Tukio la kuanguka kwa jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Congo na Mchikichi jijini Dar es Salaam liliibua simanzi miongoni mwa watu, kutokana na kusababisha vifo na majeraha kwa makumi ya watu.
Ghorofa hilo liliporomoka asubuhi ya Novemba 16, 2024. Picha zilizopigwa eneo la ajali tangu siku ya kwanza zinaonyesha namna jengo hilo lililokuwa likitumiwa kwa ajili ya maduka na uhifadhi wa mizigo lilivyo sasa.
Katika picha hizo si tu utaona waokoaji wakifanya shughuli zao, bali utashuhudia bidhaa zilizotapakaa na nyingine zilikiwa zimegandamizwa na maporomoko ya ukuta na kulaliwa na nguzo za zege.
Mpaka sasa hasara ya uhai iliyopatikana ni kubwa, lakini pia hasara ya mali nayo bila shaka si haba, kwani hakuna mwenye uhakika wa kukuta mali zake kama alivyoziacha.
Japo kwao inaweza kuwa zaidi, lakini hasara hiyo haiishii tu kwa waliokuwa na maduka katika jengo, bali wafanyabiashara wengi, hususan wa mitaa jirani.
Katika mitaa ya Congo, Aggrey, Manyema, Msimbazi, Muhonda na Mchikichi iliyopo karibu na ilipotokea ajali hiyo, maduka yake yamefungwa hivi sasa kwa siku tatu mfululizo.
Sababu za kufungwa kwa maduka hayo ni tahadhari za kiusalama, lakini pia lengo ni kupunguza msongamano katika eneo hilo ili kurahisisha shughuli za uokoaji.
Pamoja na hofu ambayo inaibuka sasa katika majengo ya Kariakoo, wafanyabiashara wa mitaa iliyofungwa sasa wana kiu ya kurejea katika shughuli zao, huku wakidai kukosa mapato, jambo ambalo linaanza kuwapa hali ngumu ya kifedha.
Kufungwa kwa maduka hayo pia kumewaathiri wateja wa bidhaa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ambao wamekuwa wakitegemea Kariakoo kwa ununuzi wa bidhaa, hususan wanunuzi wa nguo.
Mitaa iliyofungwa ni maarufu zaidi kwa uuzaji wa nguo, lakini pia vifaa vya muziki, huku Muhonda ikiwa ni kwa biashara mchanganyiko na Narung’ombe ni mtaa maarufu wa manunuzi ya viatu.
Katika siku za kawaida mitaa ya Congo na Msimbazi inakuwa na pilikapilika nyingi za kibiashara, yaani ni mwendo wa msongamano wa watu, magari na mikokoteni kutoka na ufinyu wa njia, kwani barabara zake hugeuka meza ya wachuuzi.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Amina Mwinyi, mchumi wa biashara anasema ajali hiyo imesababisha hasara kubwa kwa wafanyabiashara na hata nchi.
Anasema kuanguka kwa jengo na kufungwa kwa maduka kuna madhara makubwa kwa uchumi wa nchi kutokana na kodi iliyokuwa inaingia Serikalini kwa siku na wale ambao wanategemea kuingiza pato la siku pia wamepata hasara na kupoteza wateja.
“Karikaoo ni kitovu muhimu cha biashara ya jumla na rejareja nchini, kufungwa kwa maduka katika eneo hilo kunaleta mapungufu ya bidhaa, kuongeza gharama za biashara, na kuathiri usambazaji wa bidhaa katika masoko mbalimbali,” anasema Dk Amina.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana yeye anasema mzunguko wa pesa umeshuka na wakati huohuo kuna wafanyabiashara wana mikopo ya taasisi za kifedha, hivyo ajali hiyo imeleta changamoto kubwa kwao.
“Kinachotufanya tuvumilie yote hayo ni kwamba wafanyabiashara wenzetu bado wapo hai wapo chini na wanapiga simu kwa wenzetu wakiendelea kuwasiliana nao,”anasema Mbwana.
Anasema mitaa iliyofungwa kwa kawaida ina umati mkubwa, hivyo kufungwa kwake kunasaidia upatikanaji wa mawasiliano kwa hurahisi na wale waliopo chini, kwani kukiwa na msongamano kunakuwa na mawasiliano hafifu.
Mbwana anasema hadi Jumatatu ya Novemba 18 baadhi ya mitaa ilianza kufunguliwa, lakini inayozunguka jengo hilo na mtaa husika wa Mchikichi itaendelea kufungwa ili kuzuia watu kujazana na kushangaa kinachoendelea na inaweza kuzua taharuki.
Kwa wafanyabiashara waliofunga maduka yao, hasara ya kila siku imekuwa kubwa. Wengi wanategemea mapato ya kila siku kumudu mahitaji ya kila siku na kuendeleza biashara zao.
