Simulizi ya kijana mwenye ulemavu anayepambana na maisha kupitia Sanaa

Handeni. Ulemavu haujamzuia kijana huyu kuzifikia ndoto zake. Kwake, umeibua fursa mpya za kumwezesha kuendesha maisha yake bila kumtegemea mtu, tofauti na baadhi ya wengine wenye changamoto kama zake wanaoomba msaada barabarani.

Athuman Mhina (24), mkazi wa Handeni, mkoani Tanga, amejijengea umaarufu kupitia kipaji chake cha sanaa, hasa kucheza, ambapo amekuwa kivutio kwenye shughuli mbalimbali za burudani na hata za kiserikali.

Umahiri wake wa kucheza, licha ya kuwa na ulemavu wa mguu mmoja, umewavutia wengi.

Kijana huyu anayejulikana pia kwa jina la “Dogo Chiba”, ni mpenzi wa siasa na hata aligombea udiwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020 akiwa na miaka 18 tu, ingawa hakufanikiwa kushinda kwenye kura za maoni.

Katika mahojiano na Mwananchi, Mhina ameielezea safari yake ya maisha tangu akiwa mzima hadi kuwa na ulemavu, baada ya kung’atwa na nyoka na kulazimika kukatwa mguu mmoja.

“Ulemavu huu niliupata nikiwa darasa la tatu, niling’atwa na nyoka kwenye mguu wa kulia wakati nakwenda shamba. Nilipopelekwa hospitali, madaktari walishauri mguu wangu ukatwe baada ya kuona umeharibika. Hivyo, wazazi wangu na mimi tukakubali. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa safari yangu ya kuwa na ulemavu,” anasema Mhina.

Amesema maisha yake hayakusimama pale, badala yake tukio hilo lilimpa nguvu ya kupambana na kufanya sanaa kuwa msingi wa maisha yake.

“Nimekuwa nikishiriki matamasha na shughuli za kijamii, nikiimba na kucheza kwa lengo la kujipatia kipato. Mara nyingi huwa naalikwa, lakini wakati mwingine najitokeza mwenyewe,” anaeleza.

Kipaji chake kimewavutia wananchi na viongozi wilayani Handeni, wakiona mfano bora wa mtu anayepambana kutafuta maisha badala ya kuomba msaada.

Msanii chipukizi, Athumani Mhina maarufu kama Dogo Chiba akitunzwa katika moja ya shughuli zake za kutoa burudani katika tamasha. Picha na Rajabu Athumani

Mhina anaeleza kuwa alipenda muziki tangu akiwa darasa la tatu, akiwa shabiki wa msanii Diamond Platinum.

“Nina uwezo wa kucheza na kuimba nyimbo zake hata kwa saa moja nikiwa jukwaani. Pia, naweza kutunga nyimbo, kuimba, na kupiga gitaa,” anasema.

Baada ya kung’atwa na nyoka, uwezo wa familia yake kifedha uliyumba, hivyo alilazimika kusitisha masomo yake baada ya darasa la saba. Hata hivyo, alipata ufadhili wa wadau na kumaliza kidato cha nne.

Mhina amesema alijaribu kujiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ili kujifunza zaidi, lakini akakwamishwa na ukosefu wa fedha. Anatoa wito kwa wadau wamsaidie kufanikisha ndoto zake za kuwa msanii mkubwa.

Baba yake, Mzee Mhina Athumani, anakumbuka tukio lililotokea alfajiri wakati Mhina akiwa njiani kwenda shambani. Alipata taarifa kutoka kwa majirani, akampeleka hospitali ya Tumbi ambapo madaktari walipendekeza kukatwa mguu wake.

“Hajawahi kukata tamaa, ameendelea kupambana kwa kipaji chake cha sanaa. Anahitaji msaada wa kufanikisha ndoto zake,” amesema mzee Mhina.

Mbunge wa Handeni Vijijini, John Sallu, amesifu juhudi za Mhina akisema: “Ni vijana wachache waliokumbwa na changamoto kama zake wanaojituma kutafuta riziki. Alishawahi kugombea udiwani akiwa na hali hiyohiyo ya ulemavu. Ni wa mfano kwa jamii.”

Sallu amesema wanatafuta njia za kumsaidia kijana huyo kwa kumpatia mkopo wa halmashauri na usajili rasmi ili kumwezesha kujikimu zaidi kupitia sanaa.

Related Posts