Mabeyo ametuepusha

NIMEGUSWA na uadilifu, utiifu na uaminifu wa Mkuu mstaafu wa majeshi Jenerali Venance Mabeyo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaandika Joster Mwangulumbi… (endelea).

Jenerali Mabeyo ndiye, saa 24 kabla ya John Magufuli kufariki dunia 17 Machi 2021 katika hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, alikuwa ameishika mkononi hatima ya Tanzania. Kwa maelezo yake, yeye na wakuu wenzake wawili wa vyombo vya ulinzi na usalama, walishirikishwa kwa lengo la kujua hali ya rais inavyoendelea.

Viongozi wenzake ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), Diwani Athuman na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP), Simon Sirro.

Kwamba wakati Magufuli akiwa na hali mbaya, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alikuwa ziarani mkoani Tanga. Pia, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi (CS), Dk. Bashiru Ally, walikuwa Dodoma.

Vilevile mke wa Magufuli, Mama Janeth Magufuli na watoto wake, nao hawakuwapo karibu na kitanda cha mpendwa wao, wakati akiaga dunia.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na Aliyekuwa mkuu wa majeshi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo

Mabeyo akatuambia kwamba baada ya Magufuli kufariki dunia, kuna watu waliotaka kupindisha Katiba ili aliyekuwa Makamu wa Rais, asiapishwe kuwa rais. Jenerali Mabeyo alisema kwamba “…kulikuwa na ugumu wa kutangaza nani atarithi kiti hicho, licha ya Katiba ya kuanisha wazi.”

Watu hao walitaka kusigina Katiba kwani Ibara ya 37 (5) ya Katib inasema: “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobakia…”

Kwa kuzingatia Ibara hiyo, Jenerali Mabeyo alizuia mtu mwingine yeyote kuapishwa kama si makamu wa rais. Kwa maneno mengine ni kwamba Jeshi la Wananchi lilisimamia Katiba. Kwa hiyo, wakati baadhi wakishinikiza waliokodolea urais watajwe na wengine wakitaka iundwe tume kuchunguza kifo cha Magufuli, kwanza tumshukuru Mungu, Jenerali Mabeyo hakuwa mroho.

Tujiulize nini kingetokea ikiwa mmoja wa “watu hao wanaojulikana” angeapishwa kuwa rais? Nini kingetokea endapo Mabeyo mwenyewe angeamua awe rais?

Kwanza; Katiba ya Jamhuri ya Muungano ingesitishwa. Pili, vyama vya siasa vingefutwa kama Mali, Niger na Burkina Faso. Kusingekuwa na Bunge, wakuu wa mikoa wala wakuu wa wilaya. Tungeanza kuisikia amri kutoka Ikulu.

Je, mabadiliko yangekuwa tulivu kama Zimbabwe? Mwaka 2017 wakati wabunge wa chama cha tawala cha ZANU PF, wakiungana na upinzani kumshinikiza Rais Robert Mugabe ajiuzulu, makamanda waliingiza vifaru mjini. Kuona hivyo, Mugabe aliandika barua ya kujiuzulu.

Nini kingetokea ikiwa vikosi vingine vingemkatalia Mabeyo? Hali si ingekuwa kama Sudan ambako majenerali waliungana kumwondoa Jenerali Omar al Bashir lakini baadaye waligeukana? Dunia imewaacha Sudan wanauana hadi leo.

Jenerali Mabeyo, kwa uzalendo, alisimamia Katiba, ndipo mama Samia aliapishwa kuwa rais wa awamu ya sita. Tusifukue makaburi kwa gharama ya amani na demokrasia yetu. Jenerali Mabeyo ametuepusha.

Related Posts