Dar es Salaam. Mshtakiwa Hamis Luwongo, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe na kuuteketeza mwili wake kwa magunia mawili ya mkaa, amekana mashtaka akidai mwenza wake alitoroka na mpaka sasa hakuna uthibitisho wa kifo chake.
Ameiomba Mahakama imwachie huru aendelee kumtafuta.
Ameibua utata wa mifupa aliyowaonyesha wapelelezi kwamba ni masalia ya mwili wa mkewe aliouchoma moto, akidai aliwadanganya kwa kuwa ilikuwa ya mtu mwingine na mingine ya mzoga.
Luwongo ambaye pia anaitwa Meshack, ameeleza hayo Novemba 19, 2024 alipotoa utetezi Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, baada ya Jamhuri kufunga ushahidi na Mahakama kutamka ana kesi ya kujibu.
Katika kesi ya jinai namba 44/2023, mshtakiwa mkazi wa Gezaulole wilayani Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa kumuua mkewe, Naomi Marijani, kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.
Anadaiwa kumuua Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma moto mwili wake ndani ya banda la kuku, majivu na masalia ya mwili akayazika shambani kwake Mkuranga na kupanda mgomba juu yake.
Kesi hiyo inasikikizwa na Jaji Hamidu Mwanga. Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo kadhaa, yakiwamo maelezo ya onyo na ya ungamo ya mshtakiwa, akidaiwa alikiri kutenda kosa hilo.
Mashahidi hao wakiwamo maofisa wa polisi na wapelelezi, viongozi wa serikali ya mtaa na wananchi wa kawaida, pamoja na mambo mengine walidai mshtakiwa baada ya kukiri aliwaongoza na kuwaonyesha mahali alikomuua mkewe chumbani, bandani alikouchoma mwili na shambani alikozika majivu na masalia.
Katika maeneo hayo, wapelelezi walichukua vielelezo na sampuli yakiwamo matone ya damu, mavazi ya marehemu, chanuo, mswaki, nyembe na mashine za kunyolea, majivu na udongo uliokuwa na mafuta yaliyodhaniwa ya mwili wa binadamu, mifupa na meno.
Vielelezo na sampuli hizo ikiwemo mpanguso wa mate (katika kuta za mashavu kinywani) ya mshtakiwa Luwongo na mtoto vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi wa mpangilio na uhusiano wa vinasaba.
Matokeo ya uchunguzi yalionyesha kulikuwa na matone ya damu ya mtu wa jinsia ya kike na nyingine ya mtu wa jinsia ya kiume, lakini vingine havikuweza kutoa matokeo ya uhusiano.
Luwongo, akiongozwa na wakili wake, Hilda Mushi kutoa utetezi alikiri kuwaeleza polisi kuwa amemuua mkewe na kuwaongoza maeno ya matukio, chumbani kwa mkewe alikodai amemuua, bandani alikoeleza alichoma mwili wa marehemu.
Pia alikiri aliwapeleka shambani kwake katika Kijiji cha Marogoro, wilayani Mkuranga mkoani Pwani alikowaonyesha sehemu alikozika majivu na masalia ya mwili wa marehemu, ambapo askari walichimba na kupata baadhi ya mifupa hiyo.
Katika utetezi huo amedai hajamuua mkewe anayempenda sana, bali anashangazwa na kitendo cha upande wa mashtaka kumtaja mara kwa mara mahakamani kuwa marehemu na yeye kushtakiwa kwa kumuua, wakati hakuna uthibitisho wa kifo chake.
Anadai mkewe alitoweka baada ya ugomvi wa kimapenzi uliosababisha amkamate na kumvuta sehemu za siri mpaka akapoteza fahamu na aliporejewa na fahamu hakumkuta mkewe.
Mshtakiwa amedai maelezo aliyowapa polisi hayakuwa ya kweli, bali ni stori aliyoitengeneza kujiepusha na mateso ya kipigo kutoka kwa polisi katika Kituo cha Polisi Chang’ombe na Kituo Kikuu cha Polisi, wakimtaka akawaonyeshe maiti ya mkewe.
