KATIBU wa Halmashauri Kuu( NEC) Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu Issa Gavu amewataka wananchi wa Mkoa wa Geita kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novembe 27 mwaka huu nchini.
Gavu ametoa kauli hiyo leo Novemba 20,2024 mbele ya mamia ya wananchi wakiwemo wanachama wa ccm alipokuwa akizindua rasmi kampeni za uchaguzi huo ambapo Chama hicho pia kimezindua kampeni zake nchini kote.
“Nawaomba wananchi wa Geita na wanachama wa chama cha Mapinduzi,kuchagua wagombea wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ili kusukuma mbele maendeleo yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Wetu Dk.Samia Suluhu Hassan.”
Gavu pia amewaomba wagombea kunadi maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita katika maeneo yao na kusisitiza wagombea wanayo nafasi ya kuyaelezea mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2020-2025.