Undani miongo saba ya mishemishe Soko la Feri

Inaelezwa kuwa umri wa soko maarufu la samaki jijini Dar es Salaam (Feri) ni miaka 74 na kilichobadilika ni wingi wa watu, majengo mapya na jina tu, lakini mishemishe za wavuvi na wengine wanaonufaika na uvuvi ndo zinazidi kutaradadi.

Nyakati za asubuhi ukipata gari la umma linaoelekea Kivukoni (lilipo soko la Feri) wakati mwingine utakutana na watu, hususan wanawake wenye ndoo tu na jioni ukipanda gari kutokea uelekeo huo unakutana na zile ndoo na vikapu vikiwa na samaki au dagaa, wakati mwingine na chachandu pembeni.

Meneja wa Soko hilo la Kimataifa la Samaki, Abdallah Mfinanga akielezea historia ya soko hilo, anasema lipo tangu mwaka 1950.

“Soko lilianzishwa mwaka 1950, wakati huo likiitwa Banda Beach, soko hili lipo hata kabla ya kupata uhuru, lilikuwa ni sehemu ya meli kutia nanga na maisha mengine kuendelea. Watu wa Pwani walikuwa wakivua samaki na kuchuuza hapa hapa, na mazao mengine ya baharini.”

Anasema baadaye biashara ilikuwa zaidi eneo la bahari na samaki wanaovuliwa walikuwa wakipelekwa Miti Mirefu (Mbele ya Kilimanjaro Hotel).

Anasema baada ya watu kuongezeka, miaka ya 1980 lilijengwa soko dogo lililopo zone namba 8 A na baada ya mtoto wa mfalme wa Japan kutembelea soko hilo aliishawishi nchi yake kusaidia ujenzi wa soko jipya la samaki Feri kuanzia mwaka 1999 na likakamilika mwaka 2002.

“Hili soko lina ukubwa wa mita za mraba 14,776 na lina uwezo wa kubebe watu 1,200 na sasa tuna wafanyabiashara 3,500, baada ya kuzinduliwa lilibadilishwa jina kutoka Banda Beach likapewa jina la Soko la Samaki la Kimataifa la Feri, jina ambalo linaendelea mpaka leo.”

Mbali na kubeba historia ndefu ya shughuli za uvuvi hapa nchini, soko hilo ni eneo muhimu kiuchumi. Mwaka 2021 Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilitoa takwimu kuwa soko hilo lenye watumiaji zaidi ya 10,000 kwa siku linatoa ajira rasmi zipatazo 117 na ajira zisizo rasmi takribani 2,780, huku likichangia mapato ya Serikali kwa Sh135 milioni hadi Sh150 milioni.

Soko la Kimataifa la Samaki Feri ni kivutio kikubwa cha watalii wa chakula, watu kutoka mataifa mbalimbali hutembelea soko hilo kuonja samaki wa aina tofauti na katika mtandao wa Tripadvasor eneo hilo limepewa nyote nne na watu waliolitembelea.

Feri, linalopatikana katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam ni moja ya maeneo maarufu yanayoleta pamoja wachuuzi, wavuvi na wanunuzi kutoka pembe zote za mji.

Soko hili limekuwa chanzo cha riziki kwa wengi, si tu kwa wauzaji wa samaki, bali pia kwa wafanyabiashara wa bidhaa nyingine zinazotegemea bidhaa za baharini.

Kila siku, kabla ya alfajiri, wavuvi hukusanyika na samaki wao waliowavua usiku kucha. Wanunuzi, wakiwemo wauzaji wa rejareja, wafanyabiashara wa jumla, na wamiliki wa migahawa, hufika sokoni hapo.

Mbali na samaki wa aina mbalimbali kama Jodari, vibua, changu na kolekole, pia kuna viumbe wengine wa baharini kama kamba, kaa, pweza na chaza wanaopatikana kwa urahisi katika soko hili.

Ukifika tu unajua uko ufukweni

Mara tu unapoingia, utakaribishwa na harufu kali ya samaki na maji ya chumvi. Wafanyabiashara wanajituma, huku wakishindana kwa sauti kuvutia wateja wanaopita.