Mshtakiwa amedai masalia ya mifupa aliyowaonyesha polisi shambani kwake si ya mkewe, bali ya mzoga alioukuta wakati akisafisa shamba lake na mingine ilisalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba lake lingine, huko Mwongozo Kigamboni.
Luwongo alidai mifupa iliyofukuliwa na mafundi waliochimba udongo kutengeneza msingi wa nyumba aliyokuwa akijenga, aliichukua na kwenda nayo shambani akaiweka pamoja na ile ya mzoga akaichoma pamoja na takataka nyingine.
Anadai ndiyo maana hata uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na mkemia, matokeo yake hayakutoa uthibisho kuwa ni ya mkewe Naomi.
Tofauti na washtakiwa wengine ambao huongozwa na mawakili kwa maswali moja baada ya jingine, yeye alitawala eneo hilo kwa kutoa maelezo muda mrefu, huku wakili akimuuliza maswali ya mwongozo mara moja moja.
Kabla ya kujitetea, Luwongo alitoa kiapo ambacho kiliifanya Mahakama iingilie kati.
Luwongo baada ya kupanda kizimba cha shahidi na kujitambulisha jina na dini yake kuwa Mkristo, alikabidhiwa na karani wa Mahakama Biblia akainyanyua juu kwa mkono wa kulia na kuanza kuapa:
“Mimi Hamis Said Luwongo, mume halali wa Naomi Orest Marijani, ni…
Kiapo hicho kilimfanya Jaji Mwanga aingilie kati, akamwelekeza karani amuongoze.
“Aah! hapana, karani muongoze,” alisema Jaji Mwanga kisha karani akamuongoza kuapa.
Kwa kawaida shahidi huapa kwa kutamka:
“Mimi (anataja jina lake kamili), ninaapa kwamba ushahidi nitakaoutoa mbele ya Mahakama hii ni wa kweli, kweli mtupu, Ee, Mungu nisaidie.”
Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo ameeleza ni mfanyabiashara mkazi wa Kigamboni Gezaulole. Naomi Orest Marijani ni mke wake halali wa ndoa waliyoifunga katika Kanisa la TAG Upanga.
Amesema katika ndoa yao walipata watoto lakini aliye hai ni mmoja, Gracious Hamisi Luwongo.
Ameeleza kuwa ndoa yao ilikuwa na ugomvi uliosababisha waishi maisha ya ajabu kila mmoja kwa namna alivyotaka, wakiwa wametengana vyumba, yeye akilala cha juu ghorofani na mkewe chumba kikuu (master bedroom) kilicho chini.
Alieleza kila mmoja alitoka hata kulala nje, akidai hakumfuatilia mkewe akilala nje lakini yeye akifanya hivyo mkewe alikuwa akifanya vurumai.
Amedai viongozi wa familia zote mbili walikuwa wanajua namna wanavyoishi.
Siku ya tukio, Mei 15, 2019 asubuhi anadai mkewe alitoweka, ndoa yao ikavunjika na kusabisha mtoto wao Gracious kuishi bila kumuona mama yake.
Anadai siku hiyo hakuwa amelala nyumbani bali kwa mwanamke mwingine na aliporejea alipita chumbani kwa mkewe akamkuta anamuandaa mtoto kwenda shule naye akapanda juu chumbani kwake.
Aliposhuka anadai mkewe alianza vurumai akimtaka arudi kwa wanawake wake, huku akiwa na hasira.
Anadai alimkamata ili kumtuliza lakini mkewe alimkamata na kumvuta sehemu za siri, akaona giza na hakujua kilichoendelea.
Alipokaa sawa anadai hakumuona mkewe na mpaka jioni hakurudi. Kesho yake Mei 16 hakurudi, hivyo aliwasiliana na viongozi wa familia wa pande zote mbili kujua kama atakuwa yuko huko, lakini kote walisema hawajamuona.
Anadai alikwenda kutoa taarifa kituo kidogo cha polisi baadaye mkuu wa kituo alimweleza aende kituo kikuu cha Kigamboni ambako alikwenda akatoa taarifa.
Juni 11, 2019 wakiendelea kumtafuta mkewe na askari wa Kigamboni, anadai akiwa njiani kuelekea kwa kiongozi wa familia, mtoto wa dada yake alimpigia simu kuwa nyumbani kulikuwa na askari na ndugu wa mkewe.
