Dar es Salaam. Mtapona kwa uwezo wa Mungu. Ndilo neno lililotawala kinywani mwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipowatembelea na kuwajulia hali majeruhi wa ajali ya jengo la ghorofa nne lililoporomoka Kariakoo.
Jengo hilo, liliporomoka Jumamosi, Novemba 16, 2024 na mpaka sasa limesababisha vifo vya watu 20 na majeruhi zaidi ya 86, uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.
Siku jengo hilo linaporomoka, Rais Samia alikuwa njiani kwenda Brazil kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa kundi la G20 na akiwa huko alikuwa amatoa maagizo kwa watendaji akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu uokoaji.
Leo Jumatano, Novemba 20, 2024, Rais Samia amewasili nchini na kwenda Kariakoo kujionea hali ilivyokuwa na kuzangumza na wafanyabiashara na wananchi. Baada ya hapo, mkuu huyo alienda Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kuwajulia hali majeruhi waliolazwa hapo.
Akiwa hospitalini hapo, Rais Samia amepita katika wodi za wanawake na wanaume na kumjulia hali mgonjwa mmoja baada ya mwingine akiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Lemery Mchome.
Karibu kila majeruhi aliyemtembelea Rais Samia alikuwa akimuuliza maendeleo yake ya afya yake, alichokuwa anafanya Kariakoo na kumfariji kuwa Mungu atamsaidia atapona.
Alipofika kwenye kitanda cha Clement Jackson ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Charambe, alimuuliza alikuwa anafanya nini Kariakoo, ndipo alipohoji majibu kuwa anafanya biashara.
“Unafanyaje biashara mwanangu na wewe ni mwanafunzi,” amehoji Rais Samia.
Akijibu swali hilo, Jackson amesema, “nilienda kumsaidia kaka yangu kuuza kwenye duka lake, huwa nafanya hivyo mwishoni mwa juma ndipo janga hili likanikuta.”
Baada ya maelezo hayo, Rais Samia akaonyeshwa kuridhishwa na majibu hayo na kumuahidi kushughulikia suala lake la mtihani mmoja ulioasalia, ambao angepaswa kuufanya kesho Alhamisi Novemba 21, 2024.
“Utapona tu, utarudi shule, wizara itakuangalia, kama kurudia mitihani au nini tutaongea na wizara kwa sasa mshukuru Mungu na usali sana,” amesema Rais Samia.
Mapema leo Jumatano, Mwananchi ilizungumza na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Said Mohamed ambaye alieleza taratibu zitafuatwa kuhakikisha mwanafunzi huyo hapotezi haki yake.
“Baraza lina taratibu zake litaandaa taarifa zake na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha hatapoteza haki ya kufanya mtihani wake wa mwisho,” amesema Dk Mohamed.
Mitihani ya kidato cha nne, ilianza Novemba 11 na itamazika Novemba 29, 2024.
Mtihani ambao Jacksona amesalia kuufanya ambao angepaswa kufanya kesho Alhamisi ni wa Biolojia kwa vitendo.
Mwananchi lilimtafuta Dk Mohamed baada ya Novemba 19, 2024 wakati akisimulia tukio lilivyokuwa, mwanafunzi huyo pamoja na mambo mengine, aliomba kusaidiwa ili kumwezesha kufanya mtihani huo wa Baiolojia.