“Mama samaki! Karibu mpwa! Huku ndiko kwa bei poa!” ni maneno yanayokaribisha wageni na wakazi wanaokuja kununua au kuuza bidhaa mbalimbali.

Katika soko hili, biashara ya samaki inatawala, huku wauzaji wakiwa wamesimama pembeni ya meza zao ambazo wamepanga samaki aina mbalimbali kutoka bahari ya Hindi.

Kama mgeni, unaweza kutambua haraka kuwa soko la Feri si mahali pa kawaida. Wauzaji, wakiwa na mikono yenye matone ya maji ya chumvi, wananyanyua na kushusha samaki kwa ustadi mkubwa.

Mifuko mikubwa ya barafu imewekwa pembeni kwa ajili ya kuhifadhi samaki katika hali bora, huku wateja wakiwa na uhuru wa kuchagua samaki wanaowataka kutegemea uwezo wao kifedha.

Paa kubwa limefunika sehemu ya soko hili, kuzuia jua kali la Dar es Salaam, huku hewa nzito itokanayo na harufu ya bahari, samaki na wingi wa watu ikikumbusha kwamba hapa ni kituo kikubwa cha biashara.

Kwa mgeni anayefika katika soko la Feri kwa mara ya kwanza, hii ni safari ya kipekee kwanza, atakutana na mandhari tofauti na yenye msisimko, huku harufu ya bahari na sauti za wafanyabiashara zikimkaribisha kwa uzito.

Ingawa hali ya hewa ya ndani ya soko inaweza kuwa nzito kidogo kutokana na mazingira ya biashara ya samaki, wageni wanaelezwa kuwa uzoefu huo unawafundisha mengi kuhusu namna ya kuendesha biashara kwenye soko kubwa kama hili.

Mara nyingi, wageni hujifunza mengi kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hili kutokana na tabasamu lao na ustadi wa kuwashawishi wateja.

Mishemishe za soko la Feri zinaanza saa 11 alfajiri, kabla ya jua kuonekana, muda huo wafanyabiashara wanakuwa katika soko hilo kwa nje wakisubiri saa 12:00 asubuhi soko lifunguliwe na wao kuingia.

Kutembea ndani ya soko hili ni sawa na kuingia katika ulimwengu mpya wa harakati za kibiashara. Kila kona ina ladha yake, kila eneo lina sauti tofauti na kila mmoja ana hadithi ya kipekee kuhusu jinsi anavyopambana na changamoto za biashara na ugumu wa maisha.

Miongoni mwa sauti hizo ni za madalali wauza dagaa, wauza barafu, wafanya mnada, wavuvi, wasafisha samaki, wauza maboksi, wabeba mizigo na wapakiaji wa samaki.

Wavuvi hawa huleta samaki wao alfajiri na wengine jioni kwa kutegemeana na chombo kiliondoka saa ngapi, kwa kuwa kuna wanaoondoka jioni na kurudi alfajiri na wengine wanaondoka asubuhi na kurudi saa 9 au 10 jioni.

Hivyo wavuvi hao wanapofika sokoni asubuhi, hutangaza bidhaa zao kwa mbwembwe, huku kukisikika kelele zitokanazo na watu wengi kupayuka.

“Umeshinda kwenye maji usiku kucha unarudi nyumbani … haya chukua mzigo huo upeleke kwa mama Habiba upokelewe na watoto wako baba katoka kazini,” ni kauli za wavuvi, huku vicheko na utani vikiendelea katika eneo la bahari na kuonekana ni jambo la kawaida.

Mvuvi Ali Ame (32) anasema, “Bahari ipo sawa na lazima tushike kazi kwa ujasiri. Samaki tunaoleta hapa ni wa uhakika. Kazi yetu ni kukuletea samaki kutoka baharini,”

Anasema wao jukumu lao ni kushusha samaki na kiongozi wao ndiye anayepanga bei ambao wanapelekwa kwenye mnada au kwa wauzaji wa rejareja, kwa hiyo sio jukumu lao kusimamia na kujua gharama iliyouzwa kwa sababu pesa inayopatikana ipo kwenye mgawanyo wa makundi mengi.

