KATAMBI AONGEZA NGUVU KAMPENI CCM UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA JIMBO LA SHINYANGA MJINI

Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akikabidhi spika kwa ajili ya Kampeni za Uchaguzi Serikali za Mitaa

Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeanza mikakati madhubuti ya kampeni, ikiwa ni sehemu ya kujiandaa kwa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024 ambapo Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi, akitoa shilingi Milioni 20 na Spika za Kisasa 17 zenye thamani ya shilingi milioni tisa ili kurahisisha na kuimarisha kampeni katika kata zote 17 za jimbo hilo.

 

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi spika hizo leo Novemba 19,2024 Katambi amesema vifaa hivyo vitasaidia kuimarisha ufanisi wa kampeni ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuendelea kusukuma mbele maendeleo yaliyopangwa.

Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanatafuta kura ili kukipa ushindi chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa lakini pia katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.

Amesema mafanikio ya maendeleo katika maeneo mbalimbali yanatokana na utekelezaji wa ilani ya CCM, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuchagua viongozi wa serikali za mitaa watakaoendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Sisi kama Chama tawala, tunahitaji umoja na mshikamano ili tushinde uchaguzi huu. Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuletea miradi mingi sana ya maendeleo katika kata zetu, na maendeleo haya yanaendelea kwa sababu ya utekelezaji wa ilani ya chama chetu. Tunahitaji viongozi wa CCM ili miradi hii iweze kukamilika. Hivyo twendeni tukawahimize wananchi kuchagua viongozi walioteuliwa na Chama cha Mapinduzi”,amesema Katambi.

Mbunge huyo pia amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya vifaa vilivyotolewa, ili viweze kutoa tija kwa chama na wanachama kwa jumla na kuvitumia kwa usahihi, ikiwemo katika matukio ya kijamii kama sherehe za kipaimara na shughuli mbalimbali.

“Vifaa hivi ni mali ya chama, hivyo ni muhimu vitumike kwa usahihi. Kuna matukio mengi yanahitaji vipaza sauti, kama sherehe ndogo ndogo kama kipaimara, Send Off, tuweke uratibu mzuri lakini Kama ikitikea janga lolote vitumike bure lakini kwa usimamizi sahihi tusiwatoze pesa wananchi kwa majanga kama hayo. Tutambue kabisa imetolewa kwa chama ngazi ya kata”,ameongeza Katambi.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Hamisa Chacha, amewashauri wanachama kumaliza tofauti na makundi yaliyotokana na uchaguzi wa kura za maoni, na badala yake kuwa kitu kimoja kwa kuunga mkono wagombea waliopendekezwa na chama.

Amesema kuwa viongozi wa CCM wameshafanya uteuzi wa wagombea kwa kuzingatia uwezo wao na ufanisi wao katika kutumikia umma.

 

“Viongozi wetu wametupima na kuona kuwa wagombea hawa wanastahili kushika nafasi mbalimbali katika serikali za mitaa. Tushikamane na kuunga mkono wagombea hawa, ili chama chetu kipate ushindi katika maeneo yetu yote. Twendeni tukawaombee kura za ndio kwa wananchi ili chama chetu kiweze kupata ushindi mnono”,amesema Hamisa.

Tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa la mwaka 2024 lilitolewa tarehe 15 Agosti na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa.

Kampeni rasmi zitaanza tarehe 20 Novemba 2024 na zitadumu hadi tarehe 26 Novemba 2024, ambapo uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba 2024.

Chama Cha Mapinduzi kimejizatiti kuhakikisha kuwa wanachama wake wanashiriki kikamilifu katika kampeni na kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa na mafanikio makubwa, ili kuhakikisha maendeleo yanaendelea kwa ustawi wa wananchi.

Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi akizungumza kwenye Hafla akizungumza kwenye Hafla ya makabidhiano ya vipaza sauti kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Ngazi ya Kata

Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi akizungumza kwenye Hafla akizungumza kwenye Hafla ya makabidhiano ya vipaza sauti kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Ngazi ya Kata

Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mhe. Patrobas Katambi (katikati) akikabidhi spika kwa ajili ya Kampeni za Uchaguzi Serikali za Mitaa

 

 

 

 

Muonekano wa sehemu ya spika hizo

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga mjini Ndg. Hamisa Chacha akizungumza kwenye Hafla ya makabidhiano ya vipaza sauti kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Ngazi ya Kata

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Shinyanga mjini Ndg. Anord Makombe akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya vipaza sauti kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Ngazi ya Kata

Viongozi wa mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi kutoka kwenye Kata, Vijiji, Vitongoji na Mitaa

 

Related Posts