MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dk. Thomas Bwana amezieleza kampuni za mbegu kulipia mirahaba ya mbegu wanazotumia zinazotokana na kazi za watafiti wa TARI ili kutoa motisha kwa wagunduzi wa mbegu bora wanazouza kwa wakulima. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Dk. Bwana amesema hayo leo Novemba 19, 2024 katika ufunguzi wa warsha ya siku moja ya mfumo wa kidigitali wa upatikanaji mbegu na usajili wa mbegu iliyofanyika Dodoma.
Warsha hiyo imewakutanisha Kampuni za Mbegu, wazalishaji wa mbegu, Taasisi mbalimbali za Kilimo na Watafiti ikiratibiwa na TARI ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa AVISA unaolenga kuchochea matumizi ya mbegu bora zilizogunduliwa.
Akieleza kuhusu shughuli zinazofanywa na TARI Dk. Bwana amesema TARI inafanya utafiti na kutoa matokeo ya utafiti kwa wadau wa kilimo pamoja na kushauri watunga sera kuhusu masuala ya Kilimo lengo ikiwa ni kuongeza tija.
“Watafiti wanafanya kazi kubwa ya ugunduzi wa Mbegu bora za Mazao mbalimbali ambazo nyie kampuni kama wadau muhimu wa Kilimo mnaziuza kwa Wakulima hivyo sio vibaya mkitoa motisha kidogo kwa Watafiti.”
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha hiyo, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu amesema ugunduzi wa mbegu bora unachangia tija katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo ikiwemo utoshelezaji wa chakula, usalama wa chakula na hivyo kufikia ajenda ya Kilimo Biashara ya 10/30.
John Julius- Mkurugenzi Kampuni ya Mbegu ya TEMNAR iliyopo Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara amesema suala la kulipia mirahaba ni jambo muhimu na linafahamika huku akishauri kujipanga pande zote TARI na kampuni watumiaji kujadili namna njema ya ulipaji mirahaba.
Julius ameeleza kunufaika na warsha hiyo kwa kujifunza fursa pana zilizopo katika sekta ya Mbegu.
Mradi wa AVISA ulianza mwaka 2019 ukitekelezwa na TARI kwa kushirikiana na Taasisi zingine kama Shirika la Kimataifa la Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT), Kituo cha kimataifa cha Utafiti wa Kilimo katika nchi za Kitropiki (CIAT), Kituo cha Syngenta na kituo cha Mawasiliano na Ubadilishaji wa Tabia (CBCC).