Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa soko la Kariakoo, Benedicto Mwanalingo (26) mkazi wa Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam amesimulia namna alivyoishi chini ya kifusi kwa siku tatu, sawa na saa 72 bila kula wala kunywa.
Mwanalingo ambaye ameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya kupatiwa matibabu, amesema alikuwa akijigeuza upande mmoja kwa mwingine mpaka alipofikiwa na kikosi cha waokoaji na kupewa paipu ya oksijeni na maji ndipo nguvu zilianza kumrudia.
Mwanamlingo ni miongoni mwa majeruhi wa ajali ya jengo la ghorofa nne liliporomoka saa 3 asubuhi, Jumamosi ya Novemba 16, 2024 na kusababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 86, katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaam ambalo uokozi bado unaendelea.
Kijana huyo aliyetolewa katika kifusi usiku wa kuamkia leo Jumanne, amesema hayo leo Jumanne Novemba 19, 2024 baada ya kuruhusiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.
Mwanamlingo amesema wakati ajali hiyo inatokea alikuwa ghorofa ya kwanza, alidondokewa na kifusi na kushushwa mpaka eneo la chini ‘underground’ na kufunikwa na kifusi ambacho kilikuwa juu yake.
“Toka siku ya kwanza tuliona huduma inatolewa na wananchi na kadri masaa yanavyozidi kusogea tuliona msaada na matumaini yanazidi kuwepo, lakini kikubwa namshkuru Mungu licha ya kuwa hai lakini bila nguvu kazi ya wananchi pamoja na Jeshi la Uokoaji Zimamoto na majeshi mengine kiukweli wamenisaidia.
“Ilifikia mahali mpaka naonana na zimamoto nilikuwa sina nguvu kabisa, wakaniambia vuta paipu ya oksijeni, nikavuta. Wakanipa paipu ya maji ndipo yakazidi kunipa nguvu, tukawa tunawasiliana wanauliza unatuona, nawaambia nawaona, wananiagiza sogea upande wa pili, nasogea na hatimaye mwisho kabisa nikatoka,” amesimulia.
Hata hivyo, Mwanamlingo amesema hawezi kukumbuka ni siku gani amekaa ndani ya kifusi kwa kuwa hakujua mchana au usiku.
“Siwezi kusema ni siku gani ila ni jana nimetolewa, maana mimi kule nilikuwa sihesabu siku sijui ni mchana sijui ni saa ngapi ni mimi tu kulala najiegeza upande huu, nachoka nageukia upande huu nikisubiri maombi ya watu wote,” amesema.
Amesema wakati anaokolewa, eneo alilokuwa alikuwa peke yake, aliona mwanga wa tochi ukimulika, akasogea ulipokuwa ukitokea, akasikia sauti zikiuliza kama anauona.
“Nilizisikia nikajibu ndio, pale ndipo wale wataalamu walipoweza kuniokoa,” anasema.
Anasema simu yake ilizima chaji, hivyo hakuwa akiona chochote akiwa kule hadi alipoona mwanga wa tochi na sauti ikimuuliza kama anauona huo mwanga.
“Kabla simu haijazima niliwasiliana na kaka Jonas nikamwambia nipo chini dukani, jengo liliporomoka nilikuwa eneo langu la kazi hivyo naomba msaada wake,” anasema.
Anasema alikaa peke yake hadi alipookolewa, ingawa duka la tatu kutoka alipokuwepo pia kulikuwa na mtu mwingine.
Kijana huyo amesema anachoshukuru baada ya kutoka pale akapata huduma ya kwanza kwenye gari la wagonjwa na kupewa huduma ya haraka.
“Nimefika hapa Muhimbili wakaniangalia vipimo ndani na nje, wakanipa matibabu lakini namshkuru Mungu naendelea vizuri.
“Napenda kuchukua nafasi hii kulishukuru Jeshi la Zimamoto japokuwa ukiwa chini hauwezi kujua ni nani, najua ni wananchi na zimamoto lakini kwa Watanzania wote nashukuru kwa maombi yenu nasikitika wengine sijajua mpaka sasa hivi wana hali gani, lakini napenda kuwatia moyo watatoka salama,” amesema Benedicto.
Anasema alipoona hatari ile hakuwa na cha kufanya, zaidi ya kupigia simu watu wake wa karibu ambao mwanzoni waliwasiliana kisha simu yake ikazima.
“Sikuwa na cha kufanya, nikiangalia kote kumezibwa ni kifusi, nondo na kuna giza, hadi nilipokuja kuona mwanga wa tochi wa waokoaji,” anasema.
Jonas ambaye ndiye mwenye duka alilokuwa akiuza Mwanamlingo, amesema siku ya tukio yeye alichelewa kufika dukani.
“Nikiwa njiani nakwenda ndipo nilipata taarifa, ikawa hekaheka za kumtafuta Ben, nilikuwa na imani yupo salama kwa kuwa tuliongea akiwa amenasa chini asubuhi ya saa 4 hivi.
“Saa 7 mchana simu yake haikupatikana tena, kwakuwa nilikuwa nafahamu location ya duka langu, nikawaelekeza waokoaji ndipo wakachimba tukampata saa mbili usiku ya Novemba 18,” amesema.
Jonas amesema,”zoezi la kuchimba jana lilifanyika siku nzima tukiwa pale, zege lilikuwa kubwa, wanachimba wanakutana na zege, nondo hadi saa mbili usiku ndipo tukafanikiwa kumpata na kupelekwa hospitali, leo ameruhusiwa kurejea nyumbani,” amesema.
Wakati huohuo, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Dogo Idd Mabrouk pamoja na ujumbe wake mapema leo wamefika Muhimbili kumjulia hali Benedicto.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada alizochukua za uokozi kupitia vyombo vyote vya ulinzi na usalama, wananchi wote pamoja na watoa huduma za afya kwa namna walivyoshirikiana na wanavyoendelea kushirikiana katika juhudi za uokozi na tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapokee panapostahiki wale wote waliotangulia mbele ya haki, tunawapa pole kutokana na tukio hilo,” amesisitiza Mabrouk.
Ameipongeza Muhimbili, watoa huduma wote na hospitali zote kwa namna ambavyo wamepokea majeruhi hao na kuwapa matibabu stahiki na kuruhusiwa kwenda nyumbani ili kuendelea na shughuli zao za kijamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema mara tu walipopokea taarifa ya tukio hilo, hospitali ilijipanga na kuandaa timu mbili za watoa huduma, moja ikiwa eneo la tukio na timu nyingine hospitalini kupitia idara ya tiba na magonjwa ya dharura kuhakikisha inatoa huduma stahiki.