itavuna Sh500 milioni kwa kufuzu, ahadi zote zikitolewa ba Rais Dk Samia Suluhu Hassan.

Takwimu za mchezo huo zinaonyesha umiliki wa mpira Stars ilikuwa na asilimia 42.8 wakati Guinea ikiwa na asilimia 57.2.

Mashuti ya jumla Stars 11, Guinea 5 huku shuti lilolenga lango 1 kwa Stars, kona Stars 7 na Guinea 2.

Related Posts