Mawakili wa Boni Yai wataka upelelezi uharakishwe, wajibiwa

Dar es Salaam. Upande wa utetezi katika kesi ya jinai inayomkabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai umeiomba Serikali ikamilishe upelelezi wa kesi hiyo kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.

Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, mfanyabiashara na mwanasiasa, anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Ombi hilo limetolewa leo Alhamisi, Novemba 21, 2024 na kiongozi wa jopo la mawakili wanne mshtakiwa huyo, Peter Kibatala, muda mfupi baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.

Wakili wa Serikali, Judith Kyamba amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi kesi hiyo bado unaendelea, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kyamba baada ya kutoa maelezo hayo, wakili Kibatala alidai kwa kuwa upande wa mashtaka wao ndio walimkamata na kumleta mahakamani mshtakiwa na kumshtakiwa, wanao wajibu wa kukamilisha kwa haraka upelelezi wa shauri hilo.

“Kwa kuwa wao ndio walimkamata na kuleta mahakamani, walipaswa wawe wamekamilisha upelelezi kwa wakati kwa kuwa sheria inaelekeza hivyo,” amedai Kibatala.

Akijibu hoja hizo, wakili Kyamba amedai hata wao wanaendelea kufanya uchunguzi ili kukamilisha kwa wakati shauri hilo.

Hakimu Kiswaga baada ya kusikiliza shauri hilo, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19, 2024 itakapotajwa na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).

Taarifa hizo zinasomeka kuwa:

 “Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo kuwa zinazowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

Ujumbe huo inasomeka kuwa:

“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu …, bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi,”

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, 2024 kujibu mashtaka yanayomkabili.

Hata hivyo, Boni Yai ana kesi nyingine ya jinai yenye mashtaka ya kama hayo, mahakamani hapo.

Related Posts