Dar es Salaam. Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, Kombo Mbwana aliyekuwa mahabusu kwa zaidi ya miezi minne baada ya Mahakama ya Wilaya ya Tanga kumnyima dhamana, amerejea uraiani kwa kulipa faini ya Sh85,000.
Kombo ambaye ni Ofisa Habari wa Chadema Mkoa wa Tanga alikuwa anakabiliwa na kesi ya jinai, katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo alikuwa anakabiliwa na mashtaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
Katika shtaka la kwanza alikuwa anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.
Anadaiwa Julai 9, 2024 katika Mtaa wa Hassan Ngwilizi mkoani Tanga, alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.
Pia, alikuwa anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, na kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.
Ingawa mashtaka yake yanadhaminika, Mahakama ya Wilaya Septemba 5 mwaka huu ilifunga dhamana yake, uamuzi uliotolewa na Hakimu Mfawidhi Moses Maroa.
Hakimu Maroa alitoa uamuzi huo baada ya kukubaliana na maombi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa (RCO) wa Tanga, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Manyama Wambura.
Wambura aliwasilisha kiapo mahakamani hapo Julai 30, 2024 cha kuzuia dhamana yake, akieleza kuwa bado upelelezi unaendelea na kuna washtakiwa wengine hawajakamatwa, hivyo anaweza kukwamisha upelelezi huo.
Kombo kupitia mawakili wake Michael Lugina, Rachel Sadick na Deogratius Mahinyila alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa Mahakama ya Wilaya kufunga dhamana yake.
Hata hivyo, mmoja wa mawakili wake, Rachael Sadick amelieleza Mwananchi kuwa Novemba 11, 2024, tarehe ambayo rufaa hiyo ilitajwa mbele ya Jaji Messe Chaba, Kombo aliomba kuiondoa mahakamani na Mahakama hiyo ikaiondoa.
Wakili Sadick amesema kesi yake ya msingi imetajwa leo Jumatano Novemba 20, 2024, lakini upande wa mashtaka umemfutia mashtaka mengine na kubakiwa na shtaka moja la kutumia kadi ya simu ambayo haijasajiliwa.
Hivyo Wakili Sadick amesema leo ametiwa hatiani kwa kosa hilo na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh85,000 au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela.
“Lakini amefanikiwa kulipa hiyo faini na kuachiliwa huru,” amesema Wakili Sadick na kuongeza kuwa, kulikuwa na mazingira yaliyosababisha hayo yote ambayo amesema atayaelezea baadaye akishatulia.
Kabla ya kufunguliwa kesi hiyo, Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.
Julai 14, 2024, siku 29 baadaye Jeshi la Polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard lilitangaza kuwa linamshikilia kwa tuhuma hizo, kisha Julai 16, 2024 akapandiahwa kizimbani.