Wabunge wabainisha kasoro ubora wa elimu, wapendekeza njia za kuweka sawa

Dodoma. Wabunge wamelia na ubora wa elimu huku wakitaka idadi ya masomo shule ya msingi ipunguzwe, maprofesa vyuo vikuu wabadilike na kufuata ratiba za masomo na vyuo viache kujitanua kwa kufungua kampasi za mikoani.

Hoja hizo za wabunge zimetolewa leo Jumanne, Mei 7, 2024  wakati wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2024/25 iliyowasilishwa na waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda.

Wizara hiyo imeomba Bunge liidhinishe ya Sh1.9 trilioni.

Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma leo, Mei 7, 2024. Picha na Edwin Mujwahuzi

Mbunge wa kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha akichangia mjadala huo ametoa mifano ya mafanikio ya elimu katika nchi tano za Afrika – Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Ghana na Uganda na kwamba mafanikio yao yanatokana na ubora wa walimu, matumizi sahihi ya vifaa vya kufundishia na vya kisasa, wanafunzi wanapta nafasi ya nafasi ya kutumia lugha ya kufundishia darasani na nje ya darasa kwa ufanisi.

“Na ndio maana shule binafsi za Tanzania zinaajiri walimu wa Kiingereza na Sayansi kutoka Kenya na Uganda,” amesema Nahodha, aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Amesema mwaka jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara ya Elimu, lilizuka swali kwamba, nini hasa chanzo cha kushuka kiwango cha elimu Tanzania.

“Baada ya majibu ya waziri, mheshimiwa Spika akauliza hivi ni kweli chanzo cha kushuka kiwango cha elimu ni lugha ya kufundishia au kuna jambo jingine halisemwi, kwa bahati mbaya mpaka leo (jana) Mheshimiwa Spika swali hilo halikujibiwa naomba nilijibu,” amesema Nahodha.

Nahodha alitaja mfano wa nchi tatu zenye elimu bora Afrika, kwamba ni Ushelisheli inayotumia lugha ya kufundishia ya Kifaransa, Tunisia inatumia lugha mbili Kiarabu na Kifaransa na Mauritius ambayo inatumia Kifaransa na Kiingereza, lakini bado zina ubora wa elimu.

“Siri ya mafanikio yao ni nini? Siri ya mafanikio yao ni ubora wa walimu, matumizi sahihi ya vifaa vya kufundishia na vya kisasa, wanafunzi wanapta nafasi ya kutumia lugha ya kufundishia darasani na nje ya darasa kwa ufanisi. 

“Mfano wa pili ambao unanishangaza sana wanafunzi wa Tanzania wanaokwenda China, Ujerumani   na Urusi (Russia) wanafunzwa lugha kwa muda wa mwaka mmoja na wana uwezo wa kutumia lugha hiyo kwa ufanisi sana.

“Kwa nini wanafunzi wa Tanzania wanaaza kujifunza Kingereza shule ya msingi mpaka chuo kikuu, lakini bado uwezo wao wa Kiingereza ni tia maji tia maji”.

Kwa sababu kama nilivyoeleza, wanafunzi wanapokwenda Urusi, Ujerumani na China wanaitumia lugha ya kufundishia, ndani na nje ya darasa kwa ufanisi, walimu wanaofundisha wamebobea vizuri sana, wanaijua lugha wanayoitumia katika kufundishia,” amesema.

Nahodha alipendekeza ili Tanzania itoke hapo kwanza Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ianzishe mafunzo ya diploma ya juu ya ufundishaji wa lugha ya Kiingereza na zoezi hili liwe la kudumu.

“Katika mafunzo hayo (Kiingereza) tutumie teknolojia ya kisasa ili tutumie walimu wenye ujuzi kwa ufanisi na kuwafikia Watanzania kila mahali walipo. 

“Turudishe utamaduni wa zamani, tuanzishe mashindano ya mijadala, midahalo katika shule za msingi na sekondari ili vijana wetu wapate uwezo wa kutumia lugha.