“Nafungua duka kila siku ili kupata pesa za kulipia kodi ya fremu na pia chakula cha familia, sasa nimepoteza mapato ya zaidi ya Sh200,000 kila siku tangu nifunge duka,” anasema Yusuf Omari, mfanyabiashara wa nguo mtaa wa Aggrey.
Wengine wameeleza kuwa wateja wao wa kawaida wameanza kulalamikia kutofikiwa kwa bidhaa wanazozihitaji.
“Wateja wanapiga simu wakitaka bidhaa, lakini sina jinsi, siwezi kufungua duka hadi pale Serikali itakaposema tufungue maana siku ambayo jengo lilianguka tulifungua lakini siku ya pili hatukutakiwa kufanya hivyo ili kupisha uokoaji,” anasema Rehema Athumani, mfanyabiashara wa vifaa vya umeme mtaa wa Msimbazi.
Anasema kwa siku mbili alizofunga hajaingiza kipato ambacho anaingiza akifika dukani, kwani kwa uhakika kila siku anaingiza faida si chini ya Sh300, 000.
Wafanyabiashara wadogo wa mtandaoni, wamachinga na wakopeshaji mtaani wameeleza changamoto wanazokumbana nazo baada ya kufungwa kwa maduka Kariakoo.
Wanaeleza kuwa tukio hili limewazuia kupata bidhaa kwa wakati, hali inayosababisha kukwama kwa huduma zao.
Fadhili John, mfanyabiashara wa mtandaoni (winga) anayeuza nguo, anasema: “Kwa kawaida, karibu kila siku naenda Kariakoo kuchukua mzigo, tangu litokee tukio siwezi kufanya hivyo kwa sababu naweka bidhaa kwenye mitandao ya kijamii, kwanza mteja akihitaji namfuatia, lakini sina njia nyingine ya haraka ya kupata mzigo.”
Salome John, muuza vilemba mtaa wa Congo na Narung’ombe anasema hali imekuwa mbaya kwake kwa kukosa kijiwe cha kusimama ili kukutana na wateja wake, kwani baada ya kubomoka kwa jengo barabara zimefungwa.
“Nilishajiwekea kijiwe changu, sasa njia hakuna, sehemu zote zina ulinzi, ni ngumu kufanya biashara na hapa nilikuwa nina uhakika wa kuondoka na Sh50,000 kama faida kwa siku,” anasema Salome.
Kufungwa kwa baadhi ya mitaa na maduka wafanyabiashara wadogo wamejikuta katika wakati mgumu, kwani wapo wanaotegemea wamekuwa wakichuka mizigo katika maduka na kupata kipato cha siku.
Baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na visiwa vya Comoro wanaofika kwa ajili ya kununua bidhaa mbalimbali za kuuza katika masoko yao ya ndani sasa wamesalia hotelini ili kwanza hali iimarike.
Zabron Hantumbu, mfanyabiashara kutoka Zambia anasema hali ya sasa imekuwa ngumu kwake, kwani alihitaji kufunga mzigo Novemba 17 mwaka huu, lakini amejikuta akitumia gharama zaidi za kuishi, kwani muda wake wa kukaa hoteli umezidi.
“Nimekuwa hapa tangu Alhamisi (Novemba 14) nikitarajia kupakia bidhaa zangu kwa ajili ya msimu wa Krismasi. Sasa maduka ambayo nilitarajia kuchukua mzigo yamefungwa na siwezi kurudi nyumbani mikono mitupu. Gharama za hoteli na chakula zimekuwa kubwa mno, nilipanga kutumia Sh150,000 kulala siku mbili tu,” anasema Hantumbu.
Anaongeza: “Nilikuwa nimepanga kuweka oda kubwa, lakini sasa nalazimika kutumia pesa nyingi kwa maisha yangu hapa badala ya biashara. Hali hii ni mbaya kwa sisi na kwa wafanyabiashara wa Kariakoo pia”.
Kwa mujibu wa Hantumbu, ajali hiyo imekuwa kubwa kwao na wanajaribu pia kuulizana na wafanyabiashara wengine kama kuna wenzao walifika katika ghorofa hilo.
Inaelezwa kuwa kwa asili ghorofa hilo lilikuwa na sehemu tatu, lakini liliongezewa sehemu ya juu ambapo katika ghorofa ya pili, tatu na hiyo iliyoongezewa ziligeuzwa kuwa stoo za kuhifadhia mizigo.
Kwa maelezo ya mbeba mizigo wa jengo hilo, Hamidu Ally, ghorofa hilo lilikuwa na stoo nyingi, kwani katika floo ya kwanza kulikuwa na stoo zaidi 10 ambapo kwa hesabu ya haraka unaweza sema kulikuwa na stoo za mizigo zaidi ya 40.
“Si rahisi kuhesabu, lakini vipo vyumba vya kuhifadhia mizigo zaidi ya kumi na kuna maduka zaidi ya 30 kwenye hili jengo, kuna upande wa huku mbele na kule nyuma,” anasema Ally.