WAZIRI KOMBO AONGOZA MKUTANO WA DHARURA WA UTATU WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC ( SADC ORGAN TROIKA)

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Balozi Mahmoud Thabit Kombo ameongoza Mkutano wa dharura wa Utatu wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi, na Usalama uliofanyika jijini Harare, Zimbabwe tarehe 19 Novemba 2024.

Mawaziri wa Jumuiya ya SADC walijadiliana kwa pamoja na kuipitisha Ajenda ya Kuangazia Hali ya Usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na njia madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo. Ajenda ya Mkutano huo itaenda kujadiliwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali ili kutolea mwongozo na maamuzi.

Wajumbe wa Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt Stergomena Tax, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.Samwel Shelukindo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe.

Mhe. Dkt Tax nae alipata nafasi ya kuchangia mada, na alisisitiza nia ya Tanzania kuunga mkono juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Aidha, Dkt Tax amezisihi nchi wanachama umuhimu wa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Wakuu wa Nchi ili kufikia malengo ya kuleta Amani na Usalama katika Kanda.

Waziri Kombo amebainisha kua Tanzania itaendelea kusimama bega kwa bega kushirikiana na Nchi wanachama ili ajenda ya kurudisha Amani na Usalama DRC iweze kufikiwa.

” Mshikamano wetu ndio nguzo yetu itakayosaidia kuleta suluhu ya kudumu na kurejesha Amani na Usalama kwa ndugu zetu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo “.

Related Posts