“Vitabu hasa vya Kiingereza na Kiswahili viandikwe na watu wanaozifahamu vizuri lugha hizo. Sisi tuliobahatika kusoma katika miaka ya 1970 mwishoni, tumetumia vitabu vya Kiingereza vinaitwa East African Oxford English.

Vimeandikwa kwa lugha fasaha, vina mifano ya kifalsafa, vitu ambavyo wanafunzi wanavihitaji sana. Sasa mimi nasema kama kuna uwezekano tuvitafute vitabu hivyo, vichapishwe kwa wingi tuvipeleke mashuleni,” amesema.

Akiendelea kuchangia, Nahodha amesema: “Wakenya wanaandika vitabu vizuri sana vya Kiswahili kuliko Watanzania wenye lugha, kwa nini.”

“Wizara ya elimu izungumze na ubalozi wa Uingereza, tupatiwe walimu wenye ujuzi tuwatawanye kwenye shule zetu, tuwatawanye kwenye vyuo vinavyofundisha ualimu, ili walimu wajifunze namna ya kutamka vizuri maneno ya Kiingereza,” amesema.

Nahodha pia amesema tatizo lilopo hasa katika elimu ya msingi ni mzigo wa masomo kuwa mkubwa. 

“Haiwezekani mtoto wa shule ya msingi anasomeshwa masomo zaidi ya tisa matokeo yake anabeba begi lenye vitabu, madaftari utafikiri anakwenda kwenye mafunzo ya kijeshi.

Napendekeza hapa kwamba umefika wakati tupunguze idadi ya masomo, mimi kwa maoni yangu wanafunzi wa shule za msingi wanahitaji masomo matano, Kingereza wafundishwe vizuri, Kiswahili wafundishwe vizuri, Sayansi wafundishwe vizuri, Hisabati wafundishwe vizuri na la tano dini na maadili wafundishwe vizuri, kama ni Mkristo, dini ya Ukristo na maadili, kama Uislamu, dini ya Uislamu na maadili,” amesema

Nahodha amesema wanapofika darasa la tano la sita tuwaongeze somo moja ili waendane na mabadiliko ya dunia. Napendekeza masomo kama jiografia, historia, civics hakuna haja kufundishwa kwenye shule ya msingi, yasubiri mpaka wanafunzi wafike kidato cha kwanza.

“Kwa nini? Mtaalamu mmoja wa saikolojia Jean Piaget (Jean William Fritz Piaget) alisema: ‘Mtoto anapofikia umri wa miaka 13 ambao ni muda wa kuanza kidato cha kwanza, ndipo ana uwezo wa kumudu masomo mengi. Tusimpe masomo mengi anapokuwa shule ya msingi,” amesema.

Jean Piaget alikuwa mwanasaikolojia wa Uswizi anayejulikana kwa kazi yake juu ya ukuaji wa mtoto na aliweka umuhimu mkubwa katika elimu ya watoto.

“Ushauri wangu wa tatu, mheshimiwa Spika kwa bahati mbaya sana uteuzi wa masomo ya ubobezi au kwa Kiingereza ‘specialization’ hapa Tanzania tunachelewa sana kuanza. Uchaguzi wa masomo unaanza kidato cha tano na kidato cha sita kwa bahati mbaya muhtasari wa kidato cha tano mpaka cha sita ni mpana sana una mambo mengi. 

“Walimu wanalazimika kufundisha haraka kwa sababu ni muda wa miaka miwili, yaanze kidato cha nne ili walimu wapate muda mzuri wa kufundisha vizuri na wanafunzi wajifunze vizuri,” amesema. 

Nahodha amesema weledi wa mwanafunzi dunia haupimwi kwa kusoma mambo mengi, unapimwa kwa kusoma mambo machache na kujifunza mambo mengi.

Hata hivyo, Spika Tulia Ackson alimuhoji Nahodha kwamba masomo ya shule ya msingi yafundishwe kwa lugha gani?

