Kilombero. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amezindua utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ya wilaya hiyo kupitia mapato ya ndani kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Katika mwaka wa fedha 2024/2025, Halmashauri ya Mji wa Ifakara imetenga Sh817.6 milioni kwa ajili ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizindua utaoaji wa mikopo hiyo leo Jumatano Novemba 20, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya amevitaka vikundi vitakavyonufaika kuhakikisha mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati.
“Navipongeza vikundi vyote, lakini fedha hizi zitumike kwa malengo mliyojiwekea badala ya kuzitumia kwa anasa na shughuli zisizokusudiwa,” amesema Kyobya.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Witness Kimoleta amewahimiza waombaji na wanufaika wa mikopo hiyo kufuata kanuni, utaratibu na sheria zilizowekwa ili mikopo hiyo iweze kuleta matokeo chanya katika shughuli zao za kiuchumi.
Pia amesisitiza kuwa mpango wa utoaji wa mikopo hiyo ni sehemu ya azma ya Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya kuinua hali za kiuchumi za makundi maalumu na kusaidia kupunguza umasikini nchini.
“Tumewaandaa maofisa wa mikopo wanaoendelea kutoa elimu kwa vikundi na kuwafuatilia mara kwa mara kuhakikisha shughuli zao zinaleta matokeo mazuri na kurahisisha urejeshaji wa mikopo hiyo,” amesema Kimoleta.
Kwa mujibu wa Kimoleta, katika awamu ya kwanza, Sh261 milioni zitatolewa kwa vikundi vilivyokidhi vigezo kutoka kata 15 kati ya 19 zilizoandikishwa.
Amesema halmashauri hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi kuhakikisha mikopo hiyo inaleta mabadiliko chanya katika maisha yao.
Hilda Imani, mmoja wa wanakikundi kutoka Kata ya Katindiuka, ameishukuru Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa elimu waliyopatiwa kuhusu kujiunga kwenye vikundi ili kupata mikopo hiyo na matumizi bora ya mikopo.
“Nawasihi wanakikundi wenzangu tutambue kuwa hela hizo ni mkopo, lazima tufanya marejesho kwa wakati. Kama tutatumia vizuri, mikopo hii inaweza kubadilisha maisha yetu kwa heshima na staha, tofauti na mikopo mingine ambayo mara nyingi hutufanya tudhalilike,” amesema Imani.