“Pesa inayopatikana inagawanywa kwa watu wengi, sisi tuliokuwa kwenye chombo, tajiri mwenye chombo, ushuru wa Serikali na wauzaji wenyewe, kwa hiyo siku kukiwa na uhaba wa dagaa na samaki ndipo tunapopata pesa nzuri, mgawo unaweza kuwa hadi Sh 20,000 hiyo siku,” anasema Ame.

Wafanya mnada ni kundi maalumu la wachuuzi ambalo hupiga mnada samaki wa ukubwa na aina mbalimbali na wateja ndiyo wenye jukumu la kuongeza bei.

“Hawa hapa samaki, 10, 11, 12, 13 (hizo ni pesa kuanzia Sh 10,000 na kuendelea) haya mara ya kwanza 13 mara ya pili, mara ya tatu,” anasema Ramadhani, ambaye amekuwa akifanya kazi ya mnada kwa zaidi ya miaka mitano.

Wateja wanafurika karibu naye wakijaribu kushindana katika mnada. “Tunawafanyia mnada ili kila mmoja aweze kuchagua kadiri ya uwezo wake,” anaeleza. Mnada unapamba moto, huku wateja wakihimizana kupandisha bei na Ramadhan anaonekana mwenye furaha na haraka za kumaliza ili aweke samaki wengine.

Katika soko hilo sehemu ya mnada wa dagaa wamejaa wanawake wengi kuliko wanaume na kwenye mnada wa ngisi na pweza wanaume ni wengi, huku wanawake wakiwa wa kuhesabu ama mmoja au wawili.

“Wanasema biashara hii ni ya kiume ndiyo maana unaona tumejaa wanaume wengi na hata ukipita kwenye biashara huku mitaani unakuta wanaume wanauza pweza, sina hakika kama kuna wanawake,” anasema Zakaria Rajabu, aliyekutwa kwenye mnada wa pweza.

Katika soko hili, pia kuna wafanyakazi maalumu wa kusafisha samaki, hivyo ukinunua samaki wako ukipenda unasafishiwa hapo hapo.

“Tunakata na kusafisha kwa haraka sana. Hauhitaji kusubiri, dakika mbili tu samaki wako wameshasafishwa,” anasema Hussein Mkude, maarufu kama Mjomba.

Mkude anasema kazi hiyo inahitaji kuwa na vifaa sahihi na kufahamu mbinu za kusafisha na kukata kwa ufanisi ili kuvutia wateja wengi na uharaka, maana wateja hawana muda wa kupoteza.

Anasema usafishaji wa samaki wanaanzia Sh1,000 na inategemea na wingi wa samaki na aina pia, kwani wapo ambao wanakuwa na magamba mengi na magumu na wapo ambao usafishaji wake ni rahisi.

Kwa upande wa wafanya usafi ni kila baada ya muda wanamwaga maji na kuzoa kile kilichotupwa chini ili kuhakikisha kuwa soko hilo muda wote linakuwa safi.

“Tunafanya usafi kwa sababu ni ajira yetu hii na sichagui, naweza kufanya usafi hapa nikaenda na kusafisha bajaji zilizoleta samaki pia au gari wananipa Sh1,000, kwa hiyo uhakika wa maisha upo,” anasema Ezekiel.

Mbali na samaki wanaovuliwa na wavuvi wa eneo hilo, soko la Feri pia ni kituo cha mauzo ya samaki wanaotoka maeneo mengine, samaki hao huletwa kwa magari, pikipiki na bajaji.

Samaki hao huuzwa katika kanda namba nne A, hapo unakutana na majokofu mengi na nyuma yake kuna wafanyabiashara wanaouza samaki kwa kilo, huku wakiwa wamewekwa juu ya meza.

