Unguja. Licha ya sekta ya kilimo kuwa tegemeo kwa uchumi wa Zanzibar na maisha ya wananchi, ushiriki wa wanawake bado ni mdogo kutokana na changamoto za kijamii, upatikanaji wa ardhi na rasilimali fedha.
Hata hivyo, wanawake wameanza kujikita katika kilimo mseto, mbinu endelevu inayosaidia kuongeza kipato, kulinda mazingira, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Sekta ya kilimo inatajwa kuajiri takribani asilimia 35 ya wananchi wa Zanzibar, huku zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wakitegemea sekta hiyo kujikimu kimaisha.
Sekta hiyo inayojumuisha mazao, mifugo na maliasili za misitu ni tegemeo kwa uchumi wa Zanzibar na inachangia moja kwa moja kwa wananchi kujikimu kimaisha, kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, umwagiliaji, Maliasili na Mifugo.
Pamoja na hali hiyo, wanawake wako nyuma kutokana na mitazamo ya jamii na kukosa ardhi, ingawa, kwa sasa baadhi yao wameanza kupata mwamko na kujikita katika kilimo mseto kinachotumia eneo dogo la ardhi, kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kilimo mseto huchanganya mazao na miti katika eneo moja ili kuleta faida za kijamii, kiuchumi na kimazingira. Aina hii ya kilimo inatoa majawabu ya moja kwa moja ya tatizo la upungufu wa ardhi na nishati ya kupikia.
Kilimo hiki husaidia pia upatikanaji wa chakula, kufyonza hewa ukaa, kuboresha mzunguko wa virutubisho na kuhifadhi unyevu kwenye udongo, kupunguza kasi ya upepo na kuongeza kipato kwa mkulima kutokana na mazao ya kilimo na misitu endapo atafuga nyuki katika eneo husika.
Mtaalamu wa kilimo, Hussein Ali Ame anasema kilimo hicho hupunguza gharama ya uwekezaji, ni matumizi bora ya ardhi na kuongeza lishe kwenye familia.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wanawake wakulima katika Shehia za Uzi na Ng’ambwa, Mkoa wa Kusini Unguja, wanaeleza fursa na changamoto zinazowakabili.
Aisha Abdalla Ahmed, mkulima katika shehia ya Uzi anasema wamehamasika kujikita katika kilimo mseto ambacho kina manufaa makubwa kwa chakula na kiuchumi, kikilinda ardhi na kutunza mazingira.
“Tuna matumaini makubwa ya kupata mavuno tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma,” anasema.
Amina Rashid, mkulima katika Shehia ya Ng’ambwa anasema wazee wao walikuwa wakilima lakini wao hawakujishughulisha na kilimo.
Anasema walishindwa kulima kwa sababu ya kukosa ardhi na mitazamo ya jamii kwamba mwanamke anastahili kufanya kazi za nyumbani na si shughuli au kazi zenye mrengo wa biashara.
“Elimu naona imeanza kuingia, kwa sasa tumepata mwamko. Tunalima kilimo mseto chenye mazao mengi ya biashara na chakula kwa wakati mmoja, kwa hiyo inasaidia ukikosa hiki utapata kile,” anasema.
Kwa upande wake Najjat Msimu Hassan anasema licha ya jitihada zinazofanyika, hawawezi kufikia malengo pasipo kushikwa mkono na wanaume.
Pia anasema wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbegu, huku zingine zikiharibika kama vile miparachichi kutokana na mazingira na ardhi ya eneo hilo.
Mtoro Simai Vuai, mkulima katika Shehia ya Ng’ambwa anasema kilimo kinawasaidia kuondokana na utegemezi kwa wanaume.
Anasema mafunzo yamewawezesha kulima kwa tija.
“Katika kilimo hiki tunachanganya, kuna kilimo cha muda mrefu na muda mfupi, humo tunapata chakula, tunaweza kupata fedha za matibabu na kujiinua kiuchumi,” anasema.
