Simba yamvutia waya Ibenge, bosi wa Nabi nae yumo

JINA la kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge (62) linatajwa kupewa kipaumbele cha kwanza na mabosi wa Simba kumrithi Abdelhak Benchikha aliyeondoka mwishoni mwa mwezi uliopita lakini wakati wakiendelea kujifikiria zaidi, bosi wa zamani wa Kocha Nasreddine Nabi naye amewasilisha maombi mezani akiomba kupewa kibarua cha kuinoa timu hiyo.

Uongozi wa Simba ulikuwa na hamu ya kufanya kazi na Ibenge tangu alipokuwa akiinoa AS Vita lakini hilo lilishindikana baada ya kocha huyo kupata ofa nono RS Berkane na baadaye Al Hilal ya Sudan lakini inaamini sasa ni wakati sahihi wa kutimiza ndoto waliyokuwa nayo kwa muda mrefu.

Kwanini? Sababu mbili zinaonekana kuupa uhakika uongozi wa Simba wa kumpata Ibenge hivi na ya kwanza ni taarifa za kocha huyo kuomba kuondoka Al Hilal ili apate timu ambayo itamfanya awe bize kutokana na ligi ya Sudan kutochezwa kwa muda mrefu kwa sababu ya vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo.

Ibenge inaripotiwa hafurahishwi na kitendo cha kukaa muda mrefu bila kufundisha licha ya juhudi za uongozi wa timu hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu Sudan kuomba Al Hilal ije kushiriki katika Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuwezesha wachezaji wake kupata ufiti wa mechi jambo ambalo halijawa na uhakika.

Lakini jambo la pili linalowapa matumaini Simba ya kumnyakua Ibenge ni mahusiano mazuri ambayo amekuwa nayo kwa muda mrefu na klabu hiyo hasa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Uzoefu mkubwa ambao Ibenge amekuwa nao kwa soka la Afrika na nguvu kubwa ya ushawishi kwa wachezaji wengi, vinaufanya uongozi wa Simba kumuweka kocha huyo kama kipaumbele chao cha kwanza katika mchakato wa kumsaka kocha mpya ukiamini kwamba atajenga timu imara ambayo itairudisha kwenye mstari siku za usoni.

Ibenge ambaye ana leseni ya daraja la kwanza ya ukocha ya Umoja wa vyama vya Soka Ulaya (Uefa) ijulikanayo kama Uefa Pro Licence huku akiwa muumini wa kutumia mfumo wa 4-2-3-1, aliwahi kuiongoza timu ya taifa ya DR Congo kutwaa ubingwa wa Chan mwaka 2016 na mwaka 2015 aliiongoza kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Chan).

Akiwa na AS Vita, kocha huyo aliiongoza kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2014 na mwaka 2018 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, pia aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya DR Congo mara tatu tofauti.

Ibenge akiwa Berkane alitwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021/2022 na msimu mmoja nyuma aliiwezesha kutwa taji la Throne na akiwa Al Hilal ametwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara moja.

Mbali na Ibenge, Mwanaspoti linajua aliyewahi kuwa mkurugenzi wa ufundi wa FAR Rabat inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi, Mfaransa Fernando Da Cruz (51) ametuma wasifu Simba kuomba kazi. Da Cruz aliwahi kuwa kocha mkuu na pia mkurugenzi wa ufundi wa FAR Rabat, aliachana na timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022/2023 akiwa ameiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo ‘Botola’. Kocha huyo amewahi kuzinoa Mouscron ya Ubelgiji na timu ya vijana ya Lille na pia amewahi kuwa mkuu wa idara ya uskauti ya Lile.

Simba pia inao mezani  Julien Chevalier wa Asec Mimosas, Maxime Gouaméné wa FC San Pedro na kocha wa zamani wa Angola na  Sr Vasiljevi.

Related Posts