Besigye ashtakiwa mahakama ya kijeshi kwa njama za kulipua kambi

Kampala. Mwanasiasa mkongwe wa upinzani wa Uganda, Dk Kizza Besigye aliyetoweka Nairobi nchini Kenya Jumamosi na baadaye kudaiwa kutekwa, ameibukia kizimbani kwenye mahakama ya kijeshi nchini Uganda.

Besigye amefikishwa mahakamani jijini Kampala leo Jumatano, Novemba 20, 2024, na kusomewa mashtaka kadhaa, likiwemo kosa la kumiliki bunduki kinyume cha sheria.

Pia, anakabiliwa na tuhuma za kufanya mikutano katika nchi za Kenya, Uswisi na Ugiriki kwa lengo la kusaka uungwaji mkono wa kifedha na zana kwa lengo la kushambulia kambi za kijeshi nchini Uganda.

Imedaiwa mipango hiyo inalenga kuhujumu usalama wa Jeshi la Uganda (UPDF).

Wakili wa Dk Besigye, Erias Lukwago amesema hati ya mashtaka ilikuwa na dosari.

“Kwa hivyo kesi hii ni batili,” ameliambia Shirika la Habari la Reuters baada ya Dk Besigye kukana mashtaka yote dhidi yake.

Kulingana na Reuters, Dk Besigye amepelekwa mahambusu katika Gereza la Luzira hadi Desemba 2, 2024.

Awali, mkewe kiongozi huyo wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC), Winnie Byanyima alidai kuwa mumewe alitekwa na maofisa wa usalama wa Uganda wakisaidiwa na wenzao wa Kenya.

“Ninaomba Serikali ya Uganda imwachilie huru mume wangu, Dk Kizza Besigye kutoka mahabusu ya kijeshi ambamo wamemzuilia. Yeye si mwanajeshi,” amesema kupitia mtandao wa X (zamani Twitter).

Dk Besigye ambaye alienda Kenya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na mwanasiasa Martha Karua, alitoweka Jumamosi jioni katika jengo la 108 Riverside Apartment, eneo la Westlands ambako ilisemekana alienda kukutana na ‘watu fulani.’

Alikuwa amekodisha chumba cha kulala Waridi Paradise Hotel and Suites katika mtaa wa Hurlingham, Nairobi.

Kiongozi huyo wa upinzani Uganda alitarajiwa kuwa miongoni mwa wahutubiaji Jumapili Novemba 17, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, akatoweka.

Wapinzani Afrika wataka aachiwe

Viongozi wa upinzani Afrika wameshinikiza kuachiliwa huru kwa Dk Besigye. Pia, wamelaani mienendo ya Serikali za mataifa ya Afrika wanazosema zinaendeleza vitendo vinavyokiuka sheria.

Kwenye taarifa ya Jumatano, Novemba 20, 2024 wanachama wa muungano wa viongozi hao (PAOLSN), tawi la Afrika Mashariki, wamedai Dk Besigye alitekwa na maofisa wa usalama wa Kenya wakishirikiana na wenzao wa Uganda.

“Tukio hilo linaudhi na kuogofya zaidi. Tunashuku kuwa Dk Besigye huenda alitekwa nyara baada ya kufikishwa katika jengo la Riverside Apartment. Na waliohusika ni maofisa wa usalama wa Uganda wakisaidiana na maofisa wa usalama wa Kenya,” umesema muungano huo, kwenye taarifa iliyotiwa saini na kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua.

“Tunataka vyombo vya usalama nchini Kenya, haswa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) kufichua aliko Dk Besigye. Utekaji unaoendeshwa na maofisa wa usalama ni kinyume cha sheria ya ushirikiano kati ya Kenya na Uganda. Huu ni ukiukaji wa sheria za nchi husika na sheria za kimataifa,” taarifa hiyo imeongeza.

Hata hivyo, msemaji wa Polisi nchini Kenya, Dk Resila Onyango amekana madai kuwa Dk Besigye, ambaye ni kiongozi wa FDC alitekwa nchini Kenya.

“Hatuna habari zozote kuwa mwanasiasa wa Uganda Kizza Besigye alitekwa. Kutoweka kwake hakumaanishi kuwa amatekwa. Hata hivyo, uchunguzi unaendelea kuhusu kisa hicho,” alisema.

Wakati huohuo, Serikali ya Uganda imevunja ukimya kuhusu suala hilo ikishikilia kuwa haina habari kuhusu kutoweka kwa Dk Besigye jijini Nairobi.

Katika mahojiano na gazeti la “Daily Monitor” Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) na Mwongozo wa Kitaifa, Chris Baryomunsi, amekana kuwa na habari kuhusu tukio hilo na kusema Serikali itafanya uchunguzi kubaini ukweli.

Related Posts