“Si samaki wote wanavuliwa siku husika, wengine wanakuwa wamelala kutokana na muda walioletwa maana wapo wanaokuja jioni ambapo tunasema ‘Maji ya jioni’ na wakati huo hakuna wateja, pia hapa tunahifadhi samaki wanaoletwa kutoka mikoani na nje ya nchi,” anasema mmoja wa wauza samaki.

Aidha, ukiachilia mbali ununuzi wa samaki kwa bei ya jumla, pia katika soko hilo kuna wachuuzi wa rejareja.

Vilevile, katika soko hilo pia ipo mitumbwi inayosafirisha abiria kutoka na kwenda Kigamboni wanaita usafiri wa haraka, nao wanasikika wakihamasisha abiria.

“Safari hii hapa Kigamboni, dakika chache hadi upande wa pili!” wanaita kwa sauti kubwa huku wakihamasisha abiria kuingia kwenye boti.

Usafiri wa Feri kuelekea Kigamboni ni sehemu muhimu ya biashara na maisha ya wakazi wengi wa Dar es Salaam, na mzunguko huu wa usafiri umeongeza uhai sokoni kwa wageni wanaotembelea.

Kanda namba nne B hutumiwa na wavuvi kupumzika na kufanyia marekebisho vyombo vyao, kurekebisha vifaa vinavyotumika kuvulia samaki.

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Soko la Feri, Nassoro Mbaga anasema eneo hilo linatumika kwa ajili ya wavuvi, kwani hata kiongozi wao ni mvuvi, licha ya uwepo wa mama na baba lishe pia.

“Kutokana na ufinyu wa maeneo, wafanyabiashara ya chakula waliwekwa katika makundi matatu ambapo waligawanywa katika kanda ya nne, saba na nane na hapa wanakutana na wavuvi,” anasema Mbaga.

Vilevile anasema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya watu kufanya udalali ambapo wanaharibu sifa ya soko kwa kuwakamata wateja na kuwazuia kuingia sehemu maalumu zilizowekwa kwa ajili ya manunuzi ya samaki.

“Madalali wana tabia ya kuwakamata wateja getini kwa wale wageni na kuwaambia samaki wa eneo fulani ni wabovu, hivyo ampeleke moja kwa moja kwa wavuvi, kumbe si kweli, wanazunguka na kuwachukulia wale waliosema wabovu,” anasema.

Anasema wapo madalali ambao wanaibia wateja wakati wa mnada, wanakusanya pesa na kisha kutoweka nazo, kwa kuwa hawajasajiliwa ni ngumu kutatua jambo hilo.

Kutokana na changamoto hiyo anasema wameshaandaa muongozo kwa ajili ya kutambua wafanyakazi wa soko hilo ambapo baadhi ya vikundi kama cha Bagamoyo wameshaweka sare za watu wao.

Dawa za kulevya na vileo sokoni

Katika eneo la fukwe wanapoweka vyombo vyao vya kuvulia samaki, baadhi ya wavuvi vijana hujipumzisha kwa muda, huku wakivuta sigara na vingine vinavyofanana na tumbaku kwa kudai kuwa wanatafuta stimu ya kufanya kazi na kupata usingizi.

“Baharini kuna mambo mengi, bila kutumia hivi vitu unaweza usilale na kuingia woga wa kufanya kazi, natumia hiki kitu ili nione kitu cha kawaida nitakachokutana nacho kwenye bahari na muda huu kinanipa mzuka wa kulala,” anasema kijana Mudi (siyo jina lake halisi).

Kutokana na matumizi hayo, alipozungumza na Mwananchi, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alisema wameanza kutoa elimu kwa watu wote wanaohusika katika fukwe za bahari, wakiwepo wavuvi, wafanyabiashara na mabeach boy.

“Kwa sasa tumeanza kutoa elimu ikihusisha watu wote wanaojishughulisha kwenye bahari kwa kushirikiana na wenzetu wa jeshi la Marine ili kuwaeleza kile tulichokusudia kuhusu matumizi na biashara ya madawa ya kulevya,” alisema Lyimo.

Related Posts