JKT Tanzania haitaki unyonge kwa Prisons

LICHA ya historia kutofurahisha kwa JKT Tanzania inapocheza dhidi ya Tanzania Prisons, lakini Kocha Ahmad Ally anaamini maandalizi yao wakati ligi imesimama yataleta mabadiliko ya kiufundi katika mchezo huo.

Timu hizo zinatarajiwa kukutana Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar, ambapo JKT wanalenga kuvunja mwendelezo wa matokeo yasiyoridhisha dhidi ya wapinzani wao hao.

Takwimu zinaonyesha kuwa, tangu mwaka 2018, JKT Tanzania imepata ushindi mmoja pekee katika mechi 10 za Ligi Kuu Bara dhidi ya Prisons. Kwa upande mwingine, Prisons imeibuka kidedea mara nne, huku mechi tano zikimalizika kwa sare.

Hata hivyo, katika mechi tatu zilizopita, timu hizo zimetoka sare ya bao 1-1 mfululizo. Hali hii inathibitisha kuwa ushindani baina yao ni wa hali ya juu, na mchezo ujao unatarajiwa kuwa kivutio kingine. Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesisitiza kuwa historia hiyo haiwaogopeshi, badala yake inawachochea kufanya kazi kwa bidii zaidi. 

“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo huu. Tumefanyia kazi udhaifu wetu hasa kwenye kutengeneza nafasi na kumalizia, tunaamini kwamba safari hii tutapata matokeo mazuri,” alisema kocha huyo.

Related Posts