Leo, vyama vya siasa nchini vinaanza kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuuza sera zao kwa wananchi ili kuwashawishi kuwapa ridhaa wagombea wao ili waongoze vijiji, mitaa na vitongoji kwa miaka mitano ijayo.
Kampeni hizo zitafanyika kwa siku saba tu na Novemba 27, mwaka huu, ndiyo siku ya uchaguzi huo ambayo wananchi wanatarajiwa kufanya uamuzi kwa kuchagua wagombea kutoka kwenye vyama vyenye sera zinazowavutia.
Mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari, jijini Dodoma, Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema nafasi za uenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280 na kwamba, vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea 6,060, sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo.
Alisema nafasi za uenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264, huku vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo.
“Nafasi za uenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 vyama 18 vya siasa vimeweka wagombea 21,636 sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo,” alisema Mchengerwa.
Alisema kwa kuzingatia maeneo ya utawala yaliyotangazwa katika gazeti la Serikali Tangazo Namba 796 na 797 yote ya Septemba 6, 2024, vijiji vilivyopo ni 12,333, mitaa 4,269 na vitongoji 64,274.
Hata hivyo, kutokana na halmashauri za wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo, na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji kutokana na sababu mbalimbali, maeneo yatakayofanya uchaguzi Novemba 27, 2024 ni vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeweka wagombea katika nafasi zote za vijiji, vitongoji na mitaa, huku upinzani ukiweka katika nafasi 30,977, sawa na asilimia 38 ya nafasi zote 80,430 zinazoshindaniwa.
“Hii ina maana wagombea wa CCM takribani asilimia 60 watapigiwa kura za Ndiyo au Hapana kwa mujibu wa sheria za uchuguzi huo.
“Nimeona ni muhimu kuweka idadi hii wazi ili kuupa umma taarifa ya hali halisi ya uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali kwa vyama vyote vya siasa, hata kabla ya malalamiko ya kuenguliwa kinyume cha utaratibu,” alisema Mchengerwa.
Kauli hizo za Waziri Mchengerwa zimefuata baada ya kuwepo malalamiko ya wagombea wa vyama vya upinzani kuhusu kuenguliwa kwenye uchaguzi huo na sarakasi nyingi zilizotokea tangu mchakato huo ulipoanza katika hatua ya uandikishaji wapigakura.
Chama cha ACT Wazalendo, kwa mara ya kwanza kimekuja na ilani yake ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji yenye mambo tisa, yatakayosimamiwa na kutekelezwa na viongozi wao watakaochaguliwa katika uchaguzi utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Miongoni mwa mambo hayo ni kutoa viongozi waaminifu, jasiri na mahiri, kurejesha nguvu za serikali za mitaa kwa wananchi, kuboresha huduma za jamii kwa wote mijini na vijijini na kuwahudumia wananchi kwa kutoa huduma bora na stahiki, kusikiliza changamoto zao kwa ukaribu.
Mengine ni kupambana na ufisadi, kuhudumia watu wote na sio watu wachache na kuhakikisha kila fedha inayokusanywa, inatumika kuondoa umaskini vijijini, kuondoa vitisho, ubabe na uonevu kwa wananchi.
Akiizindua ilani hiyo mwishoni mwa wiki, Kiongozi wa Chama, Dorothy Semu aliwataka Watanzania kutumia kura yao kufanya mabadiliko, akisema ahadi ya chama hicho ni kuwajibika, kutoa huduma bora na kujenga mitaa, vijiji na vitongoji vinavyostawi.
Chadema na ilani za halmashauri
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema hawawezi kuzindua ilani ya kitaifa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, isipokuwa kila halmashauri watakuwa wanazindua kutegemeana na mahitaji yao.
“Hatutaki kurudia makosa yale yale ya miaka yote, uchaguzi huu ni wa mitaa, vitongoji na vijiji, watu katika maeneo yao wana mahitaji yao, unakuta wengine kujenga vyoo, sasa chama hakiwezi kuja na ilani ya kitaifa,” anasema.
Mrema anasema wamejipanga na kila halmashauri itakuja na ilani zao zitakazozinduliwa katika kila kata kwa kuzingatia mahitaji yao.
“Tanzania nchi yetu ni kubwa na tuna jamii nyingi ambazo changamoto hazilingani, kuna wanaofuga, wakulima na wengineo, huwezi kuja na ilani moja ya kitaifa, ni makosa,” anasema.
Katika hatua nyingine, Mrema alipoulizwa namna gani mchakato uliopita ulivyowaathiri, alidai umewaathiri kwa kiwango kikubwa, huku akieleza ukatili waliofanyiwa viongozi wa chama hicho, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
NLD na mahitaji ya wananchi
Akiwa na mtazamo kama huo, Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo anasisitiza kwamba hawawezi kuwafanyia wananchi sanaa za kisiasa ambazo hazina tija.
“Hatutaki na hatuwezi kutengeneza ilani ya kitaifa, mahitaji yanatofauatina, mfano Handeni katika eneo la Kabuku, wana shida kubwa ya maji na wananchi wake ni wakulima wa matunda, changamoto hiyo ni tofauti na maeneo mengine,” anasema.