Anadai alipompigia tena simu hakuongea, hivyo alimpigia simu mpelelezi akihoji ametoka kwake lakini ametumaje askari, lakini alijibiwa kuwa hajawatuma.
Anadai alienda kituoni akamwomba mpelelezi waende pamoja nyumbani kwake, hivyo walienda akiwa na askari wanne.
Anadai nyumbani aliwakuta wakwe zake na askari ambao hakuwafahamu (kutoka Temeke).
Anaeleza askari wa Kigamboni waliwauliza vipi mbona wamewavamia eneo lao bila taarifa, maana askari akitoa sehemu moja kwenda nyingine lazima utaratibu unatakiwa ufuatwe.
Anadai swali halikujibiwa bali waliitana wakazungumza pembeni wakaelewana, hivyo askari wa Kigamboni walimtuliza asiwe na wasiwasi aache wafanye uchunguzi.
Anadai askari hao asiowafahamu walimtaka awaonyeshe maiti ya mkewe na kwamba, ujumbe wa simu alikuwa amejitumia mwenyewe.
(Ujumbe huo ulitumwa kutoka namba ya Naomi kwenda kwenye simu ya mshtakiwa akimuaga anaondoka kwenda nje ya nchi na kwamba, Luwongo abaki na umalaya wake)
Anadai aliwaeleza askari hao kuwa amefungua taarifa Kituo cha Polisi Kigamboni na uchunguzi unaendelea, kwa hiyo habari wanazomwambia hazielewi.
Anadai askari walianza kufukuafukua kutafuta maiti ya mkewe, wakaita na watu wengine, hivyo walimtia hasara.
Mshtakiwa alidai alichukuliwa akapelekwa Kituo cha Polisi Chang’ombe ambako aliteswa na askari wakiongozwa na Inspekta Katabazi na askari wengine wakimtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.
Julai 15, 2019 anadai alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi mbele ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) Camillius Wambura wakati huo (sasa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi -IGP) ambako aliwakuta maofisa wengi wakubwa wa polisi.
Anadai Wambura alimuuliza ilipo maiti ya mkewe na kwamba sms amejitumia kulidanganya Jeshi la Polisi.
Anadai alielezwa na Wambura kuwa wao kama Jeshi la Polisi watamwelekeza mahali maiti ya mkewe iliko.
“Mheshimiwa sijui nirudie tena,” shahidi huyo alimuuliza Jaji Mwanga kuhusu kile alichoelezwa na ZCO, kisha aliendelea na ushahidi.
Amedai alivuliwa nguo zote akabaki uchi, akafungwa kamba, akaning’inizwa kwenye mabomba kichwa chini miguu juu na mwingine akawa anampiga kwenye unyayo.
Baada ya mateso kuzidi anadai aliomba wamuache apumzike atawaambia ukweli. Hivyo walimwachia wakampeleka mahabusu.
“Niliwaza hawa watu wanataka maiti na nitawaonyesha maiti gani ili niepukane na mateso haya. Niliwaza usiku ule kuwa niwapeleke sehemu yoyote yenye makaburi,” alidai na kueleza ana shamba Kijiji cha Marogoro, wilayani Mkuranga ambalo alilinunua kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha kisiasa.
Anadai kuna sehemu alimpa kijana kazi ya kufyeka kwani alitaka kujenga nyumba ya wafanyakazi na aliyefyeka akachimba mashimo matano kwa ajili ya kupanda migomba ya kisasa na shimo kwa ajili ya choo.
Anadai majani ambayo yalifyekwa siku walipokwenda kuyazoa wakakuta mifupa ya mzoga wa mnyama aliyekuwa amekufa.
Ameeleza kuna shamba lingine alilonunua Mwongozo, Kigamboni kulikuwa na kaburi lakini wakakubaliana na wenye eneo hilo wakalihamisha na yeye akaanza ujenzi ili ahamie na familia yake.
