Hatimaye watu wa Zanzibar wameona dalili za Serikali kupania kupambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa kuwabana wanaofanya biashara hiyo ambayo inakisiwa kuathiri miili na akili za watu wapatao 10,000 Visiwani hapa.
Wengi wa waathirika ni wa umri wa kati ya miaka 13 na 35 na wamo wanawake na wazee. Kwa sasa zipo nyumba zipatazo 10 za kuwarekebisha walioathirika na dawa za kulevya (nyumba maalumu za waathirika).
Hatua iliyoifurahisha jamii ni ile iliyotangazwa wiki iliyopita na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (ZDCA) ya kutaifisha mali zenye thamani ya Sh976 milioni za watu wanaosemekana ni washiriki wakubwa wa biashara hii haramu.
Mali hizi ni pamoja na shamba la bangi lililolimwa Paje, Kusini Unguja na raia wa Ujerumani aliyekuja nchini kama mwekezaji, Andreas Wolfgang Fretz. Kwa ujumla, mali zake zilizotaifishwa zina thamani ya Sh519 milioni.
Miongoni mwa wananchi waliotaifishiwa mali zao ni Mohamed Abdulla Juma, mwanasheria aliyewahi kuwa ofisa mwandamizi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa ZDCA, Kanali Burhani Zubeir Nassor, huyu mwanasheria alivunja sheria kwa kufanya utakatishaji wa fedha za watuhumiwa wawili waliosemekana kufanya biashara ya dawa za kulevya, Saleh Khamis Baslem na mkewe, Gawar Bachi Kakir Bahi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kanali Zubeir, huyu mwanasheria aliingiza nchini simu za satelite zilizotumika kuwasiliana na manahodha wa meli kutoka Afghanistan walioingiza dawa za kulevya nchini.
Pamoja na kuipa heko ZDCA kwa kusimamia sheria ya Zanzibar ya kudhibiti dawa za kulevya ambayo inaweka katika adhabu, kutaifisha mali za wanaofanya biashara hii haramu, yapo mambo ambayo yanahitaji kupekuliwa kama ilivyofanyika kwa kuwabana hao watuhumiwa.
Kwanza ni kujiuliza huyu mwekezaji amekuwa na hilo shamba la bangi kwa muda gani na nani walionunua hiyo bangi kutoka kwake.
Je, huyu aliyejidai kuja kuwekeza Zanzibar ili kuchangia maendeleo na badala yake kuchangia kuharibu maisha ya watu, ni mwekezaji pekee anayefanya vitendo vya uhalifu vya aina hii au wapo wengine kama yeye?
Kijiji cha Paje na maeneo ya karibu, kina ofisi ya mwakilishi wa serikali ajulikanaye kama sheha, ambaye pia ana wasaidizi, zaidi ya askari 200 wa Jeshi la Polisi na vikosi vingine vya ulinzi. Wote hawa wamekuwa wapi hata huyu mwekezaji akawa na shamba bila kujulikana?
Vilevile, tumeelezwa kupatikana simu za satelaiti zinazotumika kuwasiliana na meli katika bahari kuu zinazoleta dawa za kulevya. Je, hawapo watu wengine wanaomiliki simu hizi na je, hakuna njia ya kugundua kwa urahisi wanaomiliki simu za aina hii nchini?
Jambo la muhimu zaidi kwa sasa ni kufanya juhudi za kuufumua mtandao mzima wa hawa majahili wanaofanya biashara hii haramu na kuwachukulia hatua kali za kisheria kama zilizochukuliwa kwa huyu Mjerumani na hao wengine.
Lakini mbali ya mali zao kutaifishwa, pia waonje joto la jiwe kwa kufanya kazi ngumu na kwa muda mrefu gerezani kwa vile wanaojihusisha na hii biashara ya dawa za kulevya hawatofautiani na wauaji.
Hawa ni watu walioharibu maisha ya vijana wengi na kuzivuruga familia zao na jamii kwa jumla, mbali ya kuvipa visiwa vya Unguja na Pemba sura mbaya ya kuwa kituo maarufu cha uingizaji wa dawa za kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Vilevile, Serikali ifanye uchunguzi wa kina kujua kazi wanazofanya hawa wawekezaji, hasa kwenye baadhi ya hoteli za kitalii ambazo mwenendo wake umekuwa unatiliwa mashaka na baadhi ya watu.
Jingine muhimu ni kuhakikisha masheha ambao ni tochi ya serikali katika mitaa na vijiji wanakuwa macho kugundua mapema watu ambao nyendo zao zina mashaka na sio kujikita tu kwa masuala ya kisiasa na kuandika barua za watu wanaoomba leseni za biashara, kushajilisha
mapokezi ya mbio za mwenge.
Heko ZDCEA kwa kazi nzuri, lakini inahitaji kuungwa mkono na kila mwananchi ili mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini yafanikiwe na kulinusuru taifa kuwa na kundi kubwa la watu wasiojijua wala kujitambua wanaokuwa mzigo usiobebeka kwa familia
zao, majirani na taifa.