Taoussi mzuka umepanda Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Rachid Taoussi amesema kikosi hicho kwa sasa kipo tayari kwa ajili ya kuendeleza ushindani msimu huu, wakati itakapocheza na Kagera Sugar Jumamosi hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar.

Akizungumza na Mwanaspoti, Taoussi alisema licha ya kukaa wiki mbili bila ya mchezo wowote wa kiushindani, lakini bado ameridhishwa na uwezo wa wachezaji katika mazoezi hasa kwa wale waliokosekana timu zao za taifa.

“Tumekuwa na maandalizi mazuri na kama nilivyosema tangu awali malengo yetu ni kuendelea kushikilia nafasi tuliyopo na ikiwezekana tuzidi kusogea juu walipo wapinzani wetu, hakuna kilichobadilika zaidi ya morali kwa kila mmoja wao hapa,” alisema.

Taoussi aliongeza kwamba, jambo zuri ndani ya timu hiyo kwa sasa ni kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi akiwemo Sospeter Bajana na Yahya Zayd, ambao wameongeza wigo mpana wa machaguo katika eneo la kiungo cha kati.

“Kwa hali ya kikosi kwa sasa ni nzuri na hakuna taarifa ya majeraha mapya ambayo tumeyapata, baada ya ujio wa nyota wengine waliokuwa katika timu za taifa ndipo tutafanya tathimini ya mwisho kwa ajili ya mchezo wetu na Kagera Sugar,” alisema Taoussi.

Kikosi hicho kitapambana na Kagera Sugar inayojitafuta msimu huu, huku rekodi zikionyesha mara ya mwisho zilipokutana katika Ligi Kuu Bara Uwanja wa Azam Complex, Azam FC ilishinda kwa mabao 5-1. Ilikuwa Mei 25 mwaka huu.

Tangu Kocha Taoussi ateuliwe kukiongoza kikosi hicho Septemba 7 mwaka huu akichukua nafasi ya Msenegali, Yousouph Dabo, ameiongoza Azam FC katika michezo tisa ya Ligi Kuu Bara, ameshinda sita, sare miwili na kupoteza mmoja tu.

Msimu huu Azam FC imecheza michezo 10 ya Ligi Kuu Bara ikishinda sita, sare mitatu na kupoteza mmoja.

Related Posts