Moshi. Wakati baadhi ya vyama vya siasa vikizindua kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, mkoani Kilimanjaro, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejinadi kwa kutumia miradi ambayo imetekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu huku kikiwataka wabunge wa Mkoa huo, kutoa mitungi ya gesi ya kupikia kwa wananchi ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Mbali na kuwagawia mitungi hiyo, pia chama hicho kimewataka wabunge kupambana kuhakikisha bei ya gesi ya kupikia inashuka ili kila mwananchi aweze kumudu gharama.
Kampeni hizo zilianza jana Jumatano, Novemba 20, 2024 ambapo katika viwanja vya Pasua sokoni Manispaa ya Moshi, Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (Suki) na Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, Rabia Abdallah Hamid amesema chama hicho kimefanya kazi kubwa za maendeleo mkoani Kikimanjaro, hivyo wananchi wanapaswa kukiunga mkono kwa kuhakikisha kinawachagua viongozi wa serikali za mitaa wanaotokana na CCM.
“Fedha zilizoletwa Kilimanjaro kwa ajili ya maendeleo ni nyingi na niwaahidi kwa niaba ya mwenyekiti wa CCM Taifa (Samia Suluhu Hassan) leo (jana) amerudi kutoka nchi nyingine (Brazil) kwa masilahi ya Taifa ile kauli ya Rais halali ni halali kweli kweli.
Kila siku anatafuta fedha za maendeleo kwa niaba yetu na hakuna kata ambayo hajaifikia kwa maendeleo kwa kipindi cha miaka mitatu aliyokaa madarakani, ni kwa imani kubwa mama anastahiki,” amesema Rabia.
“Niwaombe sana wabunge mlioko hapa na mpeleke salamu kwa wabunge ambao hawako hapa, kasi ya mitungi Kilimanjaro iongezeke, muwagawie wananchi mitungi ya gesi ya kupikia, na ninaomba na sitaki kusema agizo kwa sababu nina mamlaka ya kuagiza wabunge, lakini ninaomba muende mkapambane muwaongezee kina mama hapa mitungi ya gesi ya kupikia kwa umoja wenu,” amesema.
Aidha Rabia ambaye ni mlezi wa Kilimanjaro kichama, ametumia pia nafasi hiyo, kuwataka wanachama wa chama hicho kuwaepuka makada ambao wamekuwa wakisababisha matabaka na mitafaruku ya wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama.
“Kuna watu wana tabia ya kuleta mtafaruku na matabaka baina yetu, tuwapige vita, watu wote ambao wanatabia ya kutuchochea, nawaomba sana kama mlezi wenu, tuwapuuze, na sisi tuunge nguvu ya pamoja, tusimamishe Kilimanjaro yenye upendo, ambayo inasifika Tanzania nzima,” amesema Rabia.
“Chama ni familia, familia inaishi kwa malengo yanayofanana, malengo sawa, nia sawa lakini wanaunda nguvu ili kutekeleza jambo lao, tuunganisheni nguvu twende tukakitafutie Chama Cha Mapinduzi ushindi, tuheshimike kitaifa,” amesema.
Ametoa wito katika maeneo ambayo CCM pekee ndiyo imesimamisha wagombea, kutodharau kwenda kupiga kura ya ndiyo, kwa sababu kura hiyo ina ujumbe maalumu kuwa chama hicho kinakubalika.
“Pia twendeni tukafanye kazi na kila mmoja ajenge utamaduni wa kujiuliza kila siku hivi mimi leo ninafanya kitu gani cha kujiingizia kipato, mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, tuseme ukweli ukilala nani atakuletea chakula, usipojituma utatoboa kweli, usipokuwa na chako mwingine si atakunyanyasa, tujujengee utamaduni wa kupambana,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema chama hicho kimesimamisha wagombea katika vijiji vyote 519, mitaa 60 na vitongoji 2,257 katika Mkoa wa Kilimanjaro na kuwaomba wananchi kuwachagua viongozi wanaotokana na chama hicho ili kuchochea kasi ya maendeleo.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa maelekezo manne kwa wanachama wake kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Jumatano Novemba 27, 2024, ikiwemo kuanzisha ‘Operesheni Ondoa Mizigo’ Moshi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo katika viwanja vya Manyema Manispaa ya Moshi, Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema kuanzia jana Jumatano hadi kufikia Novemba 27, hakuna kulala.
“Tunaanzisha operesheni ya Ondoa mizigo Moshi, wale wanaogombea na watu wetu, chagua watu wetu, wale wanaogombea peke yao piga kura za hapana,” amesema Lema.
“Agizo la pili kila mahali ambapo tumedhulumiwa, watu wetu wameondolewa kibabe, chukueni mamlaka ya mtu huyo aliyeletwa kibabe, nendeni mkamtangaze huyo wa Chadema ndiye mwenyekiti wa wananchi, asifanye kazi za siasa, afanye za kijamii, mkienda kuzika mpelekeeni shada la maua, apeleke kwa niaba ya kijiji kizima,” amesema.
“Kuanzia leo (jana), Novemba 20 mpaka Novemba 27 wanachadema hakuna kulala, tunatembea mtaa kwa mtaa kila siku kuanzia asubuhi mpaka usiku kuomba kura, na tarehe 27, tunaenda kuwatoa watu wakapige kura mkishapiga kura mnasogea mita 100 mnapiga kambi, hakuna kuondoka, hakuna kuruhusu watu kufanya uhuni au vurugu siku ya kupiga kura,” amesema.