Shungu: Beki mpya Yanga ni mtu na nusu

WAKATI Yanga ikibakiza hatua chache kumalizana na beki wa kushoto wa FC Lupopo, Chadrack Boka, Raul Shungu amewaambia ; “Ni bonge ya beki.”

Kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha Yanga kwa mafanikio miaka ya tisini, ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu kuwa, Boka ni beki wa maana na kama Yanga itamnasa itakuwa imezipiga bao timu nyingi ikiwemo AS Vita, DC Motema Pembe na hata TP Mazembe.

Shungu ambaye kwasasa ni kocha msaidizi pale AS Vita ya Congo alisema, Boka ni beki sahihi kuziba nafasi ya Lomalisa Mutambala; “Sina wasiwasi na Yanga imejijengea jina kubwa sana kwa wachezaji wa Kikongomani wanaona wakienda pale wako salama sana,”alisema Shungu ambaye amewahi kuwa Kocha wa Rwanda na Shelisheli.

“Boka ni beki mzuri sana kama watamalizana naye utakuwa usajili mwingine wa nguvu kwa Yanga hapa kwetu (DR Congo) klabu zote kubwa zilikuwa zinamtamani, lakini shida ya hapa sio rahisi Lupopo kuziuzia timu zingine kubwa mchezaji sisi (Vita club) tulimtaka, Mazembe na hata Motema Pembe lakini hatukufanikiwa,”aliongeza Kocha huyo mwenye mapenzi makubwa na Yanga akilielewa vizuri soka la Afrika.

Alisema Boka ni beki anayejua kukaba na kupandisha mashambulizi akiwa na ujuzi wa kupiga krosi za maana lakini pia anajua kufunga mabao kwa staili ya uchezaji wa Yanga yenye malengo ya kufika mbali Afrika.

“Anajua sana kukaba ni mtulivu anajua kupiga hesabu zake vizuri anapokabiliana na mashambulizi ya timu pinzani, pia anajua sana kupanda mbele na kupiga krosi kama Yanga itakuwa na watu wazuri wa kufunga watafunga sana.

“Unaona ule urefu wake utakuwa msaada sana kwa Yanga kwa kuwa anajua kucheza mipira ya juu ni beki anayependa kupambana muda wote akiwa uwanjani, anataka sana kushinda sio mtu wa kukata tamaa,”alisema

Yanga inamtaka Boka kuja kuziba nafasi ya Lomalisa ambaye ana nafasi kubwa ya kuachwa mwisho wa msimu baada ya mkataba wake kumalizika huku akihusishwa kwa mbaali na Simba ambayo hatahivyo inadaiwa kwamba walikuwa wakiwatingisha Yanga ili wasimteme.

Usajili wa beki huyo mpya unaelezwa uko kwenye hatua za mwisho baada ya Rais wa Yanga injinia Hersi Said kumpandia ndege kukamilisha taratibu za makaratasi baada ya kufanya vikao vingi kwenye mitandao na wamiliki wake Lupopo ambayo miaka ya 2000 wamewahi kuwapa Yanga mastaa watatu, Patrick Katalay, Alou Kiwanuka na Pitchou Kongo.

Hata hivyo Yanga italazimika kuweka mzigo wa fedha mzuri mezani kumchukua beki huyo ambaye amebakiza mwaka mmoja na klabu yake hiyo yenye maskani yake jijini Lubumbashi, DRC.

Yanga imepania kufanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake lengo likiwa ni kufanya vizuri kimataifa msimu ujao.

Ingawa wanafanya kimyakimya lakini Mwanaspoti limeambiwa kwamba wamepania usajili umalizike sambamba na msimu huu ili wanapokwenda mapumziko mafupi kila kitu kiwe kinajulikana. Nini maoni yako;  0658- 376 417

Related Posts