Vijana waliokuwa wanachimba udongo kwa ajili ya msingi, wakaanza kutoa mifupa, ambayo walihamisha lile kaburi hawakutekeleza kazi yao vizuri na kwamba hiyo mifupa itakuwa ni ya yule marehemu waliyemhamisha.
Anadai siku hiyo alikuwa na safari ya kwenda Marogoro hivyo aliichukua mifupa hiyo akaipeleka huko akairundika kwenye rundo la uchafu, akawaambia vijana wachome moto.
Alieleza kwa kuwa majivu ni mbolea akayachukua akapandia migomba.
Hivyo kutokana na mateso aliyopata ndipo akaona awapeleke katika mabaki ya mifupa aliyoikuta shambani na aliyoitoa kwenye kiwanja, Mwongozo na kutunga uwongo kuhusu maiti ya mkewe na kuwaongoza polisi nyumbani na maeneo mengine.
Amesisitiza maelezo aliyotoa si ya kweli, bali alitaka tu ajiokoe na mateso na kwamba, tangu mwanzo aliwaeleza mawakili wake wayapinge yasipokewe mahakamani kama kielelezo cha upande wa mashtaka.
“Hawa mawakili wao wanataka tu nihukumiwe kunyongwa. Lakini Mheshimiwa mfano leo mimi nihukumiwe kunyongwa halafu baadaye mke wangu anatokea sijui upande wa Jamhuri watakuwaje,” alisema.
“Lakini hayo yote ni stori ya kutunga na ni feki kabisa. Kila siku unawasikia hapa upande wa mashtaka kuwa marehemu Naomi, ukiwauliza wana uthibitisho gani kuwa Naomi alifariki hawana. Kwa hiyo Mheshimiwa upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza majukumu yao,” alidai.
Luwongo alidai anashangaa hata upande wa mkewe wanaaminishwa bila uthibitisho, maana hata udongo uliotolewa mahakamani (kielelezo kinachodaiwa kilikuwa na mchanganyiko wa mafuta ya binadamu) hauna chochote.
“Mheshimiwa kwa ukweli kabisa haya hayahusiani na mke wangu. Mkemia ripoti yake yote hakuna mahali ambako amesema hivyo,” alidai.
“Suala la msingi hapa ni je yale masalia waliyoyatoa kule shambani ni ya Naomi yameoana na mke wangu Naomi?” amehoji.
Kuhusu matone ya damu ambayo wapelelezi walichukua chumbani kwa marehemu na kwenye banda la kuku, alidai si ya kweli.
“Hivi Mheshimiwa, kweli mimi nifanye tukio hilo halafu zile damu niziache tu? Wanasema kuna damu nyingine walizikuta kwenye chaga, mheshimiwa hakuna damu mahali popote,” alidai.
Alidai walichokuwa wanafanya polisi walikuwa wanabahatisha tu kuwa hiyo ni damu, maana miezi miwili huwezi kukuta damu.
Kuhusu ripoti ya Mkemia ya uchunguzi wa sampuli iliyodaiwa kuwa ni matone ya damu yaliyochukuliwa eneo la tukio ni ya jinsi ya kike, alidai alikuwa yake na kawaida ya kuwa na wanawake wengine.
Alidai mwanamke (kati ya hao aliokuwa akiwapeleka kwake) anaweza kuingia kwenye hedhi, hali ambayo si ajabu na kwamba wanawake wengine ni wazembe anaweza kutoa uchafu ule akautupa pale.
Alidai hata mkewe alikuwa akiingia kwenye hedhi, hivyo damu kuwemo ndani ya chumba cha mume na mke ni jambo la kawaida.
“Ndiyo maana nasema hawa uchunguzi wao ulikuwa mbovu sana. Wala hakuna uthibitisho kuwa mke wangu amefariki lakini wanataka tu ninyongwe.
“Mheshimiwa Jaji kulingana na hay,a naomba Mahakama yako iniachie huru niendelee kumtafuta mke wangu na upande wa mashtaka unapaswa kutekeleza wajibu wao waendelee kumtafuta mke wangu mahali aliko au wanimbie mwenyewe mahali aliko.”
Keshi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu Novemba 25, 2024 siku ambayo daktari aliyemchunguza afya ya akili atahojiwa na upande wa mashtaka.