Mbowe: Tutailinda Chadema | Mwananchi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amekiri kuwepo kwa minyukano ndani ya chama hicho, akisema wanaimaliza ndani kwa ndani na watakilinda chama hicho kwa gharama yoyote.

Kauli ya Mbowe imekuja kufuatia ukimya wake wa zaidi ya miezi miwili, huku kukiwa na mivutano ya hoja ndani ya chama hicho, ikiwamo kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, Tundu Lissu aliyoitia Novemba 12, 2024 mjini Singida, akisema chama hicho kilidanganywa na CCM kwa lugha laini ya maridhiano.

Lissu pia katika mkutano wake huo, alisema uchaguzi umevurugwa na umekwisha, hivyo akakitaka chama chake kijipange upya.

Mbali na kauli hiyo, Lissu amekuwa akitoa kauli za madai ya kuwepo wa rushwa ndani ya chama hicho, akiwaonya makada kutojihusisha nayo.

Hata hivyo, Chadema ilitoa taarifa kwa umma iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema ikikanusha hoja hizo, ikijibu hoja hizo.

Mbali na kauli za Lissu, kumekuwa pia na mnyukano wa kauli miongoni mwa viongozi katika chaguzi za ndani zinazoendelea, Novemba 16, 2024 Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema alimtaja Naibu Katibu mkuu wa chama hicho-Bara, Benson Kigaila, akimhusisha na vurugu zilizoibuka katika uchaguzi wa chama hicho Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 19, 2024 katika ofisi za makao makuu ya chama hicho Mikocheni Dar es Salaam, Mbowe amesema kauli za makamu wake, Lissu hazionyeshi kuwepo mgogoro kwa sababu ni msimamo wa chama.

“Kwamba makamu mwenyekiti wetu alisema uchaguzi umevurugwa, ni kweli. Kwani nani ambaye hajasema hivyo? Kila mwenye akili timamu amesema uchaguzi umevurugwa.

“Lakini makamu mwenyekiti hajawahi kusema tujitoe kwenye uchaguzi, kwa sababu anajua tumejadili nini kwenye vikao,” amesema Mbowe.

Katika kusisitiza hakuna mgongano wa kauli, Mbowe amesema Lissu atazindua kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa kesho Jumatano Novemba 20 mkoani Singida kisha atakwenda wilayani Tarime Mkoa wa Mara kuendelea na kampeni.

 “Suala la kujipanga upya alilosema makamu, ni sahihi. Uchaguzi mmoja unazaa uchaguzi mwingine, mchakato mmoja ukiisha haukati tamaa unajipanga upya, ndiyo inamaanisha hivyo, tatizo liko wapi,” amehoji.

Akifafanua zaidi kuhusu mivutano ya hoja ndani ya chama hicho, Mbowe amesema mivutano ndani ya vyama ni jambo la kawaida.

“Ukishakuwa na chama kisichokuwa na minyukano, hicho chama ni mfu. Kuna wakati viongozi wetu wanapotea wanakwenda kidogo mbali lakini hiyo ndiyo siasa ilivyo, mkiwa kwenye siasa mnakubaliana asilimia 100 siku zote hiyo safari hamtoboi,” amesema Mbowe.

Amesema kuna wakati viongozi wa chama hicho wanateleza katika kauli, “Mbowe anaweza kuteleza kauli, makamu akateleza kauli, katibu mkuu akateleza kauli, lakini eti tuna mnyukano ambao utaua chama hiki…sikiliza niwaambie hiki chama kina miaka 30, kimefika hapa kwa maumivu makubwa yetu wote na sisi wote tumeshaapa tutakilinda hiki chama kwa gharama yoyote ile.”

“Kwa hiyo kama kuna mtu anafikiri kuna mgogoro utakaotugawa Chadema hatuko wamoja, watu watanyukana tu. Kuna mambo mengine tunayarekebisha kwenye vikao vyetu. Kwenye mazingira kisiasa watu wanaweza kufika mahali hasira zinapanda, watu wake waemenguliwa mahali anakasirika, mtu ametoa kauli inayomkwaza mwingine, hayo yanatokea,” amesema.

Amesema chama hicho kinabeba masilahi ya Watanzania hivyo wao ni wajenzi tu.

“Chama siyo cha Mbowe wala sio cha Lissu, wala sio cha (John) Mnyika, hiki chama ni cha Watanzania wengi ambao ni Wanachadema na wengine sio Chadema, ambao wana masilahi na chama hiki kwa sababu chama hiki kina masilahi ya Taifa. Sisi ni wajenzi na walinzi wa chama hiki na tutakilinda kwa wivu mkubwa. Kwa hiyo hatuna ugomvi, hayo ni mambo ya kawaida,” amesema.

Akizungumzia uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliozua minyukano miongoni mwa makada, Mbowe amesema chama hicho ni kikubwa hivyo kinaweza kupambana na uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi wa ndani.

“Tuna uwezo wa kufanya mambo yote kwa pamoja kwa sababu chama kina mifumo mikubwa. Kamati kuu hata isiposema neno, kanda zina,” amesema.

Mbowe pia amezungumzia ukimya wake wakati minyukano ikiendelea miongoni mwa makada, akisema minyukano haikemewi hadharani.

“Ni mara nyingi kunatokea ukosefu wa nidhamu katika chama chetu, viongozi kushutumiana bila sababu, sasa sio kila wakishutumiana viongozi mwenyekiti unatoka hadharani unakemea, ahaa!

“Hatukemei hadharani tunamalizana ndani kwa ndani. Hiki chama ni imara kuliko jana na kitakuwa imara kuliko juzi,” amesema.

“Kuna Watanzania kwa mamilioni ndoto zao za ukombozi wa kweli wa Taifa hili ziko Chadema. Chochote kitakacholeta ufa ndani ya Chadema tutaudhibiti mapema, wala hatutaruhusu ufa wowote utokee kwa sababu ile hiki chama ni kikubwa ni chama cha watu, lazima tukilinde kwa gharma yoyote,” amesisitiza. 

Related Posts