MSHAMBULIAJI wa Geita Gold, Andrew Simchimba ambaye katika mechi tisa za Ligi ya Championship msimu huu amefunga mabao sita, amesema malengo yake ni kumaliza msimu akiwa na mabao kuanzia 10.
Msimu uliopita akiwa na KMC, mshambuliaji huyo alicheza mechi moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu, hivyo anatamani msimu huu arejee katika kiwango chake.
“Msimu uliopita niliumia sana hadi nilikata tamaa ya kuendelea na soka, nashukuru kuna watu ambao walikaa karibu na mimi kunijenga kuona changamoto katika maisha haziepukiki.
“Tangu nilipoumia mwaka jana Novemba, nimepona Julai mwaka huu, ndio maana natamani kupata mechi nyingi ili niendelee kuwa fiti,” alisema.
Simchimba aliongeza kuwa ingawa Championship ni ngumu lakini kikubwa wanachopigania ni pointi tatu kufikia malengo.
“Ligi ya Championship inahitaji fiziki, stamina na pumzi, ushindani uliopo unafanya nijitume zaidi mazoezini ili nitimize ndoto zangu,” alisema.