Doyo anasema kutengeneza ilani moja “uniform” (inayofanana) ni kutowatendea haki wananchi, huku akieleza mpango wao ni kushughulika na shida za raia zaidi.
“Serikali inajinasibu imesambaza umeme vijiji vyote nchini, lakini tumebaini baadhi ya vijiji vimerukwa na wananchi wanalia, kazi yetu ni kuwaeleza uhalisia na kuwaambia wakituchagua tutatatua shida zilizopo,” anasema.
Doyo anasema ilani za kitaifa mara nyingi huwa zinaangalia zaidi mambo mapana kama ya kiusalama, uchumi, huduma za kiafya za wananchi na mambo mengine yanayowagusa watu wa maeneo yote.
Kuhusu kuathiriwa kwa mchakato wa uchaguzi wa serikali za mitaa, Doyo anakanusha, huku akibainisha kwamba maeneo mengi wagombea wao wamepenya na jukumu walilonalo ni kutengeneza mbinu za kuwashawishi wananchi.
“Tuliwekewa mapingamizi sehemu chache na figusu tulifanyiwa na wagombea wenzetu kutoka chama tawala, lakini tulikata rufaa na wagombea wamepitishwa, hivyo hatuna wasiwasi muda uje tu,” anasema.
CUF yajifungia kutafakari
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Magdalena Sakaya anasema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umewaathiri kwa kiwango kikubwa kiasi cha wanachama wao kukosa nguvu ya kuwaunga mkono.
“Tumejifungia tunakusanya takwimu kutoka nchi nzima kisha tutafanya kikao na kutoka na msimamo. Kusema kweli CUF tumechoka, ni kama tulilengwa kwa namna fulani, haiwezekani maeneo ambayo tulitegemea wagombea wetu wote waliokata rufaa hakuna aliyepenya,” anasema.
Katika maelezo yake, Sakaya anasema maeneo waliyokuwa wanayategemea ambayo chama hicho kimekuwa kikiungwa mkono, mathalani mikoa ya Kusini, Kondoa na Chemba, wagombea wao wametupwa nje.
“Tumefanyiwa unyama, tulitegemea kamati za rufaa zingetenda haki labda kutokana na maagizo ya waziri, lakini matokeo yake wajumbe wa kamati hizo wamewakandamiza zaidi,” anasema Sakaya.
Sakaya anasema katika maeneo hayo rufaa nyingi walizowekewa baada ya kufuatilia wamebaini hajulikani aliyewekwa, huku akishuku ni mpango wa chama tawala kuendelea kujitengenezea dira ya kutaka kuwanyima uhuru wa machaguo mengi wananchi.
“Kwa kuwa wamefanya ukatili huo, tunakusanya takwimu kama chama, tutatoka hadharani kueleza msimamo wetu wa jumla. Wanachama wetu wako njiapanda hadi sasa,” anasema
Anasema wameandaa ilani ya uchaguzi huo ambayo haijazinduliwa, ikiathiriwa na wagombea wao kuondolewa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema uchaguzi wa mwaka huu umeshuhudiwa kuwa na hekaheka nyingi kutokana na matukio yaliyojitokeza wakati wa mchakato wake.
Anataja matukio hayo kuwa ni pamoja na kukatwa kwa wagombea, suala zima la kukata rufaa, kurudishwa kwa walioenguliwa huku kubwa zaidi akisema suala la Chama cha Mapinduzi (CCM) kusimamisha wagombea maeneo yote nchi nzima huku upinzani ukisimamisha asilimia 38.
Akizungumzia ilani iliyotangazwa na chama cha ACT Wazalendo, anasema ni jambo la kupongezwa kwa sababu limekuja katikati ya hekaheka zinazoshuhudiwa.
“Suala la ilani unajua vyama vingi huwa vinatoa ile ya miaka mitano, hasa kuelekea katika uchaguzi mkuu, hili walilolifanya ACT Wazalendo ni kama surprise (kushangaza) wanahitaji kupongezwa,” anasema mwanazuoni huyo.
Anasema kwa maoni yake, ACT Wazalendo wana mpango wa kutaka wananchi wajue viongozi wao wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wataenda kufanya nini japokuwa ipo kisheria.
“ACT Wazalendo wamekuja na kitu kipya ambacho ni kizuri, kinachoweza kuleta hoja mezani, kwamba wanaochaguliwa kuwa wenyeviti wanakuja kufanya nini,” anasema Dk Loisulie.
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Lusungu Mubofu anasema mpaka sasa wameona kwa kiasi kikubwa maandalizi ya mikutano kwa ajili ya wagombea kwenye baadhi ya maeneo ni hatua nzuri kwenye demokrasia, lakini hawajaona sana ilani za vyama.
“Nadhani ACT Wazalendo wameonyesha mfano kwa kuzindua ilani, maana ndio msingi wa sera. Itapendeza kama huu utakuwa utaratibu kwenye chaguzi zijazo za serikali za mtaa.
“Jambo lingine la kuangalia ni kuona namna gani tunaweka mazingira mazuri wakati mwingine kwa vijana wengi kushiriki kupiga kura, kwa kushusha umri wa kupiga kura kutoka 18 kushuka hadi 16 na umri wa kugombea kushuka kutoka 21 hadi 18,” anashauri.