Nahodha alijibu: “Napendekeza kwa hali ya sasa ilivyo, mtoto anapofikia darasa la nne, ndio wakati sahihi hapo anaweza kuanza kuyasoma masomo hayo kwa lugha ya Kiingereza. Na darasa la kwanza mpaka la tatu tutumie lugha ya mama ya Kiswahili.” 

Naye mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya akichangia mjadala huo amesema miongoni mwa matatizo ni wanafunzi wa vyuo kuishi nje ya chuo ambako wanakumbana na changamoto za maisha kama kukosa kodi ya pango.

Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya  akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2024/2025, jijini Dodoma leo Mei 7, 2024. Picha na Edwin Mjwahuz

Profesa Manya ametoa mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwamba maabara zinazopaswa kuhudumia wanafunzi 20 kwa sasa zinahudumia wanafunzi 200 hadi 300.

“Mazingira haya, hayawezi kuleta ule ubora unaokusudia kwenye elimu ya mafunzo kwa vitendo.”

Pia, amesema mhadhiri mmoja anajikuta na darasa la wanafunzi 800 hadi 1,000 ambao ni wengi. Na uwiano wa idadi ya wanafunzi kwa mhadhiri mmoja ndio kigezo cha kimataifa katika kupima ubora wa vyuo vikuu. 

“Hata miundombinu ya vyoo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vinatakiwa kuhudumia watu 4,000 sasa vinahudumia watu 20,000 na havijaongezeka sana,” amesema.

Pia, ameisema wahadhiri hadi wanne wanachangia ofisi inayopaswa kutumiwa na mhadhiri mmoja na kukosa hata nafasi ya mhadhiri kuzungumza na mwanafunzi wake.

Amehoji posho za kujikimu za maprofesa wa Chuo Kikuu akisema wanalipwa Sh170, 000 kwa siku wanapokuwa safari wakati ofisa mwanadamizi wa wizara analipwa posho ya Sh250, 000 akisema hiyo siyo haki. 

“Pendekezo, kama tunatamani kutoa zao bora la wanafunzi wanaotoka vyuoni, Serikali inayo sababu ya kuongeza bajeti ili kuboresha mazingira ya kujifunza na mazingira ya kujifundishia.

“Mfano mafunzo ya vitendo, vyuo vimepunguza muda wa kwenda kwenye mafunzo ya vitendo kwa sababu ya bajeti ndogo, mtu badala ya miezi mwili anakwenda mwezi mmoja sababu ya ufinyu wa bajeti.

“Tunasema wanafunzi siyo bora, lakini hawakuwa na muda wa kutosha wa kufanya mafunzo kwa vitendo,” amesema. 

Pia, amezungimzia ubaya wa vyuo vikuu kujitanua kwa kuongeza kampasi mikoani, akisema huko ni kuongeza gharama za utawala badala ya kuandaa wanafuzi bora. Na amevitaka vyuo viwe sehemu moja ili wanafunzi wote waende pale badala ya kufungua kampasi kila mkoa. 

Naye Mbunge Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza, ameitaka Wizara ya Elimu ianzishe elimu ya watu wazima kwa ajili ya matumizi ya kijiditali na hasa matumizi ya vishikwambi. Tunahitaji dijitali sehemu zote nchini mijini na vijijini.

Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma leo Mei 7, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu amebainisha umuhimu wa kuifanya elimu ya juu kuwa chanzo cha mapato kwa wanafunzi wa  nje kuja kujifunza kwenye vyuo vya Tanzania kama ilivyotokea kwa wanafunzi wa udaktari kutoka Sudan waliokuja kujifunza Muhimbili. 

Msambatavangu amesema ili kufikia hali hiyo ni vizuri maprofesa wakabadilika kwa kufuata ratiba ya semista ya ufundishaji badala ya ratiba binafsi.

“Maprofesa nao wabadilike kutoka kwenye utaratibu waliozoea. Inatolewa ratiba ya semista nzima ili mtu afuate, lakini inafika siku anayoamua iwe Idd au Krisimasi anaita wanafunzi, leo natoa testi. Mambo kama haya ukiwachukua wanafunzi wa nje hawawezi kukaa,” amesema.

Related Posts