Rais Samia aipongeza Stars kufuzu Afcon, asisitiza haya

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Taifa ya mpira wa miguu, Taifa Stars kwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 huku akisisitiza yawepo maandalizi mazuri.

Rais Samia ameandika hayo leo Jumanne Novemba 19, 2024 katika kurasa zake za mitandao yake ya kijamii muda mchache baada ya Taifa Stars kufuzu michuano hiyo kwa kuichapa Guinea bao 1-0.

“Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025. Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini.

“Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa.”ameandika Rais Samia.

“Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo,”ameongeza Rais Samia.

Related Posts