Rais Mwinyi apangua wakuu wa mikoa, wilaya

Unguja. Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amefanya mabadiliko ya wakuu wa mikoa na wilaya.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Jumanne Novemba 19, 2024 na kusainiwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Said, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid amehamishiwa Mkoa wa Kusini Pemba na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Mattar Zahor Masoud amehamishiwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hamid Seif Said amehamishiwa  Wilaya ya Mjini Unguja kutoka Wilaya ya Kaskazini B. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka amehamishiwa Wilaya ya Kaskazini A Unguja.

Pia, Sadifa Juma Khamis amehamishiwa Wilaya ya Magharib A akitoka Wilaya ya Kati na Othman Maulid akihamishiwa Wilaya ya Kusini Unguja akitoka Wilaya ya Kaskazini A.

Cassian Gallos Nyimbo amehamishiwa Wilaya ya Kati Unguja akitoka Wilaya ya Kusini Unguja huku Khatib Juma Mjaja akihamishiwa Wilaya ya Micheweni Pemba akitoka Wilaya ya Mkoani Pemba.

Mwingine Abdalla Rashid Ali amehamishiwa Wilaya ya Wete Pemba akitoka Wilaya ya Chakechake Pemba huku Hamad Omar Bakari amehamishiwa Wilaya ya Mkoani Pemba akitoka Wilaya ya Wete Pemba.

Mgeni Khatib Hassan ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Pemba akitoka Wilaya ya Micheweni Pemba na Juma Sururu Juma ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B.Unguja kabla ya uteuzi huo alikuwa ofisa mwandamizi katika ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora.

Taarifa hiyo imemtaja Hawah Ibrahim kuwa Naibu Katibu Mkuu (Mawasiliano na Uchukuzi) katika Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Udhibiti wa Mifumo ya utoaji wa leseni za biashara, Zanzibar.

Wateule wote wataapishwa Jumamosi Novemba 23, 2024 saa 4:00 asubuhi Ikulu, Zanzibar.

Related Posts