Mahakama kutoa uamuzi wa kesi ya mirathi ya Jenerali Kiwelu

 

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam leo Novemba 20 ,2024 inatarajiwa kutoa uamuzi wa maombi ya kuwakataa wasimamizi watatu wa mirathi ya familia ya marehemu Jenerali Tumainieli Kiwelu. Anaripoti Mary Victor, Dar es.Salaam … (emdelea).

Shauri la maombi ya kuwakataa wasimamizi wa mirathi lilifunguliwa mahakamani hapo na kupewa namba 11987 la mwaka 2024.

Wasimamizi hao wa mirathi ya Jenerali Kiwelu ni watoto wake Julius Kiwelu, Robson Kiwelu na Anita Kiwelu ambao kwa zaidi ya miaka mitatu wanadaiwa kushindwa kuzitambua, kuzikusanya na kugawa mirathi hiyo kwa warithi halali.

Waliofungua maombi hayo ni watoto sita wa marehemu Kiwelu wakiwakilishwa na Leslie na Charles Kiwelu baada ya shauri la msingi la mirathi lenye namba 160 la mwaka 2021 lililopo kwenye Mahakama hiyo kushindwa kuendelea kwa muda mrefu kutoka na kuahirishwa mara kwa mara kwa shauri.

Katika shauri la msingi la ugawaji wa mirathi hiyo, wasimamizi hao walipewa miezi sita na Mahakama hiyo kuhakikisha wanazitambua na kuzikusanya mali zote za Jenerali Kiwelu zilizopo ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Mbali na Leslie na wenzake , watoto wengine wanaounga mkono kuondolewa kwa wasimamizi wa awali mirathi ni pamoja na Frank Kiwelu, Joyce Kiwelu na Jenifer Kiwelu.

Akizungumza na Raia Mwema jijini hivi karibuni Leslie alisema ni muda mrefu umepita tangu shauri la msingi la mirathi namba 160 la mwaka 2021 likwame kushughulikiwa mahakamani hapo, hali inayochangia kuanza kuwa na mashaka na usikilizwaji wake.

“Hawa wasimamizi ni watoto wakubwa WA marehemu baba, tunashindwa kuwaelewa kwa maana hakuna kikao cha mirathi tulichowahi kukutana wala kuitwa mahakamani. Mambo yote yamesimama, muda unakwenda ndugu zetu wapo kimya kana kwamba hakuna kinachoendelea, sasa kama wameshindwa ni Bora Mahakama iwaondoe katika kusimamia mirathi na kwamba tuoendekeze watu wengine wa kusimamia”

Naye Charles Kiwelu alisema kwamba baba yao ameacha mashamba, majengo ya biashara na makazi kwenye mikoa tofauti alimokuwa mkuu wa mkoa ikiwemo Mkoa wa Kagera lakini suala la kushangaza baadhi ya majengo yamepangishwa na kaka zao hao pasipo wao kupatiwa gawio lolote.

“Baba amekuwa Mkuu wa Mkoa WA Tabora , Tanga, Rukwa, Shinyanga, Kagera na kwingineko kwa vipindi tofauti wadhifa ambao aliupata baada ya kuwa mtumishi ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) huku akitunukiwa nishani mbalimbali ikiwemo ya Vita ya Kagera na Operesheni Msumbiiji.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu Mmoja wa wasimamizi wa mirathi hiyo Robson Kiwelu alisema kwamba Hana taarifa ya kukataliwa kwake kuwa msimamizi na kwamba ni mara ya pili anasikia kwamba kuna madai hayo.

Naye Julius Kiwelu ambaye pia ni msimamizi aliandika ujumbe wa simu kwamba yupo kikaoni.

About The Author

Related Posts