Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika leo Novemba 19,2024 katika ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam ikishuhudiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb).
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa Taifa ambapo yatawajengea uwezo walimu, wanafunzi na Menejimenti ya NCT katika aina mbalimbali za vyakula, lugha, suala la ukarimu kwa wageni na utalii.
“Kipaumbele chetu ni kuongeza idadi ya watalii kutoka Mataifa yote duniani ikiwemo soko la Italia hivyo makubaliano haya ni mojawapo ya mkakati wa kutoa huduma bora kwa watalii hatimaye kuongeza idadi ya watalii nchini” Mhe. Chana amesisitiza.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dkt. Florian Mtey amesema kuwa makubaliano hayo yatasaidia katika ukuzaji na utekelezaji wa mitaala katika nyanja za Ukarimu na Utalii, kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kufundisha ukarimu, na usimamizi wa vyuo vya utalii na ukarimu.
“Juhudi hizi za ushirikiano zitaimarisha kwa kiasi kikubwa utoaji wa mafunzo katika sekta ya utalii na ukarimu, na hivyo kuchangia ukuaji wa sekta hiyo, ambayo inabakia kuwa kipaumbele katika uchumi wa nchi yetu” amesema Dkt. Mtey.
Aidha, amesema pia makubaliano hayo yatasaidia katika kubadilishana uzoefu wa ubunifu na kusasisha teknolojia za ufundishaji na maabara, kuongeza ujuzi katika ukarimu na utalii sambamba na kubadilishana uzoefu na ujuzi wa mbinu bora katika mafunzo ya kiufundi ya utalii na ukarimu.
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mhe. Giuseppe Sean Coppola, amesema kuwa kubadilishana uzoefu baina ya nchi hizo mbili ni muhimu katika kukuza Sekta ya Utalii ambayo ni sekta muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Rais wa ENAIP Veneto Impresa Sociale, Mhe. Antonino Ziglio, Maofisa kutoka Ubalozi wa Italia nchini Tanzania, Viongozi kutoka ENAIP Veneto Impresa Sociale-Italia, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii,Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Wakuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Wajumbe wa Menejimenti ya NCT na Watumishi wa NCT.