Mtoro anasema changamoto kubwa ni uhaba wa maji, akisema kunahitajika visima kwa ajili ya umwagiliaji.
“Kama tukipata visima bila shaka tutazidi kuneemeka, maana changamoto kubwa ni maji yaliyopo mbali,” anasema.
Baadhi ya wanaume waliozungumza na Mwananchi akiwemo Malik Mbaraka Makame, mkazi wa Shehia ya Ng’ambwa, wamesema kuna mwamko kwa wanawake kushiriki shughuli za kilimo.
“Juhudi za wanawake tunaziona lakini wanatakiwa kushirikiana na wanaume maana wakiachwa peke yao inawezekana wakafika sehemu wakakwama kwa sababu mahitaji ni makubwa na kuna baadhi ya kazi ni ngumu,” anasema.
Hata Ahmed Ali Mussa ana mtazamo kama wa Makame kuwa wanaume wanapaswa kuwasaidia wanawake wanapokwenda shambani, ingawa wakati mwingine wanabanwa na majukumu mengine ya kutafuta riziki.
Sheikha wa Shehia ya Uzi, Othman Mwinyi Haji anasema kuna changamoto ya maji ya chumvi kutoka baharini kuingia kwenye mazao kutokana na mikoko kukatwa.
Anasema kipindi cha nyuma maji yalikuwa yakipanda angalau mara moja kwa mwaka lakini kwa sasa yanaingia kila siku kutokana na uharibifu wa mazingira.
Anasema wananchi katika shehia hiyo, hususani wanawake wamepata mwamko na kujikita katika kilimo mchanganyiko.
“Zamani ulikuwa ukilima kwenye mwitu unakuta mbolea yenyewe na mihogo ilikuwa mizuri, lakini ukirejea mara ya pili nguvu zinapungua kwa hiyo kwa sasa kutumia mbolea ni muhimu,” anasema.
Amesema Serikali haijapeleka miundombinu yaumwagiliaji lakini wao hutumia visima vilivyochimbwa na wananchi, baadhi vikiwa na maji yenye chumvi.
Ofisa wa teknolojia ya uzalishaji katika mradi wa Zanzibar Women Leadership in Adaptation (ZanzAdapt), Shaaban Peter amesema kupitia mradi huo wanalenga kuwafikia wakulima 4,000 kati yao asilimia 80 ni wanawake.
Mradi huo unatakelezwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Kimataifa la Misitu (CFI), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa –Zanzibar), na Jumuiya ya Misitu Pemba (CFP) kupitia ufadhili wa Global Affairs, Canada.
“Tunalenga wanawake kwa sababu wengi ndio waathirika wa mabadiliko ya tabianchi, wakitambua namna ya kukabiliana nayo na wakiwa na vipato vyao, itawasaidia kukuza uchumi na kuhifadhi mazingira,” anasema.
Anasema katika kilimo ni lazima wapate miche bora na huwafundisha wakulima mbinu bora za kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa, kuhifadhi udongo na kuhifadhi unyevunyevu.
Shaaban anasema wametoa miche ya migomba, nanasi, ndimu na parachichi kwa zaidi ya wakulima 300.
Katika Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ya mwaka 2024/25 licha ya kutaja jitihada mbalimbali za kuinua kilimo kisiwani humo, jitihada kubwa zimejikita katika umwagiliaji katika uzalishaji mpunga.
Bajeti hiyo inalenga kufikia hekta 1,928 za umwagiliaji tofauti na miundombinu ya zamani.
Waziri mwenye dhamana, Shamata Khamis Shaame alisema lengo kuu la wizara ni kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbinu bora na teknolojia za kisasa, upatikanaji wa masoko na hatimaye kukuza pato la Taifa sambamba na uhifadhi wa maliasili.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Khamis Ali Juma amesema upo mpango mkakati unaojumuisha kilimo kwa ujumla Zanzibar ambao wanaamini kukamilika kwake kutaleta tija katika kilimo kwa ujumla.